Picha ya Mwaka EPL 2012/13
Licha ya kutoka bila kombe msimu uliopita, Arsenal wamefarijika baada ya kutoka na Picha ya Mwaka ya Ligi Kuu ya England 2012/13.
Bodi ya EPL imeipa jina picha hiyo yenye wachezaji zaidi ya nusu ya wachezaji wa Arsenal wakishangilia bao kwa namna yake kuwa ni ‘Barclays Shot of the Season’.
Picha hiyo, kama inavyoonekana hapa, ilipigwa na Adrian Dennis wakati kikosi cha Arsenal kikishangilia bao, baada ya beki wao wa kati, Laurent Koscielny kusawazisha bao katika dakika za mwisho dhidi ya Manchester City msimu uliopita.
“Nimefurahishwa sana kupata ushindi huu kwa sababu haya ni mashindano yanayochukuliwa kwa umuhimu mkubwa zaidi miongoni mwa wapiga picha, ushindi huu umeniingizia maishani tunu nzima ya mchezo wenyewe,” akasema Dennis.
Jopo la majaji lilishirikisha Mwenyekiti wa Wahariri wa Picha wa Uingereza, Alan Sparrow, Mchambuzi wa Soka wa Sky Sports, Martin Tyler, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Soka Uingereza, Andy Dunn na mshindi wa msimu uliopita, Owen Humphreys.
Dennis alipata zawadi ya vifaa vya kazi yake vyenye thamani ya £5,000
KIFAA KIPYA KUJIUNGA ARSENAL SASA?
Arsenal wanatarajiwa kufanya tena shitukizo la usajili, kwa kumchukua mpachika mabao wa Romania, Ciprian Marica.
Mshambuliaji huyo aliye na timu yake ya taifa katika mechi dhidi ya Uturuki Jumanne hii kwa ajili ya kutafuta kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2014 ni mchezaji huru.
Taarifa kutoka Romania zinasema mchezaji huyo ana dalili kubwa za kucheza Ligi Kuu ya England (EPL), West Ham United wakimuwania, lakini uwezekano mkubwa ni kutinga Emirates.
Marica (27) aliondoka Schalke msimu wa kiangazi na amekuwa akihusishwa pia na klabu kadhaa kama Shakhtar Donetsk, Lazio na Inter Milan.
Kwa vile alikuwa mchezaji huru kabla ya dirisha kufungwa, anaweza kusajiliwa hata sasa, na wadau wengi wanamtupia macho. Ndiye aliwafungia bao Romania dhidi ya Hungary Ijumaa iliyopita.
“Marica ni mshambuliaji nguli ambaye tayari ana uzoefu katika soka ya Ulaya Magharibi kwa hiyo ni wazi kwamba klabu kubwa zitamfukuzia,” akasema wakala wake, Ioan Becali ambaye pia ndiye alikuwa na Vlad Chiriches aliyejiunga na Tottenham Hotspur hivi karibuni.
Becali alikwenda mbali zaidi na kusema kwamba dili la Marica kujiunga Arsenal lipo kwenye mchakato, akiongeza; “anakaribia kujiunga Arsenal, lakini inabidi tusubiri hadi wiki ijayo.”
Marica mwenyewe hajasema chochote, bali anatarajiwa kutoa neno baada ya mechi muhimu ya Romania dhidi ya Uturuki ya kundi D. ana rekodi nzuri ya kufunga mabao kwa nchi yake, akiwa na mabao 22 katika mechi 63.
Comments
Loading…