*Polisi Moro, Ruvu Shooting washuka daraja
*Toto, Mwadui, Majimaji, African Sports juu
Ligi Kuu ya Tanzania imefikia hatima, ambapo kubwa lililokuwa likisubiriwa ni timu gani zingeshuka daraja, nazo zimetambulika kuwa ni Polisi Morogoro na Ruvu Shooting.
Ubingwa tayari ulikuwa umenyakuliwa mapema na Yanga na nafasi ya pili ikaenda kwa Azam wiki iliyopita baada ya kuwafunga Yanga walipocheza kwenye Uwanja wa Taifa uliokuwa umetota maji huku mvua ikinyesha.
Matokeo ya mechi za mwisho, ambapo timu zote 14 zilijitupa uwanjani, ndiyo yamezihukumu Polisi na Ruvu Shooting. Polisi walichezea kichapo cha 1-0 kutoka kwa Mbeya City jijini Mbeya, wakati Ruvu Shooting waliadhibiwa kwa idadi hiyo hiyo ya mabao na Stand United.
Polisi wanashuka daraja wakiwa ndio tu wamecheza msimu mmoja walipopanda sambamba na Ndanda wa Mtwara na Stand United wa Singida. Polisi wamemaliza ligi wakiwa mkiani na pointi 25 tu.
Ruvu Shooting waliokuwa wakifundishwa na Tom Olaba kutoka Kenya wamejikuta katika hali ya ajabu, kwani kabla ya mchezo walikuwa katika nafasi ya tisa wakiwa na pointi 29 na walihitaji pointi moja tu ili wabaki juu.
Vinginevyo wangefunga mabao manne hata wakapoteza mechi wangebaki juu maana wanafungana pointi na Mgambo. Inaelekea bahati haikuwa yao na msimu ujao wasikilizaji watamkosa msemaji wao aliyekuwa na makeke, Masau Bwire.
Baada ya Yanga kuwa wakigawa dozi ndani na nje ya nchi, Bwire kabla ya kukutana nao alijigamba kuwa wangewatuliza na kuwafunga, akawafananisha na lori la mkaa lililokatika breki linaloserereka mlimani, ambapo watu walishindwa kuweka vigingi vyenye nguvu, akisema Ruvu wangewamaliza, lakini wakaishia kucharazwa 4-0.
Timu zilizoepuka kushuka daraja katika mechi za mwisho kwa kuwa zilikuwa zikichungulia huko ni pamoja na Mgambo na Prisons waliomaliza wakiwa na pointi 29 sawa na Ruvu walioshuka.
Msururu wa timu ambazo zingeweza kukumbana na balaa la kushuka daraja ulikuwa mrefu, kwani Stand United, Ndanda, Mtibwa Sugar na Ruvu JKT zingeweza kushuka kwa sababu zimemaliza zikiwa na pointi 31 na kadhalika Kagera Sugar wangeweza kukionja kikombe hicho kwa sababu wamemaliza wakiwa na pointi 32 ambazo kama Ruvu Shooting wangeshinda mechi ya mwisho wangezifikia.
Timu pekee zilizokuwa salama ni Yanga waliomaliza wakiwa na pointi 55, Azam 49, Simba 47 na kwa kiasi fulani Mbeya City waliopata kuchungulia kaburi kabla ya kujizatiti na kufikisha pointi 34 sawa na Coastal Union.
Msimu wa 2015/16 utashuhudia timu mpya zilizopanda daraja kutoka Ligi Daraja la Kwanza hadi Ligi Kuu, ambazo ni Toto Africans ‘Watoto wa Yanga’ wa Mwanza, Mwadui wa Shinyanga, African Sports ‘Wana Kimanumanu’ wa Tanga na Majimaji kutoka Songea na kufanya Ligi Kuu kuwa na timu 16.
Comments
Loading…