Ni Liver na Man City Ulaya
*Arsenal nje kwa mara ya kwanza miongo miwili
*Chelsea kwa raha zao tele wakabidhiwa mwali
Pazia la Ligi Kuu ya England (EPL) limefungwa kwa Chelsea kukabidhiwa mwali, huku timu mbili za kuungana na matajiri hao wa London na Tottenham Hotspur kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) wakijulikana.
Ilikuwa wikiendi ya kuvutia, timu zote 20, zikiwamo zile zilizoshuka daraja zikiingia dimbani kumenyana kumaliza msimu wa 2016/17, ambapo kulikuwapo mabao mengi, ikiwa ni pamoja na timu kuitungua nyingine kwa mabao saba.
Antonio Conte alimaliza msimu wake wa kwanza Chelsea kwa kutwaa ubingwa, ambapo Jumapili hii alimalizia kwa kukutana na David Moyes wa Sunderland walioshuka daraja, akawacharaza 5-1.
Manchester City waliokuwa wakihitaji walau sare kujihakikishia nafasi UCL, waliifanya kazi hiyo kwa nguvu na kufanikiwa kuwafunga Watford 5-0 huku Liverpool waliokuwa wakihitaji ushindi ili kuondokana na bughudha za Arsenal, waliwakanyaga Middlesbrough 5-0. Nao wameshuka daraja.
Arsenal walihitaji ushindi wakicheza dhidi ya Everton na wakashinda 3-1 lakini uvukaji wao kwenda UCL ungetegemea na Man City kupoteza na Liver kwenda sare au kupoteza, lakini haikuwa hivyo.
Hali hiyo imehitimisha ushiriki wa Arsenal UCl ambao umekuwa wa miaka 20 mfululizo chini ya Wenger. Mfaransa huyo amedai kwamba utata juu ya hatima yake klabuni hapo kama kocha ndio ulisababisha Arsenal wakafanya vibaya.
Mkataba wake unamalizika kiangazi hiki na uamuzi wa kuendelea au la utatolewa na Bodi ya Wakurugenzi baada ya fainali yao na Chelsea kwenye Kombe la FA Mei 27. Kutofuzu kwao kunaongeza wasiwasi iwapo wachezaji wao nyota, Alexis Sanchez na Mesut Ozil watabaki. Wanakaribia kumaliza mikataba yao Emirates. Arsenal msimu ujao watacheza Ligi ya Europa.
Kocha wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson amemtetea Wenger ambaye alipata kuwa hasimu wake, akisema anawashangaa washabiki wa Arsenal wanaoeneza kampeni za kumtaka aondoke, akisema amefanya mengi kwa klabu hiyo kwa kipindi cha miaka 21, akiwabadilisha kabisa walivyokuwa.
Ligi ilihitimishwa kwa Burnley waliokuwa nyumbani kufungwa 2-1 na West Ham, Hull walioshuka daraja kumaliza vibaya zaidi kwa kunyukwa 7-1 na Spurs, Leicester wakatoshana nguvu na Bournemouth, Manchester United wakawafungwa Crystal Palace 2-0, Southampton wakiwa nyumbani wakalala 1-0 mbele ya Stoke na Swansea wakacheka kwa kuwafunga West Bromwich Albion 2-1.