KUMZUNGUMZIA mchezaji yeyote lazima uwe mwangalifu na kugawanya vizuri mambo makuu matatu; uimara wake, udhaifu wake na kitu cha ziada. Katika hili tunaweza kutumia mtazamo wa kocha Marcelo Lippi na Roberto Mancini wote wa Italia. Mwaka 2006 kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Ujerumani timu ya Taifa ya Italia iliibuka bingwa. Katika kikosi chao kulikuwa na mshambualiaji mrefu Luca Toni ambaye katika historia ya uchezaji wake amepachika zaidi ya magoli 300. Marcelo Lippi alipomteua Luca Toni kuwa mshambuliaji namba moja kwenye kikosi chake alitamka bayana kuwa anahitaji mchezaji wa eneo hilo ambaye atampa kitu cha ziada kwenye kutafuta ushindi. Luca Toni alibarikiwa urefu, nguvu na maarifa lakini hakuwa mjanja kama Filipo Inzaghi ambaye mara nyingi alikuwa akionekana kwenye matukio ya kustaajabisha na kupachika mabao. Tofauti yao ni kwamba Luca Toni alikuwa na uchezaji kama Didier Drogba, anaweza kupambana na mabeki wa nguvu yaani mabavu na kustahimili viatu anavyopigwa na mabeki, lakini alikuwa mahiri kwenye mabao ya vichwa, mashuti na wakati mwingine kutoa pasi nzuri. Pia Roberto Mancini kwa nyakati tofauti amepata kumwelezea mshambuliaji Mario Balotelli kama mchezaji mwenye kitu cha ziada ambaye anaweza kukupa ndani ya dimba ikiwa atatulia.
Kimsingi makocha wengi wanatamani kuwa na wachezaji wale wenye uwezo wa kuwapa vitu adimu katika timu yake. Novatus si mchezaji wa daraja la Luca Toni wala Mario Balotelli. Wala hachezi nafasi ya washambuliaji hao wawili. Lakini ni mchezaji ambaye anaweza kumpa kocha unafuu mkubwa pale anapohitaji kufanya mabadiliko ya mchezaji au kimbinu. Kwa mfano kwenye kikosi cha Arsenal kulikuwa na kiungo mkabaji Mathieu Flamini.

Kuna wakati Arsenal chini ya Arsene Wenger ilikosa beki wa kushoto baada ya waliokuwepo kuumia. Wenger hakwenda sokoni kusajili beki mpya, badala yake alimpa jukumu hilo Mathieu Flamini. Alimbadilisha nafasi tu na akafanya vyema kwenye kikosi chake. Ilikuwa Arsenal yenye kikosi cha kuunga unga kwa maana ya wachezaji kuchezeshwa nafasi zisizo zao, lakini wakafanya vizuri sana. pale Chelsea alikuwa mshambuliaji mmoja matata sana, Mateja Kezman. Kwa asili Mateja Kezman alikuwa namba 9 lakini alipowasili Chelsea ya Jose Mourinho alikuwa akipangwa hata winga wa kulia akipokezana na Damian Duff na Arjen Robben kulingana na mbinu za kocha wao na mchezo husika.
Ukiachana na wachezaji wa nje ya nchi tugeukie wale wa Timu ya Taifa ya Taznzania. Labda tukumbushane, unamkumbuka Amir Maftah wa Yanga, Mtibwa na timu za Taifa kuanzia vijana hadi wakubwa? Huyu alikuwa winga, lakini aliweza kucheza nafasi ya beki wa kushoto. Unamkumbuka Fred Mbuna wa Yanga na timu za Taifa? Huyu alikuwa na uwezo wa kucheza namba 9 na beki wa kulia. unamkumbuka Henry Joseph wa Simba na timu za Taifa? Huyu alikuwa kiungo namba 6 mwenye uwezo wa kucheza kama kiungo wa pembeni yaani namba 7 (ambayo kwa asili ni winga), lakini makocha wanapotaka kujihami wanatumia viungo kama yeye kucheza upande huo. Unakumbuka Erasto Nyoni?
Huyu ni mchezaji wa aina yake kutokea Tanzania. Erasto Nyoni alikuwa na uwezo wa kucheza nafasi ya beki zote yaani namba 2, 3, 4 na 5. Pia Nyoni alikuwa na uwezo wa kucheza namba 6 kwa ufasaha. Kwahiyo utaona Erasto Nyoni ndiye alikuwa na mchezaji mwenye vitu vingi vya ziada katika kikosi cha Simba au Taifa Stars. Ukikumbuka bao pekee walilofungwa Burkina Fasso kwenye dimba lao la nyumbani mjini Ouagadougou? Basi lilipachikwa na Erasto Nyoni. Katika mazingira hayo wachezjai wa aina yake wanakupa kipaji cha ziada kuelewa mchezo na kukubali kutumikia nafasi wasiyozoea.
Kikosi cha Taifa Stars kwa sasa kina wachezaji wachache sana wenye uwezo wa Erasto Nyoni. Ni ule uwezo wa mwalimu kuamua kumpanga mchezaji katika nafasi nyingine tofauti na aliyozoea kisha akafanya vizuri. Ni mchezaji ambaye anao uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja, na inategemea mwalimu wake anataka nini kutoka kwake kulingana na mchezo husika. miongoni mwa nyota wenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi katika kikosi cha sasa ni Kibu Dennis. Unaweza kumpanga Kibu Dennis katika nafasi ya winga wa kulia akakupatia vitu adimu na kuisaidia timu.
Kisha unaweza kumpanga katika nafasi ya winga wa kushoto pia akaleta vitu adimu ambavyo vitamfanya mwalimu wake azidi kuumiza kichwa ni wapi atampanga nyota wake. hali kadhalika Kibu Dennis anaweza kucheza nafasi ya mshambuliaji yaani namba 9, na akawa anapachika mabao.
Tofauti ya Yusuf Kagoma na Novatus
Katika sifa hizo ndizo anakuja Novatus Dismas, nyota wetu wa Kimataifa ambaye ana sifa zaote za Erasto Nyoni. Baadhi ya mashabiki huwa wanafurahishwa kwa mechi fulani anapopangwa nafasi ya beki, lakini wapo ambao wanasema hawaridhishwi hata kucheza mbele ya Yusuf Kagoma. Tofauti kati ya viungo hawa wawili ni ufanisi kulingana na nafasi. Yusuf Kagoma hachezi kama Erasto Nyoni, kwa sababu nafasi yake anayotumikia ni namba 6. Halafu kuna wengine wanaweza kucheza nafasi hiyo na nyinginezo.
Novatus anaweza kucheza namba 3, 4, 5, 6 kulingana na mahitaji ya mwalimu. Kwa maana hiyo mwalimu Adel Amrouche alipokuwa akimpanga kama beki namba nne alikuwa ameona maarifa ya zaida aliyonayo nyota wake. lakini kwa aisli Novatus ni kiungo namba 6 mwenye uwezo wa kucheza nafasi za beki wa namba 4, 5, na beki wa kushoto. Katika machaguo ya mwalimu mchezaji wa aina hiii anapata nafasi zaidi kuliko mwingine.
Ukimhitaji Novatus kucheza beki wa kushoto fahamu atatumikia vyema zaidi. Ukihitaji Novatus acheze beki wa kati nayo atatumikia vizuri. Kana kwamba haotisho katika klabu zake Ulaya huwa wanatumia kama winga wa kushoto na anafanya kazi yake vizuri sana. huyu ni mchezaji mwenye ufanisi katika maeneo mengi na unahitaji kuwa naye katika kuimarisha uwezo wa timu. Ni sababu hiii Novatus atacheza sana Taifa Stars kwa sababu ana kitu cha ziada kama Erasto Nyoni, lakini anamhitaji Yusuf Kagoma ili kuongeza ushindani na maarifa yake kunolewa zaidi.
Comments
Loading…