Wiki chache zilizopita Tanzania Sports iliwatangazia habari za kifo cha mwanasoka maarufu wa Brazil, Carlos Alberto aliyepata mstuko wa moyo akiwa na miaka 72. Carlos Alberto alikuwa nahodha wa timu maarufu iliyotwaa kombe la dunia Mexico City mwaka 1970.
Anajulikana kwa bao linalohesabiwa kuwa kali na bora kuzidi yote katika historia ya fainali za kombe la dunia baada ya kupewa pasi kutoka kwa Pele. Pele alipokea mpira huo kutoka kwa Jairzinho na badala ya kukimbilia kufunga akasubiri wakati muafaka kabla ya kumpigia pasi Carlos Alberto aliyeweka gozi kimiani. Brazil ilishinda Italia 4-1.
Marehemu Carlos Alberto aliwahi kuulizwa nani alikuwa mchezaji mzuri kati ya Pele na Mane Garrincha- majabali wa Brazil kama walivyo Lionel Messi na Cristiano Ronaldo sasa. Carlos Alberto: “Pele alikuwa mchezaji aliyekamilika. Garrincha ana kipaji cha kuzaliwa…”
Haya ni maneno yanayotuanzishia hoja yetu leo.
Miezi michache iliyopita wakati nikitathmini mustakabal wa EPL hapa England nilisema moja ya tofauti kati ya Mourinho na Wenger iko katika namna wanavyonunua wachezaji. Falsafa yake Wenger ni ujenzi wa timu na wachezaji ilhali mwenzake Mourinho hununua wachezaji walioshakamilika na lengo lake ni kushinda vikombe siyo kujenga timu.
Lengo la makala haya lakini si kuzungumzia ukocha bali maana ya mchezaji aliyekamilika. Katika riadha wapo wanariadha wanaocheza katika vikundi au timu mathalani ngalawa, mpira wa kikapu, nyavu, mikono, nk. Au wanaocheza peke yao yaani mmoja mmoja: wakimbiaji, wapiganaji masumbwi, waogeleaji, warukaji, watupa tufe, nk. Katika makundi haya mawili huzuka wanariadha waliojijenga katika fani nyingi na ambao wameganyika katika michezo mitano, saba, nk. Kwa wanawake maarufu ni Heptathlon.” Hepta” maana yake ni saba kwa Kiingereza na “athlon” ni ushindani kwa Kigiriki.
“Triathlon” huchanganya michezo ya aina tatu katika masafa marefu yaani kuogelea, kukimbia na kuendesha baiskeli.
Tukizungumzia soka, mchezaji aliyekamilika ni yule anayeweza vipengele mbalimbali vya mchezo huu, yaani hewani yaani kutumia kichwa- chenga, kutawala mpira, ushirikiano na wenzake, kuchangia kufunga mabao au yeye mwenyewe kufunga, mwepesi kukimbia na akiwa katulia nk.
Kidesturi ufundi huu wanao wachezaji wa nafasi ya kati (midfield) – viungo vya timu. Mwanasoka wa kwanza kuchukua taji hili alikuwa Pele au Edson Arantes do Nascimento. Pele alikuwa kiungo namba kumi. Kuanzia kwake ndiyo namba hiyo imekuwa maarufu kwa wachezaji kama Diego Maradona, Zinedine Zidane, Lionel Messi, Wayne Rooney nk.
Pele alimudu nafasi zote ikiwepo ugolikipa akiwa timu ya Santos. Mbali na mpira alipenda riadha, kuruka viunzi, kuogelea nk. Kama mfungaji aliorodhesha mabao mengi kuliko wenzake wote wa enzi zake. Alisifika kwa nidhamu, hakutumia dawa za kulevya au ulevi kama mwenzake maarufu, Mane Garrincha.
Pele alitimia kiasi ambacho serikali ya Brazil ilimwita hazina ya taifa na haikuruhusu kabisa auzwe nje. Kwa hiyo Pele hakuwahi kucheza mpira Ulaya, hadi alipostaafu na kununuliwa na Cosmos ya Marekani. Yeye na bondia mashuhuri Muhammad Ali wanaitwa wanamichezo bora wa karne ya 20.
Miaka mingi umekuwepo ubishi kuwa nani bora kati ya Diego Maradona na Pele. Watetezi wake Maradona hudai, Maradona alishinda kombe la dunia 1986 peke yake.. Hudai Pele alitwaa vikombe hivyo mara tatu 1958, 1962 na 1970 kutegemea kocha na timu nzuri zilizokuwa na wachezaji wazuri. Upande wa Pele hutetea namna alivyokuwa mshirika na wenzake, alivyoweka ufundi wake katika timu badala ya kufanya kila kitu peke yake.
Maradona hakuwa na nidhamu na utumiaji wake wa dawa za kulevya ulimfanya afukuzwe kombe la dunia la 1994. Kutokana na uhakiki huu Pele amekuwa mfano na kipimo cha mchezaji aliyetimia. Leo tunao viungo mashuhuri Cerc Fabregas, Mezut Ozil, Lionel Messi, Zinedine Zidane nk.