MABINGWA wa Ngao ya Jamii, Simba wametangaza kuachana na winga wao Peter Banda raia wa Malawi. Uamuzi wa Simba umekuwa huku ikiwa imeshacheza mechi mbili za Ligi Kuu Tanzania Bara. Peter Banda anafuata nyayo za wachezaji wengine ambao wemetupiwa virago klabuni hapo. Hivi Sasa mjadala mkubwa ni kuhusu kuondoka winga huyo huku kukiwa na mgawanyiko miongoni mwa mashabiki wa soka na Simba.
TANZANIASPORTS inaangazia masuala muhimu ambayo yamechangia Nyota huyo kung’olewa katika klabu ya Simba.
USHINDANI
Simba ni klabu kubwa, inawindwa na nyota wengi wa Kimataifa ambao wanatamani kutangaza soka Lao kupitia timu hiyo. Idara zote za klabu hiyo kumekuwa na ushindani mkali ambao wachezaji wachache wanaweza kupenya katika kikosi cha kwanza. Peter Banda akiwa na uzoefu wa kukaa klabuni hapo, alikuwa akiwekwa benchi hata na winga Msenegali Pape Sakho. Ushindani wa eneo analocheza ni sababu nyingine iliyomfanya Nyota huyo akubali kuondoka Simba. Msimu huu Simba imemrudisha winga Louis Miquissone ambaye amekuja kuleta changamoto katika eneo hilo na kuifanya nafasi ya Peter is kuwa finyu.
MAJERAHA
Peter Banda ni mchezaji ambaye alikuwa anapata majeraha mara kwa Mara hivyo kuathiri mwendelezo mzuri wa kipaji chake. Ni mchezaji ambaye ana kila sifa ya kwa winga hatari lakini bado hakuwa ameonesha mwendelezo tokana na majeraha mara kwa mara. Hii ni miongoni mwa sababu zilizoifanya Simba ichukue hatua za kuachana naye.
MUDA NI MWINGI
Simba wamefanya uamuzi sahihi wa kuachana na Peter Banda “The Wonder Kid” kwa sababu wamempa muda mrefu ili adhihirishe thamani na kipaji chake. Ikiwa baadhi wanapinga uamuzi huo basi wanapaswa kujiuliza ni muda upi sasa na namba anayocheza wachezaji ni wengi. Kwa muda aliokaa Simba ni somo tosha kwake kutafuta changamoto mpya kwa vile akiwa Simba alikuwa mkaaji wa benchi hali ambayo inadumaza kipaji chake.
UPANA WA KIKOSI
Kocha Robertinho anao wachezaji wengi wa kuwatumia katika eneo la winga wa kulia au kushoto. Kibu Dennis, Luis Miquissone na Osamba Onana ni miongoni mwa wachezaji wanaoweza kucheza nafasi za ushambuliaji wa pembeni. Peter Banda alishindwa mbele ya Pape Sakho. Pia akafeli mbele ya Kibu Dennis, huku Simba ikiwa imeongeza wachezaji wapya kikosini hali ambayo inamnyima nafasi winga huyo.
MKOPO NA KUKATA TAMAA
Baadhi ya taarifa za ndani za klabu ya Simba zinaeleza kuwa nyota huyo hakuwa tayari kwenda kucheza klabu nyingine kwa mkopo. Hii ina maana Peter Banda huenda alitambua shughuli iliyokuwa mbele yake ilikuwa kubwa na kuna uwezekano alishakata tamaa ndio maana hakutaka kucheza kwa mkopo katika klabu nyingine hapa nchini.
MFUMO KUMKATAA
Kila kocha anahitaji wachezaji ambao watampa uwezo wao wote hata pale wanapochezeshwa sehemu tofauti. Kibu Dennis anaweza kucheza nafasi ya winga wa kulia,kushoto na mshambuliaji. Wakati Peter Banda nafasi zake ni mbili tu yaani winga wa kulia na kushoto. Ikiwa kocha anataka kutengeneza mbinu ya kujilinda ni lazima atamtumia Kibu Dennis ambaye hufanya kazi zote mbili; kusaidia ulizi na kushambulia.
Lakini kwa kuangalia kipaji, Peter Banda ana kipaji kizuri lakini kiwango chake kinakosa mwendelezo tu.
KUJIHAKIKISHIA NAMBA
Kwa kipindi chote alichocheza Simba, Peter Banda hakuwa na uhakika wa namba kikosini. Mara kadhaa amecheza mechi za Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika, amekuwa mchezaji wa kucheza leo, kisha kesho benchi, au keshokutwa kusota benchi muda mrefu. Hivyo kipaji chake kinakuwa hakitumiki vizuri. Sababu hata alipopewa nafasi bado hakuwaridhisha Walimu wake.
Comments
Loading…