Nikiwa njiani kutoka Morogoro kulikokuwa kukifanyika mashindano yaTaifa kutafuta klabu bingwa nchini mpira wa wavu napokea simu kutoka kwa Mwinga Mwanjala Afisa Utawala wa Kamati ya Olimpiki Tanzania akinieleza rafiki yako Erasto Zambi hatuko naye tena amefariki usiku wa leo.
Ukweli nilihuzunika sana kwa taarifa ile. Kilichohuzunisha zaidi ni yale masihara niliyokuwa nikimtania kila tukikutana. Ni siri gani waliyokuwa nayo kwani toka waondoke hatujaambulia hata medali ya bati . Ni miaka 32 sasa kuna nini. Kwa masihara naye alipenda kusema hamtaki kuja kuniona . Wazee tunaondoka hamtaki kuja kufahamu siri.
Erasto Zambi ana historia ndefu kimichezo kwani alitumia zaidi ya nusu ya maisha yake katika michezo.
Miongoni mwa wanafunzi wake kimichezo ni pamoja na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete katika mchezo wa Basketball.Zambi alipenda sana kusema kuwa Kikwete alikuwa mwanafunzi wake bora kwani hata walipokuja walimu na wachezaji bora wa Marekani kama vile Kareem Al Jabaar walimsifu sana Jakaya.
Erasto Zambi alizaliwa mwaka 1938 mkoani Mbeya. Akiwa mwalimu wa michezo aliajiriwa na Shirika la Elimu Kibaha mapema miaka ya sitini. Shirika la Elimu Kibaha ndio Shirika pekee wakati ule la msaada toka nchi masikini za Scandanavia wakati ule kwenda kwa nchi masikini Afrika kwa maendeleo.
Sina hakika Shirika la Elimu Kibaha lilienziwa vipi katika miaka hamsini ya Uhuru wa Tanganyika
Hata hivyo mapema miaka ya sabini Erasto Zambi alijikuta akiajiriwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam UDSM kama mwalimu wa michezo hapo chuoni. Wanafunzi wengi waliopitia hapo chuoni akiwemo Mwenyekiti wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF Leodgar Tenga wamepitia katika mikono yake.
Binafsi kamwe sitomsahau kwa kunifungua macho katika ulimwengu wa michezo. Alikuwa ni Erasto Zambi aliyehakikisha Tanzania inakuwa mwanachama wa Shirikisho la Mpira wa Wavu Duniani FIVB mapema miaka ya themanini Tanzania ilijiunga na Shirikisho la Mpira wa Wavu FIVB 1984.
Zambi alitoa kila aina ya msaada ikiwemo kulipa ada kwa Shirikisho hilo kuhakikisha Chama cha Mpira wa Wavu nchini TAVA kinapata utambulisho wa kimataifa. Kama vile haitoshi Zambi alitoa msaada mkubwa kwangu kwa kuhudhuria mafunzo mbali mbali ya uongozi wa michezo kupitia Kamati ya Olimpiki Kimataifa International Olympic Committee kule Olympia Greece mwaka 1984.
Alipenda sana nijifunze mengi kiuongozi wakati ule
Zambi alinishirikisha pia katika mafunzo ya kwanza nchini mwaka 1997 kutafuta Wakurugenzi wa mafunzo ya Utawala wa michezo Sports Administration chini ya Kamati ya Olimpiki Duniani.
Watanzania wawili ikiwa pamoja na Ndugu Samson Kayobyo tulibahatika kufanikiwa kufaulu mafunzo hayo. Ingawa leo Tanzania ina watu zaidi ya kumi kwenye Tanzania Olympic Academy bado Erasto Zambi ana mchango mkubwa unaohitaji kuenziwakatika uanzilishi wa Academy hiyo.
Mchume mimi nimetembelea karibu nchi zote Duniani alipenda kusema mara nyingi tunapokutana .
Ni kweli sina ubishi na hilo kwani amekuwa Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania kwa karibu miaka 27.
Naamini wanamichezo kwa ujumla tutafuata yale yote mema alioyatenda na kumuenzi .
Mungu ailaze roho ya marehemu Zambi mahali pema peponi.
Makala hii imeandikwa na Muharame Mchume
Comments
Loading…