Nigeria wamaliza mgomo
Nigeria wamemaliza mgomo wao juu ya posho na wanafanya mazoezi makali kwa ajili ya kuwakabili Ufaransa Jumatatu hii.
Wamerejea mazoezini kwa ari mpya baada ya Rais Goodluck Jonathan kuingilia kati mzozo baina ya wachezaji na Shirikisho la Soka la Nigeria (NFF).
Wachezaji wanataka kila mmoja dola 30,000 wakati NFF linataka kuwapa dola 15,000 kila mmoja hadi hatua waliyofikia ya 16 bora.
Wachezaji wote 22 waliopo kwenye kikosi wamekuwa wakijifua wikiendi yote, ambapo Victor Moses aliyekuwa kando naye ameingia baada ya kupata ahueni ya majeraha.
Hata hivyo kiungo Michael Babatunde ndiye pekee hakufanya mazoezi baada ya kuumia kwenye mechi za makundi.
Rais Jonathan aliingilia kati, akazungumza kwa simu na kocha Stephen Keshi na nahodha Joseph Yobo kuwahakikishia kwamba fedha zao zitalipwa hivyo wajitume kwa ajili ya mechi ya Jumatatu ili wapate nyingi zaidi.
“Tupo vizuri kisaikolojia na imara sana kiufundi kwa ajili ya mechi ya Jumatatu. Hatujali tunacheza na timu ipi; iwe ni Hispania katika Ligi ya Mabara au Liberia katika mechi ya kirafiki, nimekuwa nikiwaambia vijana kwamba ushindi ni lazima,” anasema Keshi.
Hii ni mara ya kwanza kwa timu mbili za Afrika kusonga mbele kwenye hatua hii, ambapo Algeria nao wanajipanga kuchuana na Ujerumani.
Iwapo Nigeria na Algeria watashinda mechi zao, watapambana wenyewe kwa wenyewe kwenye robo fainali katika dimba maarufu la Maracana.
Wachezaji wamekuwa hawazungumzi na vyombo vya habari tangu Alhamis mzozo wa posho ulipozuka.
Walifuata nyanyo mbaya za Cameroon na Ghana, ambapo matatizo yao yalimalizwa lakini wakaishia kutolewa kwenye mashindano.
Takwimu zinaonesha kwamba Nigeria walicheza na Ufaransa 2009 ambapo Nigeria walishinda 1-0 mfungaji wa bao akiwa Joseph Akpala
Comments
Loading…