*Watwaa kombe baada ya miaka 14
Nigeria wamekata kiu ya miaka 14, kwa kutwaa kwa mara ya tatu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa kuwashinda Burkina Faso kwa bao 1-0.
Goli zuri la Sunday Mba limetosha kuwarejeshea ufalme Nigeria, na kuamsha nderemo na vifijo Afrika Kusini na nyumbani Nigeria.
Stephen Keshi ameweka rekodi ya kutwaa kombe hilo mara mbilo, kwanza kama mchezaji na mwaka huu akiwa kocha.
Super Eagles walianza kwa kutawala mchezo, pakawa na kosakosa na dakika tano kabla ya mapumziko, Mba alinasua mpira kutoka kwa mpinzani Mohamed Koffi na kuupachika kwenye kona ya juu ya lango.
Burkina Faso nusura wasawazishe kupitia kwa Wilfried Sanou, kama si kazi ya ziada ya golikipa Vincent Enyeama aliyeokoa kwa ncha ya vidole vyake.
Katika mechi nzuri iliyohudhuriwa na Rais Jacob Zuma katika Uwanja wa FNB Soccer City jijini Johannesburg, Nigeria walionekana dhahiri kustahili ushindi kwa jinsi walivyojituma.
Hata hivyo, wangeweza kupata ushindi mnono zaidi, kama si umaliziaji mbaya na wakati mwingine kazi ya ziada ya mabeki na golikipa wa Burkina Faso.
Hata hivyo, Burkina Faso wanaondoka Afrika Kusini wakiwa vifua juu, kwa sababu ushindi wa pili ndiyo mafanikio makubwa zaidi kisoka katika historia ya nchi yao.
Keshi amewadhihirishia waliokuwa wakimpinga kwamba alikuwa sahihi, kwanza kwa kukubali uteuzi akiwa mzalendo, na pili kuacha baadhi ya majina makubwa wadau waliyotaka yajaze kikosi hicho.
Wachezaji wake Efe Ambrose, Victor Moses,
Ideye Aide Brown, John Obi Mikel na Uche waling’ara.
Hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 21 kwa kocha mweusi kuiwezesha nchi yake kutwaa kombe hili. Yeo Martial wa Ivory Coast ndiye alikuwa wa mwisho kulitwaa mwaka 1992.
Nigeria walitwaa kombe hili mwaka 1980 na 1994 wakati kabla ya mashindano haya ya 29 ya AFCON, Burkina Faso hawakuwa wamepata kushinda hata mechi moja nje ya ardhi yao.
Comments
Loading…