WAHENGA walipata kusema; ‘heri nusu kitumbua ulichonacho mkononi kuliko kitumbua kizima kilicho dukani’.
Kauli hii inafaa kusambaa katika akili ya mwanamuziki wetu Nasib Abdul, maarufu kama Diamond Platnumz.
Yeye ni mwanamuziki kijana ambaye ana kila sababu kujivunia hatua anazopitia maana ni wanamuziki wengi wa Tanzania wameshindwa kufikia hatua hiyo.
Kwa miaka mingi hatukuweza kuwa na rekodi yoyote katika tuzo za MTV bali AY na Black Rhino ndio miongoni mwa wanamuziki waliotupa sifa kubwa kwa kuteuliwa kuwania tuzo za Kora na Channel O.
Hatua hii ilikuwa kubwa zaidi, na kila mmoja anaweza kujivunia.
Wanamuziki wetu wa kizazi kipya wanajitahidi kila njia kufanya mambo mazuri, lakini wale wenye malengo zaidi ndio hufika mbali.
Kuna kushirikisha na wanamuziki wa nje ya nchi ambao kwa namna moja au nyingine wameonesha kukubali kazi za wanamuziki wetu.
Mwanzoni mwa miaka ya 2000 kulikuwa na kundi la Gangwe Mob.Hili lilifanikiwa kushirikishwa wimbo mmoja na kundi la ‘Necessary Noise’ likiwa na ‘Nazizi na Wyre’.
Tunafahamu kazi nzuri ilitengenezwa na ‘Gangwe Mob’ wakiwa chini ya Inspekta Haroun na Luteni Kalama wakiwa bega kwa bega na na zazi na Wyre.
Walitengeneza wimbo mzuri tu, ukavutia washabiki wa Kenya na Tanzania.
Ilikuwa hatua nzuri na alama kwamba Bongofleva ilikuwa inasogea mbele kidogo.
AY kwa upande wake alifanya juhudi hizo, akawaunganisha pia wanamuziki wa Bongo Fleva na Wakenya.
AY alituletea Maurice Kirya wa Uganda kisha wakatengeneza wimbo wa ‘Binadamu’.
Bamboo ni mwanamuziki ninayempenda sana na anatoka Kenya. Ni miongoni mwa wanamuziki waliofanikiwa kupenya soko la muziki nchini Kenya pamoja na Tanzania.
Vituo vya redio na televisheni vilimpa wakati mzuri zaidi kutoka na nyimbo zake. Bamboo ana washabiki hapa Bongo, ni daraja la mafanikio ya wanamuziki wa Bongofleva pia Lady Jadee aliungana na ‘Mafikizolo’ kutengeneza wimbo mzuri tu.
Kundi zima la East Coast Team, chini ya King GK nalo lilianza hatua kama hizo kwa kuhakikisha wanarekodi nyimbo zao kwa maprodyuza kama wa Ogopa Dj’s pamoja na watengenezaji wa video kutoka Uganda.
Hatua hizi zinaweza kuwa moja ya mafanikio makubwa kimuziki.
Yote hayo yalikuwa mambo makubwa kwa wanamuziki wa Tanzania, Kenya na Uganda. Lakini kuwania tuzo za MTV ni kubwa zaidi.
Napenda kumwita Nasib Abdul kuliko Diamond Platnumz.
Yeye amefanikiwa kufika mahali ambapo kila mwanamuziki wa Tanzania anatamani.
Kuanzia wimbo wa ‘Mbagala’ hadi kwenda MTV. Wqkati huu nadhani Diamond anatakiwa kujisifu. Pia ni wakati wake kuona kuwa anaweza kutamba katika majukwaa ya kimataifa kama atafanya kazi nzuri.
Katika mashindano yoyote kuna kushindwa na kushinda. Mwanamuziki unapochaguliwa kuwania tuzo; iwe MTV Base, MTV Afrika/Mama au yoyote ya nje ya nchi yako ina maana kazi zake ni bora na zinawekwa daraja moja na nyingine za kimataifa.
Diamond anapaswa kujivunia nafasi hii. Anapaswa kutembea kifua mbele. Anapaswa kuringa. Anapaswa kutamba kila hatua aliyofikia pale jukwaani.
Kwa mapromota makini kuteuliwa kwa Diamond kuwania tuzo za MTV ni faida kubwa kibiashara na muziki wao. Nadhani Diamond atajiendeleza zaidi ili awe bora kabisa kimataifa kwa kila namna na anyakue tuzo kedekde.
Comments
Loading…