Wakati Liverpool wakikataa ofa ya pauni milioni 25 kutoka Manchester City kumsajili Raheem Sterling, Chelsea na Liverpool wanamgombea Radamel Falcao.
Liverpool wamesema kwamba hawana nia ya kumuuza mchezaji huyo, lakini Man City wanatarajiwa kurejea na ofa kubwa zaidi.
Sterling, 20, amekataa mkataba mpya wa pauni 100,000 kwa wiki Anfield, akisema anataka kucheza klabu kubwa inayotwaa makombe, ambapo anahusishwa pia na Arsenal na tayari ameuza nyumba yake Liverpool akitafuta nyingine London.
Bosi mpya wa Real Madrid aliyepata kuwafundisha Liverpool, Rafa Benitez amesema anapenda mchezaji wa aina ya Sterling lakini kocha wa Liver, Brendan Rodgers amesema anaamini mchezaji wake huyo atabaki Anfield msimu ujao.
Pamoja na mambo mengine, City wanajitahidi kupata mchezaji Mwingereza ili kulandana na kanuni za soka, kwani baada ya kuondoka kwa James Milner, Frank Lampard na Micah Richards, Mwingereza pekee aliyebaki ni kipa Joe Hart.
Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho amesema anataka kumsaidia mshambuliaji wa kati wa Colombia, Radamel Falcao kurejea kwenye kiwango cha juu.
Mourinho ameahidi kufanya hivyo, akieleza kusikitishwa kwake na watu wanaomchagiza na kudhani kwamba Falcao wa kweli ni aliyeonekana Man United msimu ulionalizika.
Chelsea wamekuwa kwenye mazungumzo kumpata mpachika mabao huyo aliyeshindwa kuwika msimu uliopita lakini kinachogomba ni mshahara wake wa pauni 265,000 kwa wiki.
Liverpool wanamhitaji Falcao, 29, ili kunoa safu ya ushambuliaji ambayo imekuwa doro tangu kuondoka kwa Luis Suarez aliyekwenda Barcelona na kuumia mara kwa mara kwa ‘pacha’ wake wa msimu juzi, Daniel Sturridge.
Kadhalika huenda wakamhitaji iwapo Sterling ataondoka au kushindwa kucheza kwa kiwango, kwani tayari ameanza kuzomewa na washabiki wa Liver. Mshambuliaji mwingine ni Mario Balotelli aliyefunga bao moja msimu mzima.
Manchester United wanasema wapo tayari kutoa ofa kwa ajili ya kumnasa mshambuliaji wa Tottenham Hotspur, Harry Kane, 21.
United tayari wamekubaliana na klabu ya Hoffenheim juu ya ada ya pauni milioni 13 kwa ajili ya kumpeleka Old Trafford mshambuliaji Roberto Firmino, 23.
Mshambuliaji Jackson Martinez, 28, anayewaniwa na Arsenal na Manchester United anasema kwamba ana nia ya kuondoka Porto na kujiunga na klabu kubwa zaidi ya Ulaya.
Real Madrid wamedhamiria kukubaliana na Man U ili kumsajili kipa wao, David De Gea, 24, kabla ya safari yao ya Australia Julai 13. Inaelezwa kwamba De Gea akishaanza kuwaaga wachezaji wenzake wa United.
West Ham wapo kwenye mazungumzo ya kumsajili moja kwa moja kiungo wa Barcelona, Alex Song, 27, waliyekuwa naye kwa mkopo msimu uliopita ikielezwa ada ni kwenye pauni milioni tano.
Kadhalika wanataka kumsajili winga wa Marseille, Dimitri Payet, 28. Kocha wao mpya, Slaven Bilic aliyekuwa mlinzi wa klabu hiyo anasema kurejea hapo ni kama kulamba bingo mara mbili.