Mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Italia aliyepata kuwa kocha wa Swindon, Paolo Di Canio ameteuliwa kuwa kocha mkuu wa Sunderland.
Di Canio anachukua nafasi ya Martin O’Neill aliyefukuzwa kazi Jumapili, baada ya kushindwa kuipa timu mwelekeo mzuri, badala yake akaielekeza eneo la kushuka daraja.
Mtaliano huyo aliwasili Sunderland, kaskazini mashariki mwa England Jumapili alasiri, akahitimisha mazungumzo na mmiliki na mwenyekiti wa klabu, Mmarekani Ellis Short, na kupewa mkataba wa miaka miwili unusu.
Mazungumzo yao yalianzia jijini London, kabla hata ya Manchester United kuwafyatua Sunderland bao 1-0 na kutumiwa kama kigezo cha kumfuta kazi.
“Paolo ameonesha shauku kubwa juu ya changamoto iliyo mbele yake na anasubiri kwa hamu kuiongoza timu.
“Mlengo wa kila mmoja katika mechi saba zilizosalia ni kuhakikisha tunapata pointi za kutosha kubaki ligi kuu; naamini uwezekano wa kufanikisha umeongezeka sana kwa Paolo kujiunga nasi.
“Washabiki wetu wameonesha uvumilivu wa hali ya juu na uelewa usio wa kawaida msimu huu. Wameendelea kuiunga mkono timu kwa wingi nyumbani na ugenini.
“Uungwaji mkono huo ndilo jambo linaloendelea kutupa hamasa kwenye lengo letu la kuipa klabu mafanikio, na hiyo inabaki shabaha yetu ya msingi,” akasema Mwenyekiti Short.
Di Canio (44) alipata kusakata soka kwa mafanikio katika klabu za Sheffield Wednesday, West Ham na Charlton alipocheza nchini England. Katika ukocha Sunderland inakuwa timu ya pili baada ya Swindon.
Timu nyingine alizochezea ni Cisco Roma, Lazio,
Ternana, Juventus, Napoli, Milan na Celtic. Kwa ujumla wake, alicheza mechi 500 za ligi nafasi za kiungo na ushambuliaji na kufunga mabao zaidi ya 100.
Licha ya kuwa mtu mwenye karisma, Di Canio ni mtu mwenye vituko, aliyepata kukasirishwa na mwamuzi na kumsukuma (Paul Alcock mwaka 1998) ambapo alifungiwa mechi 11.
Alipata pia kujitangaza kwamba anaunga mkono na kushabikia ufashisti lakini si mbaguzi, moja ya mambo yaliyosababisha Makamu Mwenyekiti wa Sunderland, David Milliband kutangaza kujiuzulu nafasi yake Jumapili hii baada ya Di Canio kuajiriwa.
Hata hivyo Milliband anahamia Marekani kufanya kazi na Shirika la Uokoaji la Kimataifa, ambapo pia amejiuzulu wadhifa wake wa ubunge aliokuwa akishikilia kupitia Chama cha Labour. Nafasi yake Sunderland haikuwa ya kiutendaji.
Di Canio alichaguliwa kuwa mchezaji wa mwaka wa West Ham 1997 na mfungaji wa goli bora wa BBC msimu wa 2000. Alitwaa tuzo ya FIFA ya Fair Play 2001.
Baada ya kujiunga Swindon, alifanikiwa kuipandisha daraja hadi ngazi ya ‘Football League One’, kabla ya kujiuzulu kwa matashi yake mwenyewe Februari mwaka huu.
Alibembelezwa na viongozi wa klabu hiyo kubaki, na hata kufuatwa baada ya kuachia ngazi, lakini akakataa. Alipata kutoa fedha zake kidogo kusaidia wachezaji klabu ilipokuwa kwenye hali mbaya ikikaribia kufilisika.