Unai Emery ameanza kuonja machungu ya kukosolewa akiwa ndani ya EPL kufuatia kipigo cha 2-0 ambacho timu yake ilipokea kutoka kwa mabingwa watetezi Manchester City kwenye mchezo wake wa kwanza wa EPL uliopigwa Jumapili katika dimba la Emirates. Ni Raheem Sterling na Bernardo Silva waliofunga mabao ya Manchester City yaliyotia doa mwanzo wa safari mpya ya Arsenal tangu walipoachana na Arsene Wenger, kocha waliyedumu naye kwa zaidi ya miongo miwili.
Mbinu za Emery zimekutana na makali ya wakosoaji wa kaliba ya juu huku baadhi wakivuka mipaka ya ukosoaji na kuingia kwenye mashambulizi yanayomaanisha kumhukumu mwalimu huyo mapema mno. Sam Allardyce alijaribu kuonesha wazi kuwa yeye si mshabiki wa aina ya mchezo wa Unai Emery. Kocha huyo wa zamani wa England haungi mkono mchezo wa kuanzisha mashambulizi taratibu kutokea nyuma hasa unapocheza na timu aina ya Manchester City ya Guardiola. Amenukuliwa akisema kuwa huo ni mkakati wa kipumbavu.
“Ni kosa la meneja”. Big Sam alisema baada ya Arsenal kupoteza mchezo wao wa ufunguzi wa Ligi Kuu ya England Jumapili. “Manchester City hufanya nini? Ni kukaba, kukaba, kukaba (punde wapotezapo mpira), sasa kwanini uanze kucheza taratibu kutokea nyuma?”. Alinukuliwa Sam Allardyce na akaongeza, “Ni upuuzi kucheza mchezo wa namna hiyo… Ila kama una timu iliyo bora zaidi unaweza kufanya hivyo”. Aliongeza Allardyce.
Mmoja kati ya wachezaji wa zamani wa Arsenal waliojijengea heshima kubwa wakiwa na uzi wa timu hiyo, Tony Adams naye hakusita kupeleka mashambulizi kwa Unai Emery. Amenukuliwa akisema kuwa haoni dalili zozote za mafanikio ya Washika Bunduki wa London chini ya Mhispania huyo. “Timu imeachana na Wenger ambaye amekuwa akicheza mchezo wa wazi wa kushambulia, nilitarajia mwalimu mpya akazie kwenye ulinzi” Alisema Adams.
“Kwa miaka 10 sasa tumekuwa tukiruhusu mabao mepesi, hasa kwenye michezo ya ugenini. Nilitaka amuanzishe golikipa wake mpya (Bernd Leno) afanye kazi na walinzi wake wanne, na aweke viungo wawili wakabaji wa katikati kisha wacheze bila kuruhusu bao”. Alizungumza nahodha huyo wa zamani wa Arsenal akikosoa mbinu na uchaguzi wa kikosi wa mwalimu mpya wa Arsenal.
Adams aliongeza kuwa haoni chochote cha maana kilichofanywa na Emery mbaka sasa tangu alipoingia kazini kukinoa kikosi cha Arsenal wiki kadhaa zilizopita. Jumamosi Arsenal watakuwa na mtihani mwingine mgumu dhidi ya Chelsea katika dimba la Stamford Bridge. Hivyo huu ni wakati sahihi wa kukosoa chochote kinachoonekana hakiko sawa kuhusu upangaji wa timu ama mbinu za mwalimu Emery. Lakini si wakati sahihi wa kumhukumu kwa kutumia matokeo ya mchezo mmoja tu, tena dhidi ya Pep Guardiola.
Unawezaje kumhukumu kocha kwa kupoteza mchezo mmoja dhidi ya timu iliyoshinda taji la EPL msimu uliopita kwa tofauti ya alama 19? Unawezaje kumhukumu Emery wakati pengo kati ya timu yake mpya na timu tishio ya mpinzani wake lilikuwa la alama 37 kwenye msimu uliopita? Hatumtendei haki Emery tukihukumu kwa kutumia matokeo yake ya mchezo wa kwanza dhidi ya mabingwa watetezi.
Bajeti ya usajili ya Manchester City kwa misimu mitatu iliyopita ni takribani mara mbili ya bajeti ya Arsenal kwenye kipindi kama hicho. Mwalimu mpya anapojiunga na timu yenye bajeti finyu kiasi hiki kulinganisha na mpinzani wake anahitaji kupewa muda. Ikumbukwe moja kati ya sababu za maana zinazowafanya Manchester City kuwa tishio ni pochi lao nene. Wasifanywe kipimo kwa wakati huu dhidi ya Unai Emery ambaye ndio kwanza amecheza mchezo mmoja tu wa mashindano akiwa na timu yake mpya.
Ni sahihi kukosoa mbinu na upangaji wa kikosi wa mwalimu hasa anapopata matokeo mabaya. Lakini mkosoaji anapokwenda mbali zaidi na kuziita mbinu za mwalimu eti ni za kipumbavu anatoka nje ya mipaka ya usahihi. Mwingine, ambaye mbaya zaidi ni mtu wa kuheshimiwa kwenye historia ya klabu anapothubutu kusema eti haoni chochote ambacho Emery amekifanya mbaka sasa ni jaribio la wazi la kumkatisha tamaa Mhispania huyo. Ni mapema mno kumhukumu Emery.