Msimu wa Yanga unaweza kuwa uliisha jana Jumamosi baada ya kumaliza vibaya wiki ya pili mfululizo kwa kufungwa mabao 3-1 na Azam katikia mchezo uliojaa hasira na kadi nyekundu wa ligi kuu ya Bara, kwenye Uwanja wa Taifa.
Yanga ambayo mwishoni mwa wiki iliyopita ilifungwa bao 1-0 na Zamalek ya Misri na kuaga Ligi ya Klabu Bingwa Afrika, imebaki katika nafasi ya tatu kwa kipigo cha jana; pointi nne nyuma ya Azam iliyo kileleni angalau kwa saa 24.
Azam yenye pointi 41, moja zaidi ya jumla ya ilizokusanya msimu uliopita na kushika nafasi ya tatu, itashushwa na Simba kama mabingwa wa Bara wa zamani hao watatoka japo sare dhidi ya Toto African katika mchezo wa leo kwenye uwanja huo.
Zikiwa zimebaki raundi nane, na ikiwa ni timu mbili za juu tu zitakazoshiriki michuano ya klabu ya Afrika mwakani Yanga italazimika kufanya kazi ya ziada kurudi katika eneo hilo.
Palikuwa na vurugu za kufa mtu nje ya uwanja baada ya mchezo huo mashabiki wa Yanga wakitaka kuwadhuru waamuzi hivyo kupeleka jeshi la polisi kutumia mabomu ya machozi, gari la maji ya kuwasha na farasi kutuliza ghasia hizo.
Haruna Niyonzima, shujaa wa Yanga katika siku za karibuni, ndiye aliyekuwa chanzo cha kuporomoka kwa timu hiyo katika mchezo wa jana.
Akiwa alionyeshwa kadi ya njano kwa kupiga mpira uliotengwa na Azam kwa ajili ya adhabu ndogo mapema katika kipindi cha kwanza, alimbwatukia Israel Nkongo akipinga uamuzi wake kwamba kiungo huyo alimfanyia madhambi Ibrahim Mwaipopo wakati wakigombea mpira baadaye.
Nkongo alimzawadia kadi ya pili ya njano na nyekundu, kitendo kilichosababisha wachezaji wa Yanga walio mchezoni na benchini kumvamia wakimsukuma na kumtupia maneno makali kwa dakika kadhaa.
Fujo hizo zilipotulizwa na wanausalama, muamuzi huyo alimuonyesha kadi nyekundu Nadir Haroub kabla ya kuanzisha tena mchezo hivyo kuifanya Yanga ibaki na wachezaji tisa uwanjani kwa zaidi ya saa moja la mchezo.
Ulikuwa ushindi wa nne mfululizo wa Azam dhidi ya Yanga katika mechi za michuano na kirafiki, mara ya mwisho ikiikung’uta mabao 3-0 katika Kombe la Mapinduzi Januari.
Azam iliifunga Yanga 1-0 katika mechi ya duru la kwanza msimu huu na 2-0 katika mchezo wa kirafiki.
Magoli ya Azam yalifungwa mawili na John Bocco na moja la Kipre Balou wakati Hamisi Kiiza alikipa heshima kipigo hicho alipoipa timu yake bao lililofanya magoli yawe 1-1 lakini likaja kuwa la kufutia machozi.
Kwa magoli mawili ya jana Bocco amezidi kuongoza chati za ufungaji ligi kuu ya Bara akiwa na mabao 15, matano juu ya Kenneth Asamoah wa Yanga na Emmanuel Okwi.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
Comments
Loading…