*Kibarua cha Villas-Boas hatarini Spurs
Ndege iliyokuwa imewabeba wachezaji na viongozi wa Manchester United imebadili mpango wa kutua ikiwa umbali wa mita 400 juu ya uwanja wa ndege wa Cologne/Bonn, Ujerumani.
Kitendo hicho kiliwatia hofu wengi, wakikumbukia ajali iliyowapotezea wachezaji wake Munich 1958, ambapo Jumatano hii ndege hiyo ilirudi juu na kujipanga upya.
Wachezaji hao walikuwa wanakwenda Ujerumani kwa ajili ya mechi ya marudiano na Bayer Leverkusen katika Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL).
Hata hivyo, kwa furaha ya wana Man U na wadau wengine, ndege hiyo ilijaribu mara ya pili na kutua salama.
Klabu haikupenda kuzungumzia suala hilo mapema, lakini beki wao Rio Ferdinand aliandika kwenye ukurasa wake kwamba ndio walikuwa wametua baada ya kupata tatizo awali la kufanya hivyo lililowatia mashaka makubwa.
United watafuzu kwenye hatua ya 16 bora iwapo watashinda kwenye mechi inayopigwa leo usiku katika dimba la Bay Arena.
Kocha David Moyes anamtegemea Wayne Rooney katika ushambuliaji baada ya Mdachi tegemezi Robin van Persie kuwa na matatizo ya nyama za paja na kidole cha mguu.
Rooney yupo katika hali nzuri kimchezo japokuwa anahatarisha kuchukuliwa hatua za kinidhamu uwanjani kutokana na hasira au tabia yake wakati mwingine.
Man U itawakosa pia nahodha wake, Nemanja Vidic aliyeumia kichwa wakati wa mechi dhidi ya Arsenal na majeruhi mwingine ni Michael Carrick huku kiungo toka Everton, Marouane Fellaini akiwa na kadi inayomzuia kucheza.
ANDRE VILLAS-BOAS HATARINI SPURS
Kuna habari kwamba hatima ya Kocha Mreno wa Tottenham Hotspur, Andre Villas-Boas ipo hatarini kutokana na mwenendo wa timu hiyo.
Villas-Boas (37) anasemwa kuwa katika wakati mgumu, ambapo watendaji wa klabu hiyo wamempa muda mfupi wa kurekebisha makosa vinginevyo watafute mtu mwingine kuchukua nafasi hiyo.
Moja ya vyanzo vya kuaminika ndani ya klabu vinasema kwamba miezi mitatu iliyopita haijawaridhisha wakubwa, ambapo Spurs iliuza mchezaji wake bora, Gareth Bale na wengine na kununua saba wapya, wengi wao wakiwa ni vijana wadogo.
Utetezi wa Villas-Boas sasa ni kwamba wachezaji wake wanahitaji muda wa kuzoeana, lakini wakuu wa White Hart Lane hawataki kusikia hayo, maana wachezaji waliosajiliwa aliwapendekeza yeye na anajua ligi ikianza hakuna cha kusubiriwa.
Spurs walifungwa 6-0 na Manchester City Jumapili iliyopita ambapo analaumiwa pia kutochukua hatua za dhati na haraka kuzuia ukuta uliokuwa ukivuja.
Katika msimu wake wa kwanza Spurs, Villas-Boas aliweka rekodi kwa kukusanya pointi 72 katika Ligi Kuu ya England lakini wakashika nafasi ya tano.
Baada ya mechi 12 msimu huu, Spurs wanashika nafasi ya tisa, wakiwa pointi moja nyuma ya Manchester United wakiwa wamefungwa na timu za Man City, Newcastle, West Ham na mahasimu wao wa London Kaskazini, Arsenal.
Chelsea walimfukuza Villas-Boas baada ya miezi minane tu ambayo hawakuridhishwa naye na sasa amekaa karibu mara mbili ya muda huo Spurs. Anaweza kunusuriwa na matokeo ya mechi mbili zijazo.
Comments
Loading…