Ligi Kuu ya Tanzania inayojulikana kama NBC Premier League ni miongoni mwa mashindano maarufu zaidi ya soka Afrika Mashariki na kati. Ikiwa na historia ya muda mrefu na mashabiki wengi bila kusahau kuwa ushindani mkubwa katika ligi hii ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya soka la Tanzania.
Mpaka sasa tumeona ushindani mkubwa katika ligi jambo ambalo limeongeza ubora wa soka la kitaifa kama ambavyo tumeona Timu ya Taifa ya Tanzania ambayo imefuzu AFCON ikiwa na wachezaji wengi ambao wanacheza Ligi Kuu ya NBC.
Tukumbuke kuwa timu zinapokabiliana na changamoto kubwa kutoka kwa wapinzani wao, wanalazimika kutumia mbinu za kisasa pamoja na kujituma zaidi achana na hamasa zile za mkishinda mtapata Milioni 60 lakini tukumbuke kuwa ushindani wa hii ligi umepelekea kuimarisha vipaji vya wachezaji wengi wa kizawa ambao walikuwa wakionesha kuwa nao waaminiwe kwani wana uwezo mkubwa jambo ambalo huongeza viwango vya wachezaji ambao baadaye huwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa kama Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) na mashindano ya FIFA.
Msimu huu tumekua na ligi yenye ushindani mkubwa mpaka imepelekea kuongeza msisimko miongoni mwa mashabiki. Nani aliamini kuwa timu kama Tabora United italeta ushindani mkubwa ndani ya ligi? Wakati matokeo ya mechi hayana uhakika, mashabiki wanahamasika kuhudhuria viwanjani na kufuatilia ligi kupitia televisheni pamoja na zile taarifa za papp kwa hapo kwenye mitandao ya kijamii. Ushindani wa kweli hufanya kila mechi kuwa ya kusisimua na kuongeza uhusiano wa karibu kati ya timu na mashabiki wao.
Mpaka sasa tumeshuhudua ushindani mkubwa katika NBC Premier League kwa timu ndogo kushindana na timu kubwa. Timu ndogo kama Tabora United, Singida BS na hata Fountain Gate zimeonesha kuwa unapoweka juhudi na kushinda dhidi ya vigogo wa soka basi una uhakika wa kupata motisha ya kuendelea kufanya vizuri zaidi. Ushindani huu unasaidia kuondoa dhana kwamba ligi inatawaliwa na timu chache, jambo ambalo linaweza kupunguza mvuto wa mashindano.
Tunaona namna ambavyo timu ndogo zinavyojitahidi kufanikisha kuwa wanaonesha nao wana kitu huku wakiutaka ushindi hili ni jambo ambalo huchangia kuimarisha soka la vijana kwa kuwekeza kwenye vipaji chipukizi kama ambao tumekua tukiwaona vijana wadogo wakicheza Ligi Kuu.
Hata wewe msomaji kama unatazama vyema kabisa utaona kuwa ushindani mkubwa ambao umekua kwenye Ligi msimu huu umevutia wawekezaji na wadhamini kwani tumeona timu karibia zote ambazo zinashiriki Ligi Kuu ukiachilia mbali wadhaminj wakuu wa Ligi yaani NBC pamoja na Azam Tv lakini wapo wadhamini wengine ambao walikuwa waliweka pesa Kwa Timu hizi nyingine Tofauti na zile kubwa ambazo tumezizoea.
Usisahau kuwa Makampuni haya yanayodhamini ligi pamoja na vilabu vya soka vinavyoshiriki Ligi Kuu hufaidika na kuonekana kwa bidhaa zao kupitia mashindano haya ambayo yana mvuto wa kipekee. Timu pia zinanufaika kwa kupata misaada zaidi ya kifedha ambayo inawawezesha kuimarisha miundombinu, kununua wachezaji bora na kufundisha wachezaji wa ndani.
Vilevile, ushindani wa ligi huongeza thamani ya haki za matangazo, ambayo ni chanzo muhimu cha mapato kwa vilabu na shirikisho la soka nchini (TFF).
Achana na misimu kadhaa nyuma ambayo mashabiki wengi walipendelea kwenda kutazama mechi kubwa au zile zinazohusu Timu kubwa pekee lakini kwa sasa kumekua na mahudhurio ambayo kwa mikoani si haba sana kwani jambo ambalo liinachangia uchumi wa michezo nchini Tanzania.
Japokua tuko kwenye zama ambazo mpira umekua wa kitabu sana na kukosekana au kuwa na zile madoido machache ya mchezaji binafsi kumbuka kuwa kwa sasa Ligi Kuu ya Tanzania imekua ni sehemu ambayo inatoa burudani Kwa Jamii ya watanzania na wageni ambao walikuwa wanakuja kutazama soka.
Ligi yenye ushindani mkubwa husaidia kuepuka utawala wa muda mrefu wa timu moja au mbili, hali inayoweza kuathiri hamasa ya mashindano. Kwa mfano, kwa miaka mingi Simba SC na Yanga SC zimekuwa zikishindania nafasi za juu pekee, lakini sasa ushindani umeongezeka kutokana na juhudi za timu ndogo kama Azam FC na Singida Fountain Gate FC. Ushindani huu hufanya ligi kuwa ya kuvutia zaidi na yenye matokeo yasiyotabirika.
Ushindani mkubwa katika Ligi Kuu ya Tanzania (NBC Premier League) una umuhimu mkubwa katika kuimarisha soka la kitaifa na kukuza maendeleo ya michezo nchini.
Comments
Loading…