Mvua ilikata ghafla, manyunyu yakabaki katika anga la klabu Yanga.
Dalili ya kwamba mvua ya neema ilikuwa inapotea na kiangazi kukaribia
zilianza kuonekana baada ya mwenyekiti wa timu hiyo Ndugu. Yusuph
Manji kujiweka pembeni na klabu hii.
Hali ilianza kubadilika taratibu kwa sababu Ndugu. Yusuph Manji ndiye
alikuwa kiungo muhimu sana hasa hasa kwenye suala la uchumi.
Ilikuwa ngumu kusikia malalamiko kutoka kwa wachezaji kuwa hawajalipwa
mshahara wao kwa miezi kadhaa mfululizo.
Njaa ilikuwa mbali sana, visima vya maji vilikuwa vinapatikana kwa
wingi pale Jangwani, lakini alipoondoka Yusuph Manji ukame halisia wa
jangawani tulianza kuushuhudia.
Dirisha la usajili lilidhihirisha yote haya, Yanga ilishindwa kufanya
usajili nyota kama kipindi cha nyuma walivyokuwa wanafanya
Sajili za wachezaji vijana kutoka serengeti boys kama Ramadhani
Kabwili, Yohana Nkomola, Said Musa na wengine ilidhihirisha Yanga hii
inapitia nyakati ngumu kwa muda huo (simaanishi kuwasajili hawa vijana
Yanga walikosea, hapana ila najaribu kuonesha utamaduni ambao awali
hawakuwa nao kipindi walipokuwa na pesa za usajili).
Kocha George Lwandamina alikuwa na kikosi cha kawaida kilichokuwa
kimejaa wachezaji wengi wa kawaida katika klabu isiyo kuwa ya kawaida.
Hofu ilijaa ndani ya mioyo ya wana Yanga, wengi waliona ni ngumu kwa
Yanga kufanya vizuri kwa sababu ya kikosi walichokuwa nacho.
Kikosi ambacho kilionekana hakina ushindani mkubwa ukilinganisha na
vikosi vilivyopita, ilikuwa ngumu kuamini George Lwandamina kama
atatumia kikosi hiki kupambana kwa ajili ya ubingwa.
Mzimu wa majeruhi ukauvaa tena, matatizo yakawa yanarundikana baada ya
tatizo. Hali ya uchumi ndani ya klabu ikaungana na hali ya majeruhi ya
wachezaji nyota ndani ya timu.
Timu ikawakosa wachezaji nyota ambao walikuwa mhimili mkubwa ndani ya
misimu kadhaa waliyobeba ubingwa.
Kila mtu ndani ya Yanga alitembea akiwa ameinamisha kichwa, swali
kubwa ni namna gani Yanga inaweza kukimbia bila ya wachezaji wake
nyota.
George Lwandamina hakuamini kama huo ni mzigo mzito kwake, aliamini
kila mchezaji ndani ya kikosi cha Yanga alisajiliwa kwa ajili ya
kuwapa matokeo chanya Yanga.
Akaingiza sumu kali ndani ya wachezaji wa Yanga, wakapigana bila kuwa
na hofu kuwa wachezaji nyota wa kikosi hicho hawapo.
Wakaitumia nafasi hiyo kuonesha kiwango chao , kiwango ambacho
ƙkiliwasaidia kwa kiasi kikubwa kupata alama ambazo zilikuwa na
msaada kwao.
Hata katika mechi za kimataifa walijitengenezea mazingira mazuri ya
wao kufuzu kwenda katika hatua ya makundi ya kombe la shirikisho
barani Afrika.
Pamoja na matatizo mengi ndani ya timu, Lwandamina hakuonekana
kutetereka, leo hii hayupo na timu.
Leo hii kaiacha Yanga katika kipindi cha muhimu sana, kipindi ambacho
Yanga inamwihitaji yeye kwa kiasi kikubwa.
Kipindi ambacho Yanga inahitaji kutetea kombe lao la ligi kuu na
kufika mbali katika michuano ya kimataifa.
Hawana kiongozi tena, uwepo wake ulikuwa muhimu sana ndiyo maana
tuliona katika michuano ya kombe la mapinduzi Yanga wachezaji walikuwa
wapweke sana , timu haikuwa na morali kwa sababu baba wa timu hakuwepo
kwenye benchi la ufundi.
George Lwandamina alikuwa zaidi ya baba pale Yanga, kuna wakati alitoa
pesa zake mfukoni kuwahudumia wachezaji wake.
Wachezaji walimsikiliza yeye na kupigana kutokana na maagizo yake,
leo hii hayupo tena.
Wasiwasi unanikamata ninapofikiria Yanga watakavyoenda kucheza katika
mechi za kimataifa. Morali ya kupigana itakuwepo ndani yao kipindi
hiki ambacho hali ya uchumi ni mbaya ndani ya klabu?
Nani atawaambia wapigane kwa matumaini ya kupata kesho? Nani atawapoza
kwa kidogo chake kipindi hiki ili wapigane na njaa??
Hapa ndipo huruma inaponivaa, Yanga imeachwa kipindi ambacho ilikuwa
inamwihitaji sana George Lwandamina.