Kilikuwa ni kipindi chenye furaha sana. Kipindi ambacho kila aina ya kinywaji kilitumika kusindikiza furaha. Hakukuwepo na mipaka kwenye hili. Kila mtu alitumia kila anachokiamini kinaweza kikawa kitu bora zaidi kwenye kusindikiza furaha yake.
Ndicho kipindi ambacho wengi tulifahamu kuwa Jack Grealish ni mlevi wa kupindukia. Alitumia vileo vingi bila kujali nani anamtazama au nani anasema nini. Kwake yeye furaha ilikuwa imezidi kifani.
Hii ilikuwa ni zaidi ya furaha ya kushinda makombe matatu ndani ya msimu mmoja yani “treble”. Hii ilikuwa furaha ya kuvunja rekodi ya wapinzani wao wakubwa ambao ni majirani wao Manchester United.
Manchester United chini ya kocha bora kuwahi kutokea Duniani, Sir Alex Ferguson walifanikiwa kushinda vikombe vitatu ndani ya msimu mmoja “treble” mwaka 1999 ambapo walifanikiwa kuchukua Ligi kuu ya England, Kombe la FA pamoja na ligi ya mabingwa barani Afrika.
Baada ya miaka 23, mwanaume kutoka jimbo la Catalunya aliweza kuifikia rekodi hii Sir Alex Ferguson tena akiwa akiwa kwa wapinzani wao wakubwa Manchester City. Msimu wa mwaka 2022/2023 Manchester City walifanikiwa kuchukua vikombe vitatu vya Ligi kuu ya England, FA pamoja na ligi ya Mabingwa barani Ulaya.
Ushindi huu mkubwa uliongeza furaha kubwa sana kwenye klabu hiyo. Furaha ambayo kama nilivyokuambia ilisindikizwa na kila aina ya starehe kukamilisha furaha hiyo. Kila mchezaji, kocha , kiongozi na shabiki wa Manchester City kilele chake cha furaha kilifika Kibo.
Wakati watu wakifurahia kuna kijana alikuwa amekaa pembeni akiwatazama wachezaji wenzake walivyokuwa wanafurahia huku yeye akionekana akiwa mwenye mawazo sana. Kichwa chake kilikuwa kizito, akili yake ilikuwa inafanya kazi kwa kasi sana na muda wa yeye kufurahia haukuwepo kwenye nafsi yake.
Alikuwa hajafurahia Manchester City kushinda vikombe vitatu yani “treble”? Jibu la swali ni hapana. Kila alipokuwa akiwatazama Kelvin De Bryune, Jack Grealish, Phil Foden alikuwa anaona kiwango chao bora walichokionesha msimu husika. Kiwango ambacho kilikuwa kinampa swali yeye, Je ni lini atapata nafasi ya kucheza ?
Huyu alikuwa ni Col Palmer, mchezaji ambaye alilelewa na kukuzwa kwenye kituo cha kulelea vipaji vya Manchester City. Kwake yeye Manchester City palikuwa ni nyumbani kabisa, lakini tatizo kubwa ambalo alikuwa nalo ni yeye kupata nafasi ya kucheza.
Ilikuwa ni ngumu kujipendeza katikati ya kina Phil Foden , Jack Grealish, Kelvin De Bryune na kupata namba. Kwa umri wake kitu kikubwa alichokuwa anakitaka ni kupata nafasi ya kucheza ili kutengeneza thamani yake. Baada ya kumaliza kuwatazama wenzake wakifurahia makombe kesho yake Cole Palmer alienda ofisini kwa Pep Guardiola kuomba nafasi ya kuondoka.
Sababu kubwa ya kutaka kuondoka ni yeye kutafuta sehemu ambayo itampa nafasi ya kucheza mara kwa mara. Pep Guardiola hakuona nafasi ya Col Palmer kwenye kikosi chake kwa kipindi hicho, aliamua kumpa baraka. Col Palmer aliondoka na kwenda kujiunga na Chelsea.
Sehemu ambayo alipata nafasi ya kucheza na kuonesha kipaji chake. Sehemu ambayo ilimpa nafasi yeye kuwa mchezaji bora chipukizi msimu jana, msimu wa mwaka 2023/2024. Mpaka sasa tangu ajiunge na Chelsea, Col Palmer amehusika kwenye magoli katika michezo.
Kama Col Palmer angeamua kukaa Manchester City kwa sababu tu anauhakika wa kulipwa vizuri, kwa sababu ana uhakika wa kupata vikombe , leo hii dunia isingekuwa inamuimba Col Palmer kwa kiwango chake hicho.
Hii ipo sana kwetu Tanzania. Kuna wachezaji vipaji vyao vinadumaa kwa sababu wapo sehemu ambayo wana uhakika wa kupata mshahara mzuri na makombe mara kwa mara haijalishi kama wanacheza au wanatoka benchi.
Moja ya kipaji ninachokihusudu ni Ladack Chasambi, ni kipaji kikubwa sana na kama kikipata nafasi ya kucheza basi Tanzania tutanufaika na kipaji hiki. Ladack Chasambi yupo sehemu ambayo kuna watu wengi ambao ni ngumu sana kuwatoa kama ambavyo Col Palmer alivyokuwa Manchester City.
Kitu pekee ambacho Ladack Chasambi anatakiwa kukifanya ni yeye kuamua kuchukua maamuzi ya kuondoka Simba SC na kwenda sehemu ambayo itampa nafasi ya kuonesha kipaji chake. Kwangu mimi, sehemu ambayo naona ina nafasi kwa Ladack Chasambi ni Azam FC.
Azam FC ni sehemu ambayo inakila kitu ambacho kinaweza kumfanya mchezaji awe bora kuanzia miundombinu mpaka uhakika wa malipo. Azam FC pia inakosa wachezaji aina ya Ladack Chasambi kwa sasa. Kwa hiyo Ladack Chasambi pamoja na Azam FC wanahitajiana. Ingekuwa mimi ndiye msimamizi wa Ladack Chasambi ningempeleka Azam FC mwezi Januari.
Comments
Loading…