in , , ,

NAPATA SHIDA KUJUA MGUU WA KUSHOTO NA KULIA WA MWIGULU

“Kijana mwenye upeo mkubwa na kiongozi shupavu”, ni maneno machache ambayo unaweza kuyachagua kwenye maneno bora ya kuelezea ubora wa Dr.Mwigulu Nchemba. 

Kioo cha vijana wengi, wengi wetu tunamtumia kama kioo cha kujitazama. Hatua zake zimebeba matumaini ya vijana wengi.

Hatua zake za mafanikio ni hatua ambazo zimebeba maana halisi ya mazingira ya kijana wa Kitanzania. 

Hesabu za maisha yake zilianza kupigwa kutoka kwenye familia ya hali ya chini. Familia isiyokuwa na uwezo mkubwa wa kifedha. Lakini kwake yeye hiki hakikuwa kigezo kikubwa cha kumkatisha tamaa katika mbio za kuzikimbiza ndoto zake.

Alikimbia, alidondoka na kuna wakati mwingine alidondoshwa kwa makusudi tu ili asifike anapopaota. Hiki hakikuwa kitu ambacho kinaweza kumvunja nguvu.

Kila alipokuwa anadondoka alikuwa anaamka na nguvu kubwa ya kufanya jambo kubwa ambalo lilikuwa na matokeo chanya katika maisha yake.

Leo hii anasimama kama kijana kiongozi ambaye ni mfano mkubwa kwa wengi. Kijana ambaye ameshika nyadhifa nyingi serikalini na kwenye chama.

Kijana ambaye anapenda michezo, damu yake inazungumza mpira wa miguu ndiyo maana siyo jambo la kushangaza unaposikia ni raisi wa Singida United.

Timu ambayo ina mafanikio makubwa nje ya uwanja. Ndiyo timu ambayo ina wadhamini wengi kuliko timu yoyote ligi kuu Tanzania bara.

Hapana shaka nguvu ya Dr.Mwigulu Nchemba ni kubwa mno kwenye hili na amefanikiwa kuifanya Singida United ipunguze gharama za kuiendesha klabu kwa sababu ya wadhamini wengi waliopo kwenye timu.

Hiki ndicho kitu ambacho tulikuwa tunakililia muda mrefu, matamanio yetu ni kuona timu nyingi zinaendeshwa kisasa, zinaendeshwa kutokana na mazingira ya dunia ya sasa.

Kwenye hili, Singida United imefanikiwa kwa asilimia kubwa sana, ndiyo maana inaonekana ni moja ya timu ambayo inaleta ushindani pamoja na kwamba ina msimu mmoja kwenye ligi kuu.

Na ndiyo timu ambayo inafanya usajili wa wachezaji ambao wanaonekana wana viwango vya ushindani.

Tuliona miguu ya Tafzada Kutinyu, tukapendeshwa na kiwango cha Shafiq Batambuzie hata mikono ya Peter Manyika ilirudishwa makali yake.

Tuliiheshimu sana Singida United na bado tunaiheshimu na kuipa nafasi ya kutoa changamoto kubwa kwa Simba na Yanga.

Ambao wametawala mpira huu kwa muda mrefu lakini hawana akili za kujiendesha kisasa ndiyo maana leo hii tunaiona Yanga ikitapatapa bila msaada wowote kwa sababu jana hawakutengeneza mazingira bora ya kuishi leo.

Jana yao ilikuwa ilitengeneza mazingira ambayo leo hii Dr.Mwigulu Nchemba anaonekana kuisaidia Yanga kupitia mgongo wa Singida United.

Sakata la Faisal “fei” Toto lilikuwa kubwa sana ila macho yetu tuliyalazimisha kuliangalia katika hali ya udogo.

Tulichukulia kawaida kwa sababu tumezoea kuchukulia vitu katika ukawaida usio wa kawaida.

Najua Dr.Mwigulu Nchemba ni mpenzi wa Yanga, na muda huu ni Rais wa Singida United. Busara kubwa ingetumika katika kuisaidia Yanga wakati koti la Uraisi wa Singida United akiwa amelivua.

Kuisaidia Yanga akiwa na koti la Uraisi wa Singida United inapoteza uaminifu ndani ya ligi yetu.

Bayern Munich iliwahi kuisaidia Borrusia Dortmund kiasi cha fedha ilipodidimia kiuchumi lakini haikuwahi kuwasaidia wachezaji.

Hii inatoa taswira timu Fulani ni tawi la timu Fulani, ni busara kwa Dr.Mwigulu Nchemba kuamua ni upande upi sahihi kwake yeye kusimamia kuliko kusimama mguu mmoja Singida United na mguu mwingine Yanga.

Uimara wake unategemea sehemu ambayo aliyosimama. Sehemu aliyosimama una athari kubwa kwenye mpira wetu.

Kuna hatari ya kupungua kwa uwazi (Integrity) kwenye ligi yetu kwa kitendo hiki ambacho wanafanya Singida United.

Kitu kilichomtambulisha Dr.Mwigulu Nchemba ni busara na uhodari wake kwenye vitu vingi. Anatakiwa aoneshe uhodari wake kwa kuchagua sehemu sahihi ya kusimamia kwa manufaa ya mpira wetu.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

UITALIANO UTAKUWA NGUZO YA MAURIZIO SARRI PALE CHELSEA?

Ndemla

SAID NDEMLA KARIBU TUZIFUNGUE KURASA ZA KITABU CHAKO