LIGI Kuu Tanzania inatajwa kushika nafasi ya tano kwa ubora barani Afrika, kwa mujibu wa shirikisho la soka CAF. Ubora wa Ligi hiyo unatokana na mchanganyiko wa wachezaji waliopo kwenye timu mbalimbali. Wachezaji wa kigeni wameingia katika mifumo ya Ligi kuu na kuongeza ushindani ambapo umeipaisha kimataifa. Hata hivyo Tanzania inakabiliwa na kibarua kigumu cha kumpa mlindamlango mwenye ubora katika kikosi cha timu ya Taifa.Β
Kwa muda mrefu Taifa Stars imekuwa ikimtegemea Aishi Manula, ambaye amekuwa akisaidiwa na makipa wengine kwenye mashindano mbalimbali. Makocha mbalimbali wamekuja na kuondoka wamemwacha Manula akiwa katika umahiri uleule. Manula ameshika namba moja katika kikosi chya timu ya Taifa kwa muda mrefu na ameshiriki fainali za AFCON mara mbili mtawalia. Katika majukumu yake amekuwa akiletewa makipa wengine kama Ali Salim,
Kwesi Kawawa, Abutwalib Msheri, Metacha Mnata na wengineo. Lakini Manula amebaki kuwa namba moja na pale alipokosekana pengo laki lilikuwa dhahiri shahiri. Taifa Stars inategemea kuundwa na makipa kutoka timu zingine. Kila timu za Ligi Kuu zinategemea kuwa na makipa wenye viwango vizuri. Hata hivyo nafasi hiyo imekuwa katika kikaango kikali kutokana na makipa mbalimbali kuvurunda. Kwa maana ahiyo tumejikuta tunalo jukumu la kuziba pengo pale Aishi Manula anapokosekana.
Taifa Stars bila Manula
Hakuna ubishi kwamba Aishi Mnaula ndiye golikipa namba moja, lakini katika klabu yake ya Simba amekuwa akikalia benchi kutokana na umahiri wa Mussa Camara raia wa Guinea. Pengine majeraha yanaweza kutajwa sababu za kukalishwa benchi, lakini wakati huo huo asipocheza mara kwa mara inamgharimu nafasi yake timu ya Taifa.
Mfano hivi karibuni aliitwa katika kikosi cha Taifa Stars kwa wachezaji wa ndani kwa ajili ya kufuzu mashindano ya CHAN. Kocha wa Taifa Stars ya mashindano ya CHAN, Bakari Shime alionesha wazi wazi kuwa golikipa wetu Aishi Manula ni mchezaji muhimu mno licha ya kutocheza mara kwa mara. Hii ina maana kwamba wachezaji wa nafasi yake ni wachache ama hawana ubora kama ule alionao nyanda huyo. Vilevile ni dhahiri kuwa Aishi Manula anahitajika kuimarishwa ili aweze kulitumikia Taifa. Pia makipa wa nafasi yake bado hawachezi katika mifumo ya sasa.
Je ni ipi nafasi ya Kwesi Kawawa?
Golikipa huyu amekuja kuwakilisha nchi yake ya Tanzania. Ni miongoni mwa vizazi vya Kitanzania vilivyozaliwa nje ya nchi. Kwesi Kawawa anatarajiwa kuchuana na Aishi Manula, lakini anatakiwa kuonesha uwezo kumzidi nyanda mwenzake. Katika suala la kiwango Kwesi Kawawa hajacheza mara kwa mara timu ya Taifa au mashindano yoyote hadi pale alipokwenda AFCON na Taifa Stars. Kwahiyo Kwesi Kawawa akipewa nafasi ya kucheza mara kwa mara itamwimarisha na kumfanya ajiamini zaidi kuliko nafasi yake ya sasa.
Katika mazingira ya sasa Kwesi Kawawa hajavuna upendo wa kutosha kutoka kwa mashabiki wa soka nchini Tanzania. Vilevile mashabiki wengi hawakuwahi kuona uwezo wake hivyo hakuna anayeweza kusema ni nyanda wa kutumainiwa. Lakini makocha pekee ndiyo wanajua namna gani Kwesi Kawawa anawez akutoa mchango wake. Ili kuimarisha Taifa Stars ni muhimu kumpa nafasi Kwesi Kawawa kwa maslahi ya Aishi Manula na nafasi ya makipa.
Kwesi Kawawa hajacheza katika kiwango cha juu au kutulia vizuri langoni, kwa sababu mchezo wa kwanza aliokabidhiwa dhidi ya Morocco kwenye hatua ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia, alikumbana na presha kubwa ambayo bila shaka yoyote ilitokana na ugeni wake kwenye mchezo husika. Presha aliyokuwa nayo kuwaridhisha mashabiki wa soka nchini pamoja na makocha wake ilimzidi kipimo na hivyo kujikuta akifanya makosa madogo wakati wa mchezo.
Hata hivyo huyu ni kipa mwenye uzoefu wa kusihi nje ya Tanzania. Anafahamu utamaduni wa kimpira na mashindano ingawa hakuwa na uzoefu wa soka la Kiafrika. Kwahiyo ilia pate kuwa kwenye kiwango bora lazima apatiwe nafasi ya kucheza mara kwa mara na kuhakikisha kuwa Taifa Stars inakuwa kwenye mikono salama baad aya Aishi Manula kuumia au kutokuwa katika utimamu wa kimchezo.
Nini nafasi ya makocha?
Sasa ni dhahiri mfumo wa soka la Tanzania linatakiwa kuzalisha makipa wengine mbali ya Aishi Manula, Ali Salim, Khomeini, Mnata,Msheri na wengineo. Kwa kuwa ni nafasi ambayo inahitaji kiapji kizuri, ni muhimu maskauti wa vipaji waanze jukumu la kuwinda makipa hodari badala ya kusubiri wale wanaojitokeza kwenye vikosi vya vilabu mbalimbali. Kwenye akademi zetu za kandanda ni muhimu kutumia kila njia kuibua vipaji vipya vya soka. Ni wakati wa makocha wetu kuhakikisha wanakuja na suluhisho na makipa katika nafasi ya Taifa Stars.
Comments
Loading…