*Nigeria waingia wakijivunia historia
*Burkina Faso waingia na mkwara
Hatimaye michuano ya 29 ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) inafika ukingoni, kwa Burkina Faso kuvaana na Nigeria kwenye fainali.
Timu zote mbili zilianza kwa kusuasua, zikiwa na matumaini haba ya kusonga mbele, lakini wakafanikiwa kuvuka vihunzi vyote hadi mwisho.
Licha ya jina kubwa la Tai (Nigeria) kwenye soka, waliweka bayana kwamba walichukulia fursa ya michezo hii kujenga timu mpya.
Burkina Faso kwa upande wao, walichukuliwa kama wa kutoka mapema, lakini sasa wanafikiriwa huenda wakafanya maajabu kama Zambia mwaka jana, kwa kutwaa kombe kwa mara ya kwanza.
Burkina Faso, au Farasi Wasiohasiwa ni wa 92 katika chati ya viwango vya ubora wa soka vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Wanafundishwa na kocha Paul Put, nahodha wao ni Moumouni Dagano anayechezea Al-Sailiya ya Qatar na hawajapata kumaliza nafasi nzuri zaidi kuliko 1998 walipoandaa mashindano na kuwa wa nne.
Katika makundi ya mwaka huu, Farasi hao walishika nafasi ya kwanza kwenye kundi lao, wakawafunga Togo katika muda wa ziada kwenye robo fainali na kuwatoa Ghana kwa penati katika nusu fainali.
Nigeria kwa upande wao, wanashika nafasi ya pili katika orodha ya FIFA, na hadi jana hawakuwa na uhakika iwapo wachezaji wao nyota, Victor Moses wa Chelsea na Emmanuel Emenike wa Spartak Moscow wangecheza leo, kwani walikuwa na majeraha kidogo na walishiriki sehemu tu ya mazoezi. Hata hivyo wanaweza kucheza mambo yakibadilika na kocha wao alisema angeamua leo.
Nigeria walipata kuwika kwenye soka miaka iliyopita, ambapo Aprili 1994 walishika nafasi ya tano katika chati za FIFA, na mfungaji wao mkubwa wa kihistoria ni Rashidi Yekini.
Wanafundishwa na mchezaji wa zamani wa timu yao ya taifa, Stephen Keshi, wakati nahodha wao ni Mikel John Obi wa Chelsea.
Burkina Faso wanaingia uwanjani wakiwa na nguvu mpya, baada ya kiungo wao mahiri na mpachika mabao, Jonathan Pitroipa kufutiwa kadi nyekundu aliyopewa katika mechi ya nusu fainali.
Hata hivyo, hawatakuwa na kinara kwenye upachika mabao, Alain Traore ambaye anasumbuliwa na maumivu.
Kabla ya kuanza mashindano haya, kocha wa Nigeria, Keshi alilaumiwa na baadhi ya wadau, kwa kuchagua wachezaji sita wanaocheza ligi ya nyumbani na pia kuacha majina makubwa kama ya
Peter Odemwingie wa West Bromwich Albion na Obafemi Martins wa Levante ya Hispania.
Hata hivyo, kuna wachezaji walioonesha uhai mkubwa, kama Sunday Mba wa Warri Wolves na Godfrey Oboabona wa Sunshine Star, wanaoipa timu nguvu na kasi nzuri.
Nigeria walitwaa kombe hili mwaka 1980 na 1994 wakati Burkina Faso hawakuwa wamepata kushinda hata mechi moja nje ya ardhi yao, hadi walipoonesha cheche kwenye mashindano haya.
Keshi anaweza kuweka rekodi ya kutwaa kombe mara mbili; akiwa mchezaji na sasa kocha, na anasema anaweza kukifananisha kikosi cha sasa na alichokuwa nahodha mwaka 1994.
Katika timu hiyo, walikuwamo wachezaji mahiri kama Jay-Jay Okocha, Sunday Oliseh na golikipa Peter Rufai.
Burkina Faso walilalamika sana, kwa sababu mechi zao zote zilizopita zilikuwa kwenye dimba lenye mchanga la Nelspruit, na fainali hii itakuwa mechi ya kwanza kwenye dimba zuri.
Farasi hao, hata hivyo, hawajapata kuwafunga Nigeria, lakini historia huwa na mwanzo wake, hivyo leo wanashuka dimbani FNB, Soccer City, Johannesburg.
Kocha Put anasema wengi walikuwa na shaka naye alipowasili Ouagadougou kuanza kazi, maana walitaka kocha mwenye tambo kama Jose Mourinho.
Anasema kwamba, baada ya kuwafikisha vijana wake fainali, sasa anapokea simu nyingi kutoka kwao Ubelgiji, kwa ajili ya kazi, vipindi vya redio na televisheni.
Comments
Loading…