Fifa wamtosa ofisa mwandamizi
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limemwadhibu kwa kumpiga marufuku ofisa wake mwandamizi, Harold Mayne-Nicholls kushiriki shughuli za soka kwa miaka saba.
Mayne-Nicholls (54) aliyehusika na tathmini ya maombi ya kandarasi za kuandaa fainali za michuano ya Kombe la Dunia 2018 na 2022 amewajibishwa na Kamati ya Maadili ya Fifa.
Kiongozi huyo, hata hivyo, amepanga kukata rufaa kupinga uamuzi huo na amehoji kulikoni Fifa watangaze hatua hiyo kabla ya yeye kukamilisha mchakato wa rufaa ambao kamati imesema ni haki yake.
Mayne-Nicholls amepata kuwa Rais wa Chama cha Soka cha Chile na ni mmoja wa maofisa watano waandamizi ambao Fifa ilisema mwaka jana kwamba walikuwa wakichunguzwa.
Kiongozi huyu anakiri kuzungumza na maofisa Qatar waliokuwa wakihusika na uwasilishaji wa maombi ya nchi hiyo kupewa uenyeji. Anasema mazungumzo yao yalikuwa juu ya uwezekano wa nchi hiyo kuwapa kazi jamaa zake watatu.
Kamati ya Nidhamu ya Fifa inasema kwamba inaona majadiliano hayo yanaleta shaka tosha juu ya uadilifu uliokuwapo katika mchakato wa kukagua maombi na katika tathmini ya jumla.
Kilichomponza Mayne-Nicholls ni kuvuja kwa barua pepe kati yake na mwana kamati wa Chile wakijadili ombi lake la ajira kwa jamaa zake iwapo Qatar wangefuzu, na kweli wakafuzu.
Mayne-Nicholls alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Fifa ya Tathmini kwa ajili ya fainali za 2018 na 2022, ambapo uenyeji hatimaye ulitolewa kwa Urusi na Qatar.
Katika taarifa yake kwa Fifa mwaka 2010, Mayne-Nicholls aliyekuwa akifikiria kuwania urais wa shirikisho hilo mwaka huu kupingana na Rais Sepp Blatter alieleza wasiwasi wake mkubwa juu ya hali ya hewa ya Qatar msimu huo wa kiangazi, ambapo jotoridi hupanda hadi kufikia nyuzi 50C.
Huyu ni mmoja wa maofisa wa Fifa waliotaka ripoti ya uchunguzi juu ya mchakato wa kutoa uenyeji wa fainali hizo mbili iwekwe hadharani na kwa marefu yake yote, jambo ambalo Fifa ilikataa.
Desemba mwaka jana, Fifa iliamua kuchapisha sehemu ndogo inayozungumzia kwamba ilikuwa sahihi kisheria, lakini mwandishi wa ripoti yenyewe, Mmarekani Michael Garcia alisema ilihaririwa na kupotosha hivyo akajiuzulu.
Fifa inadaiwa kukumbwa na mkururo wa rushwa, wizi wa fedha na utakatishaji fedha miongoni mwa viongozi wake, na tayari maofisa wake saba waandamizi wamekamatwa.
Maofisa hao walikamatwa jijini Zurich siku chache kabla ya kufanyika uchaguzi wa rais wa Fifa na hadi sasa wapo rumande wakisubiri uamuzi wa maombi ya Marekani kutaka wapelekwe Marekani kujibu mashitaka.
Maofisa hao wanahusishwa na ukwapuaji wa zaidi ya pauni milioni 100 katika maeneo mbalimbali, na ulaji huo umekuwa katika kipindi cha miaka 24.