Mkataba huo, unaokadiriwa kuwa na thamani ya takriban pauni milioni 10 kwa mwaka, ulianza mwaka 2018 na umekuwa ukikosolewa kutokana na uungwaji mkono wa Rwanda kwa wanamgambo wa M23 katika migogoro inayoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mwezi Februari, Arsenal ilishtumiwa kwa kutoa dharau kwa serikali ya Kongo baada ya kudaiwa kukataa kukutana na waziri wa mambo ya nje, Thérèse Kayikwamba Wagner, kujadili mkataba huo.
Visit Rwanda ni kitengo cha Bodi ya Maendeleo ya Rwanda, ambacho ni idara ya serikali, na inaaminika Arsenal ilisaini na kuendeleza ushirikiano huo ili kukuza idadi ya mashabiki wao barani Afrika. Hata hivyo, mpango huo sasa umefikia mwisho baada ya pande zote mbili “kukubaliana kwa pamoja” kuachana.
“Tangu awali, Arsenal na Bodi ya Maendeleo ya Rwanda wamepitiliza malengo ya mkataba—kukuza uhifadhi wa mazingira na utalii endelevu, kuhamasisha mamilioni ya mashabiki kugundua nchi hiyo, na kuweka msingi imara wa ukuaji wa utalii,” ilisomeka taarifa ya Arsenal. “Ushirikiano huo pia umeunga mkono azma ya Rwanda kuwa kitovu cha michezo kimataifa barani Afrika na kuandaa matukio zaidi ya michezo duniani, sambamba na kuendesha programu za soka ngazi ya chini zilizowasaidia mamia ya vijana na makocha kukuza ujuzi wao na kuongeza ushiriki katika michezo.”
Richard Garlick, afisa mkuu mtendaji wa Arsenal, alielezea ushirikiano huo kama “safari muhimu” na kudai kuwa umekuwa “ukiisukuma mbele” ndoto ya klabu. Lakini si hivyo mashabiki wote wa Arsenal walivyouchukulia, kwani kundi la wanaharakati Gunners for Peace lilifanya maandamano nje ya Uwanja wa Emirates wakati wa mechi ya kwanza ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Paris Saint-Germain mwishoni mwa Aprili, wakibeba bango lililosomeka “Drop Visit Rwanda”. Pia waligawa vibandiko vya mkono kufunika nembo ya Visit Rwanda kwenye jezi.
Katika mwezi huo huo, PSG waliongeza mkataba wao wa udhamini na Visit Rwanda hadi 2028, huku Atlético Madrid wakitia saini mkataba mpya wa muda huo huo ambao umepelekea nembo ya Visit Rwanda kuonekana kwenye jezi za timu ya wanaume na wanawake ya klabu hiyo ya Hispania.

