SEPTEMBA 3 mwaka huu bondia wa Tanzania Hassan Mwakinyo alipanda ulingoni jijini Dar es salaam kuvaana na mpinzani wake Julius Indongo raia wa Namibia. Pambano hilo lilikuwa na raundi 12 kuwania ubingwa wa ndondi Afrika.
Mwakinyo alikuwa anatetea mkanda wake dhidi ya Mnamibia huyo. Pambano hilo lilitanguliwa na mengine kadhaa ambapo baadhi ya mabondia walionesha umahiri na ufundi wao katika mchezo.
Miongoni mwa mabondia waliovutia ni Tony Rashid wa Tanzania ambaye licha ya kuchapwa lakini alionesha umahiri mkubwa wa kucheza masumbwi, huku baadhi ya washabiki wa mchezo huo wakiwa na matumani kuwa atakuja kuwa hodari siku za usoni.
Na zaidi pambano hilo lilikuwa linaonesha ladha nyingine ya Azam TV ambao wanafanya juhudi kurudisha hadhi ya ndondi nchini Tanzania kama ilivyokuwa zama za mabondia mahiri Rashid Matumla, Mbwana Matumla, Hassan Matumla, Chaurembo Palasa na wengine wengi wa zamani.
Kwamba mchezo huo ambao ulipoteza umaarufu miaka kadhaa nyuma umerudishwa kileleni baada ya Azam TV kuutangaza na kuhamasisha wadau na washabiki kurudisha mapenzi yao kwenye mchezo huo.
Tukirudi katika pambano la Mwakinyo baadhi ya watanzania wanakejeli uwezo wa Julius Indongo, na kuibua kila aina ya sababu kushutumu uwezo wake. Wanajaribu kueleza kuwa bondia huyo hakuwa na uwezo wa kupambana na Mwakinyo. Lakini wanasahau kuwa taratibu zimefuatwa na kujiridhisha kuwa mpinzani wa Mwakinyo alikuwa na sifa zote kupanda ulingoni.
Katika pambano hilo Julius Indongo aliangushwa mara mbili katika pambano hilo. Na zaidi Mnamibia huyo alionekana kukosa stamina, hivyo kupoteza uwiano (balance) wakati wa kuhimili mashambulizi ya Mwakinyo na kujilinda.
Mchezo huo ulikatishwa na mwamuzi kwa kile alichokiona Julius Indongo hawezi kuendelea na pambano hilo kwa vile alikuwa amezidiwa na mpinzani wake Hassan Mwakinyo.
Kikanuni bondia akipigwa ngumi 10 mfululizo bila kujibu mashambulizi, mwamuzi anaruhusiwa kumaliza (kukatisha pambano). Ingawa ni kweli Mwakinyo hakupiga ngumi 10 mfululizo lakini hali ya bondia Julius Indongo ilitia wasiwasi kwani tayari alishakuwa amepoteza mwelekeo au kama wasemavyo vijana alipoteza ‘network’.
Kama mwamuzi angechukua sheria ya bondia kutoa mwili nusu nje ya ulingo basi ilibidi Mwakinyo apewe ushindi mapema sana. Kwa sababu Julius Indongo alishambuliwa mara tatu mfululizo kisha akapoteza mwelekeo hivyo nusu ya mwili wake ukawa nje ya ulingo.
Nakumbuka kuona moja ya mapambano ya bondi maarufu wa Afrika kusini Francis Botha akitangazwa kupigwa baada ya kushambuliwa na nusu mwili wake kutoka nje ya ulingoni (kwenye kamba). Mwamuzi aliashiria Botha asingeweza kuendelea na pambano kwa sababu hiyo na ilikuwa njia ya kumlinda asipigwe zaidi.
Upande chanya wa bondia Indongo alionesha uzoefu na ufundi ulingoni ambapo baadhi ya makonde yake yalitua sehemu sahihi katika uso wa Mwakinyo. Ni sababu hiyo Mwakinyo alilazimika baadhi ya raundi kutumia kujilinda kwa kuficha uso na kulikinga tumbo ili kuvuta nguvu na kumchosha mpinzani wake.
Aidha, kwenye pambano hilo Mwakinyo ameonesha wazi kuimarisha uwezo wake wa kujilinda, jambo ambalo mapambano ya nyuma alikuwa na kiwango cha chini cha kujilinda. Kwenye pambano dhidi ya bondia Tianampay raia wa Ufilipino ndipo Mwakinyo alionesha namna anavyojifua mbinu za kujilinda.
Mfilipino yule alikuwa anashambulia kwa kasi na mfumo wake unafanana na ule Pacmann. Kama si uwezo wa kujilinda basi Mwakinyo angekuwa anapigwa mara nyingi kifundi. Kila pambano anajaribu kuonesha mabadiliko, na dhidi ya Mnamibia hakuwa na kazi kubwa ya kujilinda kwa sababu mpinzani wake alipendelea mashambulizi ya mbali kuliko ya karibu.
Indongo ni bondia ambaye amewahi kuwa bingwa wa dunia wa IBF mwaka 2017. Baadaye alivuliwa ubingwa huo na bingwa namba mbili wa uzito wake Terence Crwaford nyuma ya Errol Spence ambaye pia alishindikana katika masumbwi kwenye uzani wa Middle Welter.
Hii ina maana Mwakinyo alikutana na bondia mwenye sifa stahiki na amefanikiwa kushinda. Mwakinyo ni bondia nambari moja barani Afrika kwa sasa, na nambari 24 duniani.
Tunaweza kukejeli na kuona Mwakinyo anabebwa au kupendelewa, lakini ukweli ni kwamba anafanya akzi nzuri na kubwa kufika mahali alipo. Kwa desturi Watanzania wanapenda kuwashusha mashujaa wao badala ya kuwajenga na kuwalinda.
Wao wanapenda kuona mtu anashushwa badala ya kuendelea kumfanya awe juu zaidi ya alipo sasa. Ni utamaduni wa husda na roho mbaya tu ili kuona Mwakinyo anaharibikiwa. Ni wivu ambao unatutafuna kila kukicha na kujitahidi kutamani Mwakinyo ashindwe.
Ndio maana tunahangaika kumtafutia uadui na Twaha Kiduku ambaye hajafika hata robo ya mafanikio ya Mwakinyo apambane kwa kile kinachoitwa “nguvu ya wadau”.
Ukiangalia nyuma ya nguvu za wadau hao ni wivu,husda na kutaka kumshusha Mwakinyo bila sababu, lakini kila kukicha tunajisifu na kuwafisiwa wazungu wanapopanda na kufanikiwa na kuatak tuige kwao wakati mashujaa wetu tunataka waanguke.
Ilitokea hivyo kwa Nassib Abdul mwenye lakabu ya Diamond Platinumz ambapo baadhi ya watanzania walikuwa tayari kuona Nigeria inashinda kwenye tuzo za BET kuliko raia wao,kijana wao,mtoto wao Diamond Platnumz akinyakua tuzo hizo. Ni wivu,husda,roho ya korosho tu inatusumbua.
Mwakinyo anastahili pongezi na kila mdau wa michezo na burudani. Mwakinyo anastahili kuungwa mkono kwa juhudi alizofanya,alikotoka,kuzishinda changamoto na mengine mengi. Sababu tunazotumia kutaka kumshusha hazihusiani na fani yake, bali ile roho ya kuona ameshushwa. Nadhani tutakuwa taifa la watu wa ajabu sana lenye kuwakumbatia wageni kuliko rasilimali zao.
Comments
Loading…