Kuna mvutano umeibuka juu ya jinsi Bodi ya Ligi Kuu ya England (EPL) inavyotakiwa kupokea na kuchukua hatua kutokana na kuzuka kwa maradhi yanayosababishwa na kirusi cha Corona.
Mamlaka za soka zimekuwa zikitaka kuendelea kwa michezo ya soka nchini England na Wales iliyo chini ya EPL na EFL, lakini serikali inatarajiwa kuchukua uamuzi wa kuchukua hatua kudhibiti kuenea kwa virusi vya ugonjwa huo.
Hatua zinazodhaniwa kwamba zinaweza kuchukuliwa ni ama kuahirisha mechi kwa muda au baada ya kujiridhisha kwamba wachezaji na maofisa wao wapo salama kiafya, wacheze bila kuwapo watazamani.
Zipo taarifa kwamba tayari baadhi ya wachezaji timu za EPL wameambukizwa. Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta kaambukizwa na pia mchezaji wa Chelsea, Calum Hudson Odoi. Leicester kuna hofu na pia katika klabu nyingine.
Baadhi ya nchi za Ulaya zimezuia mikusanyiko inayozidi watu 1,000, nyingine zikiamua mechi zichezwe bila watazamaji lakini nyingine, kama Italia – walioathirika zaidi kwa virusi hivyo na vifo katika Ulaya – wamesitisha Ligi Kuu – Serie A hadi mwezi ujao. Beki wa kati wa Juventus na Timu ya Taifa ya Italia, Azzurri – Daniele Rugani amepima na kukuta ana virusi vya Corona.
Na hata mwezi ujao, hakuna uhakika iwapo ligi itaendelea kama kawaida, kwani itategemea kasi ya kuenea kwa virusi hivyo na hali za watu, kwani tayari kuna wachezaji wanaodaiwa kwamba wameathiriwa.
Mataifa kama Italia, Hispania, Ufaransa na mengineyo tayari yamechukua hatua na mashirikisho yao ya soka kupokea maagizo ya serikali. Wachezaji wa Real Madrid, kwa mfano, sasa wamewekwa kwenye karantini ya wiki mbili baada ya mmoja wa wachezaji wao wa mpira wa kikapu kuambukizwa virusi hivyo.
Japokuwa hadi jana EPL walikuwa wamekataa kuzungumzia suala hilo, maofisa wa serikali walikuwa katika vikao kwa ajili ya kuhakikisha wanadhibiti kuenea kwa virusi hivyo, na kuna kila dalili kwamba mechi zitaathiriwa.
Watu zaidi ya 450 wamethibitishwa kuambukizwa ugonjwa huo nchini Uingereza, hivyo serikali itachukua hatua kwa ajili ya kudhibiti kuenea kwake, ikiwa ni pamoja na kuzuia mikusanyiko.
EFL wanataka kupata ufafanuzi kutoka kwa EPL juu ya kipi kitatokea na wajipangaje na mikakati wanapoelekea kwenye mwisho wa msimu wa soka wa 2019/2020. Lakini tayari kuna mvutano baina ya bodi hizo mbili za ligi hizo na hata miongoni mwa klabu zinazoshiriki.
Hatua moja ilipata kuchukuliwa ya kuahirisha mechi baina ya Arsenal na Manchester City iliyokuwa ichezwe juzi Jumatano, baada ya baadhi ya watu wa Arsenal kuwa wamekutana na mmiliki wa Olympiakos ambaye amejitangaza kwamba ameambukizwa virusi hivyo. Kadhallika kusalimiana kwa kupeana mikono kabla ya mechi kumezuiwa kama moja ya hatua za kuzuia kuenea kwa virusi husika.
Klabu za EFL zimekuwa zikipinga sana mpango wa kucheza mechi zao bila kuwapo watazamaji uwanjani kwa sababu za gharama za kifedha, kwani watapoteza mapato ya siku za mechi husika na wamebaki na matumaini kwamba msimu utamalizika kama ulivyopangwa au hata kwa kuahirishwa kwa muda.
Tayari imeelezwa kwamba Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa) linafanya kikao Jumanne wiki ijayo kujadili jinsi ya kuchukua hatua kuhusiana na Corona. Shirikisho hilo linasema kwa sasa mechi za ligi za nchi mbalimbali, Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL), Ligi ya Europa na Euro 2020 zitajadiliwa kujua kipi kinafanywa na iwapo ratiba zipanguliwe.
Real Madrid walikuwa wamepangwa kucheza na Manchester City kwenye UCL Jumanne wiki ijayo kikao hicho kinapokaa na haijajulikana itakuwaje, japokuwa kuna uwezekano wa Real kutosafiri kwenda Etihad, Manchester, kwani tayari wapo chini ya zuio la karantini ya wiki mbili. Klabu hizo na shirikisho wanatarajiwa kujadiliana na kutoka na suluhisho.
=-=