Kocha Mkuu wa Manchester United, David Moyes amewaandikia barua mashabiki wa klabu hiyo, akiwashukuru kwa kumuunga mkono katika kipindi hiki kigumu.
Moyes ambaye timu yake inapepesuka kwenye msimamo wa ligi na imeshatupwa nje ya mashindano mawili makubwa, amekiri kwamba washabiki wamebaki kuwa waaminifu kwa klabu na kwamba msimu wake wa kwanza Old Trafford umekuwa mbaya.
Moyes aliyepokea kijiti kutoka kwa Sir Alex Ferguson anashuhudia timu yake ikiwa vibaya, ambapo katika mechi 27 imeshinda 13 tu, na katika jarida lililotumwa kwa washabiki wanaonunua tiketi za muda mrefu, Moyes anasema hakutarajia mambo yawe hivyo.
Hao ni aina ya washabiki wanaoweza kununua tiketi za mechi nyingi, wakati mwingine mwezi mmoja, nusu msimu au hata msimu wote kulingana na mechi wanazotaka kuzitazama za klabu hiyo. Kwa mwenendo wa timu, ina maana washabiki hao wanasikitika kwani hawakununua tiketi ili mara kwa mara washuhudie klabu inafungwa.
Wanaofaidi sasa ni wale wanaonunua tiketi kadiri mechi zinavyotokezea, lakini wanaweza kupatwa na hatari ya kukosa tiketi, hasa timu inapoanza kufanya vizuri. Nchini Uingereza tiketi huuzwa na kudhibitiwa na klabu mwenyeji, ambaye humgawia klabu mwenyeji idadi wanayokubaliana.
Moyes (50) aliyechukua nafasi ya Mskochi mwenzake, Fergie, ameshuhudia Mashetani Wekundu wakifungwa Old Trafford ambayo haikuwa kawaida, na timu zilizowabomoa hapo ni West Bromwich Albion, Everton, Newcastle na Tottenham Hotspur.
Kadhalika walifungwa na Swansea kwa mara ya kwanza katika historia ya timu hiyo na sasa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya wanatakiwa kupindua ushindi wa 2-0 wa Olympiakos na kuongeza bao la ushindi ili wasonge mbele.
“Mmezoea kuiona Manchester United yenye mafanikio, uungwaji mkono mliowapa wachezaji na mimi katika muda wote huu si wa kawaida. Washabiki wanaosafiri kutushabikia ugenini wamekuwa wema mno kwetu katika mechi na ni wa kupigiwa mfano nchi nzima na hapa Old Trafford hakuna anayeweza kuwayumbisha.
“Imekuwa ngumu lakini mmebaki nasi hata wakati timu inafungwa, sina wasiwasi kwamba katika muda mfupi ujao tutashuhudia tena ile Man United yenye kushinda mechi zake,” akasema Moyes.
Comments
Loading…