*Real Madrid wapiga 2-1, Nani kadi nyekundu
*‘The Only One’ ajidai kuliwaza, kusifu Man U
Manchester United wameaga Ligi ya Mabingwa Ulaya, baada ya kukubali kichapo cha jumla ya mabao 3-2 kutoka kwa Real Madrid.
Vijana wa Jose Mourinho ‘The Only One’ waliingia Old Trafford wakiwa na ulazima wa kufunga walau bao moja ili wawiane na United.
Lakini walikuwa Man U waliotangulia kucheka, baada ya nahodha wa Real, Sergio Ramos kujifunga wakati akijaribu kuokoa majalo ya Luís Carlos Almeida da Cunha ‘Nani’ karibu na mstari wa goli dakika ya 48.
Hata hivyo, alikuwa Nani tena aliyesababisha tafrani na pengine kubadili mwelekeo wa mchezo, baada ya rafu mbaya dhidi ya Alvaro Arbeloa.
Mwamuzi kutoka Uturuki, Cuneyt Cakir alimtoa nje Nani kwa kadi nyekundu, jambo lililosababisha taharuki kutoka kwa wachezaji na kocha Alex Ferguson, aliyeshuka alikokuwa na kulalamika mbele ya mwamuzi wa akiba.
Arbeloa aliyeshindiliwa guu na Nani tumboni, alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Luka Modric, ambaye hakuchukua muda mrefu, akasawazisha bao katika dakika ya 66.
Modric aliyechezea Ligi Kuu ya Uingereza akiwa Tottenham Hotspurs kabla ya kulilia kwenda Real Madrid alikoanza kwa kusuasua, alifunga bao kwa kumzunguka Michael Carrick kabla ya kuachia kombora kutoka yadi 25 lililomshinda kipa David De Gea baada ya kugonga mwamba na kutinga nyavuni.
Kijana wa zamani wa Old Trafford, Cristiano Ronaldo hakuondoka bila kuacha alama yake, kwani aliipatia timu yake bao la pili na la ushindi katika dakika ya 69.
Aliunganisha majalo ya Gonzalo Higuan na kupasua nyoyo za washabiki wa Manchester United waliotaka kuona timu yao ikisonga mbele, lakini pia wakikumbatia tetesi kuwa Ronaldo atasajiliwa tena kwao.
Ronaldo hakushangilia bao hilo, japo wenzake walimzunguka na kufurahia, kutokana na heshima kubwa anayosema anayo kwa Ferguson aliyemkuza kisoka. Hata hivyo, alimdhuru.
Kwa ushindi huo, Real Madrid wameingia robo fainali ya michuano hiyo mikubwa zaidi Ulaya, ambapo mmoja wa mashujaa wao wakubwa alikuwa golikopa Diego Lopez aliyeokoa magoli mengi ya wazi.
United, pamoja na kubaki wachezaji 10, walijitutumua dimbani, wakikaba na kushambulia vilivyo, waliokuwa mstari wa mbele wakiwa Danny Wellbeck, Robin van Persie, Wayne Rooney na nahodha wao, Nemnja Vidic aliyepiga kichwa na kuparaza mlingoti wa goli.
Muda mfupi baada ya kadi nyekundu kutolewa, Mourinho alimsogelea Ferguson na kumnong’oneza jambo, na baada ya mpira, Mourinho alisema kwamba bila kuangalia kadi nyekundu, timu bora imefungwa na kwamba wachezaji wake hawakucheza vizuri.
Ni Mourinho aliyekuwa amejiandaa kucheka tangu mwanzo, ambapo kabla ya mechi alisema dunia yote ingesimama kushuhudia mtanange huo alioufananisha na fainali.
Kwa ushindi wake huo, Mourinho anawasogeza Real Madrid mbele kusakakombe, kwa mbinu zake nyingi za ulinzi wa uhakika, mashambulizi ya aina mbalimbali, yakiwamo ya kushitukiza.
Katika muongo mmoja uliopita, amefanikisha kazi hiyo akiwa na timu tofauti, kama Chelsea, Inter Milan na sasa Real Madrid.
Ndani ya wiki moja iliyopita, aliwaadhidi Barcelona kwa kuwafunga mara mbili – nyumbani Bernabeu na Camp Nou.
Huenda mwaka huu ukawa kama 1996, ambapo England haikuwa na timu yoyote kwenye hatua ya robo fainali, kwani Chelsea na Manchester City walishatolewa na Arsenal wapo ukingoni wanapoelekea Ujerumani wiki ijayo.
Baada ya mechi Rio Ferdinand alimwendea mwamuzi na kujidai kumpigia makofi kana kwamba anampongeza, bila shaka kuonesha kuudhiwa na uamuzi wake wa kumpa kadi nyekundu Nani, na pengine kuwanyima penati kadhaa walizodhani walistahili.
Katika mechi nyingine, Borussia Dortmund wamefanikiwa kutinga robo fainali, baada ya kuwachabanga Shakhtar Donetsk mabao 3-0, ambapo wamevuka kwa jumla ya mabao 5-2.
Comments
Loading…