MATUMAINI ya Morocco kuandaa fainali za Kombe la Dunia 2026 yamezdi kuongezeka, huku ikidhaniwa kwamba kuna wanachama wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kutoka Amerika ambao hawatapiga kura. Mchuano wa uenyeji wa fainali hizo umekuwa mkubwa, ambapo watu walio ndani ya Fifa wanasema kwamba Morocco wanazidi kupewa nafasi kadiri muda unavyokwenda.
Wakipata watakuwa nchi ya pili Afrika kuandaa fainali hizo baada ya
Afrika Kusini. Wanachuana na muungano wa mataifa ya Amerika –
Marekani, Mexico na Canada wanaotaka kuandaa kwa pamoja.
Hapana ubishi kwamba mataifa hayo matatu kuwa wenyeji kunaweza
kuonekana kwamba ni mbadala salama zaidi na wneye kuvutia kifedha
lakini hiyo haitoshi kuwahakikishia kura kutoka kwa mashirikisho
wanachama wa Fifa.
Nafasi yao ya kushinda kete hii ya uenyeji ilidhaifishwa kwa sababu ya
kuibuka kwa mzozo miongoni mwa himaya za Marekani za Guam, Puerto
Rico, American Samoa na US Virgin Islands kutokana na mgongano wa
kimaslahi.
Hii ni kura ya kwanza kwa ajili ya uenyeji wa fainali za Kombe la
Dunia tangu England walipopatwa pigo kubwa kwa kushindwa kupata
uenyeji wa fainali za mwaka huu wakati Urusi na Qatar walipochaguliwa
kuwa wenyeji wa 2018 na 2022 licha ya kuonekana dhaifu kinadharia
kwenye karatasi.
Tuhuma na shutuma nyingi juu ya rushwa kwenye shirikisho hilo katika
kupata wenyeji hao na mabadiliko makubwa ya kiungozi na hata viongozi
kukamatwa na kushitakiwa kwa rushwa, kunaonesha kwamba mambo yatakuwa
tofauti sana safari hii na uwazi utatawala.
Inatarajiwa kwamba mashirikisho wanachama 201 kati ya 211 watapiga
kura kwenye mkutano wa mwaka wa baraza la Fifa unaofanyika leo
Jumatano Expocentre, Moscow.
Mataifa manne yanayowania uenyeji hayatapiga kura wakati Ghana na
Kosovo wanajulikana kwamba hawakutuma mwakilishi. Serikali ya Ghana
imevunjilia mbali shirikisho la soka la nchi hiyo kutokana na sababu
za rushwa kukithiri humo.
Wakuu wa Fifa, akiwamo Rais Gianni Infantino – wanatambulika kwamba
wangependa kuona maombi ya Marekani na washirika wake yakikubaliwa kwa
kura, maana wameahidi (waandaaji) kwamba yakifanyika humo yatazalisha
faida ya pauni bilioni 8.1 ikilinganishwa na ya pauni bilioni 4.4.
inayotarajiwa kupatikana iwapo mashindano yatafanyika Morocco. Hata
hivyo, kuna sababu nyingine za kijiografia, kisiasa na kisoka za
kuzingatia kabla ya uamuzi kuchukuliwa.
Baadhi ya watu wanaopendelea maombi ya muungano wa nchi hizo za
Amerika wana wasiwasi kwamba kuingilia kwenye kampeni kwa Rais Donald
Trump wa Marekani kunaweza kuwa kumewaharibia.
Aprili mwaka huu aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa jamii wa
Twitter akisema; “Marekani imeweka kwa pamoja ombi zito na Canada na
Mexico kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia 2026. Itakuwa fedheha
iwapo nchi tunazozisaidia siku zote zitafanya kampen dhidi ya ombi la
Marekani. Kwa nini tuwe tunazisaidia nchi hizi ikiwa hazishirikiani
nasi (pamoja na Umoja wa Mataifa)?”
Ni maoni ya baadhi ya watu kwamba utata wake unaweza kusababisha
baadhi ya mataifa kuamua kuwapinga na kwenda na Morocco. Lakini pia
mzozo ulioibuka baina ya Trump na Waziri Mkuu wa Canada, Justin
Trudeau kunaweza kufisha nguvu ya ushirika wa waandaaji wenza hao.
Hata hivyo, inadaiwa kwamba nyuma ya pazia Trump amekuwa akipiga
kampeni, ikiwa ni pamoja na kuandika barua tatu kwa Infantino na
maofisa wengine wa Fifa, akiwahakikishia kwamba msimamo wake mkali
hautaathiri masuala ya visa kwa wageni kuingia Marekani.
Pamoja na hayo, jopo la wana kampeni wa Morocco kwa ajili ya kuandaa
mashindano hayo walikuwa na imani kwamba wangeweza kubadili mawazo ya
baadhi ya nchi wanachama wa Fifa na kuwaunga wao mkono.
Walikuwa wakiendelea na kampeni hizo kwenye vyumba na korido za hoteli
mbalimbali na baa jijini Moscow hadi muda wa mwisho ukikaribia.
Watakuwa na muda wa dakika 15 kwa ajili ya kuwasilisha mada mbele ya
baraza leo asubuhi kushawishi wajumbe ili wapate kura.