Wakati dirisha la usajili lilipokuwa lianendelea taarifa za mchezaji wa Morice Abrahm kurudishwa nchini na klabu aliyokuwa akichezea lilivuma kwa kiasi kidogo. Wakati huo Morice Abraham alikuwa akitumikia timu ya Taifa kwenye mashindano ya CHAN. Baadaye ziliibuka taarifa kuwa aliyekuwa kocha wa Simba Fadlu Davids alimhitaji kiungo huyo na ndiyo sababu alikuwa akifanya majaribio ya kujiunga na miamba hiyo ya soka nchini na Afrika. Kwa sasa imebaki kuwa simulizi pekee kwani tayari Morice Abraham ni mali ya klabu ya Simba na amecheza mechi mbili za hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United. Baada ya michezo hiyo miwili TANZANIASPORTS inachambua kwa kina juu ya mwenendo wa staa huyo kuitaka namba katika kikosi cha kwanza cha Simba.
Tishio kwa Jean Ahoua
Jean Ahoua ni kiungo mzuri sana katika klabu ya Simba. Mbinu za kocha Fadlu Davids zilikuwa zinaanzia kwa kiungo huyo mshambuliaji. Unapozungumzia mifumo ya Simba katika kupambana na wapinzani wake moja kwa moja unamtaja Jean Ahoua kama silaha yao ya kwanza ya kusaka ushindi. Mashambulizi mengi ya huundwa katikati ya dimba na kwenda kushoto au kulia na eneo la hatari huwa yanatokea kwenye miguu ya Jean Ahoua. Pamoja na kuwa na tegemeo, Jean Ahoua amekuwa akikosa mabao mara nyingi.

Katika mchezo dhidi ya Gaborone United, alikuwa na nafasi ya kupachika mabao mengi lakini hakufanikiwa. Katika maizngira hayo, Morice Abraham anaweza kuwa tishio kwa namba ya Jean Ahoua. Morice Abrahm anafunga mabao, anapiga mashuti, ana nguvu (stamina) na zaidi anajua kupika mabao. Katika mfumo wa washambuliaji watatu anaweza kutumikia nafasi hii. Kwhaiyo ni tishio kwa kiungo huyu.
Namba ya Kibu Denis hatarini
Morice Abraham licha ya kucheza eneo la kiungo mshambuliaji pia anaweza kutumika kama winga wa kushoto. Eneo la winga wa kushoto ndiko anakocheza Kibu Denis ambaye amehodhi namba hiyo kwa muda mrefu. Ujio wa Morice Abraham unamfanya Kibu Denis kuumiza kichwa na kutafuta namna bora ya kurudisha makali yake. ushindani katika namba hii utasaidia Simba kupata ubora wa wachezaji hao. Kwahiyo Kibu Denis akizembea basi namba yake inachukuliwa kikosi cha kwanza.
Mukwala na Mwalimu
Morice Abraham naaweza kutumika kama mshambuliaji yaani nambari 9 ikiwa kocha wa Simba ataamua hilo. Katika mfumo wowote Simba wanaweza kushuhudia ushindani mkubwa katika safu ya ushambuliaji na hivyo kuwa tishio kwa Suleiman Mwalimu ‘Gomes’ na Stephen Mukwala. Safu ya ushambuliaji ya Simba inahitaji mtu wa mabao na mwenye kutumia nafasi vizuri. Katika mfumo wowote Morice Abraham anaweza kusimama kama mchezaji wa kupachika mabao. Sasa ushindani wa safu ya ushambuliaji haupo kwa Mwalimu na Mukwala peke yake bali ingizo la Morice Abraham ni kengele ya hatari kwa washambuliaji hao.
Chasambi na Mutale
Morice Abraham kama ambavyo imelezwa mwanzoni anaweza kucheza nafasi ya winga wa kushoto au kulia, anaweza kupora namba kati ya Chasambi na Joshua Mutale. Wachezaji hao wanaweza kucheza eneo la winga wa kulia na kushoto lakini wanazidiwa kiasi kidogo na Morice Abraham. Katika mfumo wa kutegemea mawinga, Morice Abraham anakuwa mchezaji mwenye nguvu na uwezo wa kupambania namba katika kikosi cha kwanza. Hii ni changamoto kwa wachezaji wa Simba kwenye nafasi hizo.
Faida ya ziada ya Morice Abraham
Kiungo huyo ana faida ya kusaidia ulinzi. Katika mfumo wa viungo watatu katikati ya dimba, mfano akiwa na Jean Ahoua na Yusuf Kagoma anaweza kumpunguzia majukumu kiungo mkabaji. Hii ina maana katika suala la kusaidia ulinzi Morice Abraham yuko mbali sana kuwazidi Ahoua, Mukwala, Mutale na Chasambi.
Kwa maana hiyo kocha wa Simba atahitaji mchezaji ambaye anaweza kumpa vitu adimu vya kushambulia na kujilinda. Katika maizngira hayo, nafasi ya kikosi cha kwanza inapata ushindani, huku Morice Abraham akiwa na machaguo mengi ya kucheza ndani ya dimba. Kocha wa Simba ataamua amtumie wapi Morice Abraham, kama ni winga, kiungo au mshambuliaji. Hili ni jukumu ambalo benchi la ufundi linatakiwa kuamua namna bora ya kupata ubora wake.