Moja ya vipaji ambavyo viliwabeba Simba msimu uliopita Mohammed
Ibrahim ni moja wapo.
Alihusika katika upatikanaji na ufungaji wa magoli muhimu katika timu.
Ingawa timu ilikosa kombe kwa tofauti ya wingi wa magoli ya kufunga na
kufungwa, lakini mchango wake ulitosha kuonesha yeye alikuwa ni mmoja
wa mihimili imara ya Simba kufanya vizuri msimu uliopita.
Alionesha yeye ni moja ya viungo ambao wana madhara chanya ya moja kwa moja.
Kwani alikuwa na uwezo mkubwa wa kufunga pamoja na kutengeneza magoli.
Hiki ndicho kitu ambacho kiungo wa kisasa anatakiwa akifanye uwanjani
ili kutimiza majukumu ipasavyo kwenye timu.
Kiungo ambaye anauwezo wa kutengeneza magoli kuanzia matano na kufunga
magoli kuanzia matano kwenye ligi yenye mechi 26 ni kitu kikubwa sana
kwenye soka la kisasa.
Kwani timu inakuwa na njia mbadala ya wafungaji pindi ambapo eneo
fulani la timu likiwa limebanwa.
Mfano, Msimu huu Simba inaonekana kuimarika zaidi katika eneo la
ushambuliaji la timu togauti na msimu Jana.
Kuimarika kwao katika eneo la ushambuliaji haimanishi kuwa , watu
walio katika eneo la ushambuliaji ndiyo watakuwa wanahusika kila mechi
kufunga.
Timu bora na imara ni ile ambayo inakuwa na usaidizi mzuri wa majukumu
ndani ya kiwanja.
Timu bora na imara ni ile ambayo wachezaji wengi kwenye timu
wanahusika katika ufungaji wa magoli.
Sikatai kuwa katika timu kuna kuwa na mfungaji wa timu ambaye
tunamwita ( main target).
Kuna wakati huyu ( main target) hushindwa kuibeba timu kutokana na kubanwa.
Ndipo hapo njia mbadala inapotakiwa kutumika.
Na njia mbadala nzuri kwenye timu ni kuwa na wachezaji wengi ambao
wana uwezo wa kubadirisha matokeo wakati wowote.
Wachezaji ambao wanaweza kufunga na kutengeneza nafasi za kufunga kwenye timu.
Wachezaji ambao wana uwezo binafsi wa kufanya kitu kikubwa kwenye mechi husika.
Ndipo hapo unahitaji kuwa na Mohammed Ibrahim kwenye timu yako.
Mtu ambaye hana nafasi kwenye kikosi cha Simba, na nafasi yake ni
ngumu kurudi kwa sababu eneo analocheza yupo kipenzi cha wana Simba.
Ni ngumu kumweka nje Haruna Niyonzima kwenye mbao, na kumwingiza
Mohammed Ibrahim kwa sababu Haruna Niyonzima ni kipenzi cha WanaSimba
na Viongozi wa Simba.
Haruna Niyonzima amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwa kipenzi cha Wana
Simba na viongozi wa Simba lakini hajafanikiwa kuwa kipenzi cha timu
ndani ya uwanja.
Hajafanikiwa kuwa na madhara chanya ya moja kwa moja kwenye timu,
hajafunga wala kutoa pasi ya mwisho ya goli.
Haya ndiyo majukumu yake ya msingi, lakini hajayatimiza kwa asilimia
kubwa kitu ambacho kitaaluma hakimpi nafasi ya yeye kuanza moja kwa
moja kwenye kikosi cha kwanza cha Simba.
Lakini utaanza vipi kumweka benchi mtu ambaye amenunuliwa kwa pesa
kubwa, tena kutoka katika wapinzani wao wakubwa nchini .
Mtu ambaye ni furaha ya mashabiki wa na viongozi wa Simba?
Hakuna kocha mwenye ujasiri wa kumweka benchi kipenzi cha mashabiki na
viongozi wa Simba katika mazingira yetu ya mpira hapa Tanzania
tunavyoyajua.
Ndiyo maana inakuwa vigumu Mohammed Ibrahim kupata nafasi kwenye
kikosi cha Simba.
Hapati nafasi siyo kwa sababu ni mchezaji mbovu.
Hapati nafasi siyo kwa sababu hana uwezo mkubwa wa kucheza mpira.
Kitu ambacho kina mnyima nafasi ni Niyonzima.
Huyu ndiye anayemkaba Mohammed Ibrahim, ni ngumu kwake kupata nafasi
wakati ambao Niyonzima yupo katika utimilifu wake wa Afya ya kimwili.
Ingawa kwenye mizani, Niyonzima hana madhara makubwa chanya ya moja
kwa moja kama ilivyo kwa Mohammed Ibrahim.
Lakini kinachompa nafasi ni yeye kuwa kipenzi cha wengi.
Yeye kuwa moyo wa msimbazi, mahaba yote wamemwachia yeye, ni dhambi
kubwa kwa kocha kumweka benchi kipenzi chao .
Raha ya mashabiki wa Simba ni kumuona anacheza, kwao zile chenga
ambazo hazina faida ndiyo burudani kwao.
Ule ufundi wa kuchezea mpira kusiko na faida ni burudani kwao.
Ni ngumu kwa Mohammed Ibrahim kukaa kwenye mioyo ya mashabiki wa Simba
kama alivyowakaa Niyonzima kwa sababu Mohammed Ibrahim hana chenga za
maudhi za kuwaburudisha mashabiki , kwa sababu yeye hakusajiliwa kwa
mbwembwe na pesa ndefu kama Niyonzima.
Njia pekee ya yeye kucheza mpira kwa sasa ni kutafuta sehemu ambayo
atakuwa huru kucheza mpira.
Sehemu ambayo atapewa nafasi ya kucheza Mara kwa Mara.
Hiki ndicho ambacho kitamsaidia kuokoa kipaji chake.
Siyo dhambi kabisa kwake kutokea mlango aliotumia Ajib na Tambwe.