Mwanariadha mashuhuri wa Uingereza mwenye asili ya Somalia, Mo Farah amejitoa kwenye michuano ya Jumuiya ya Madola inayofanyika Glasgow, Scotland.
Farah alikuwa akimbie katika mbio za meta 5,000 na 10,000 lakini amekwama baada ya kuugua, ambapo amesema mwili wake haupo fiti kwa kazi hiyo.
Kujiondoa kwa Farah ambaye kwenye michezo ya Olimpiki iliyofanyika England alitwaa medali mbili za dhahabu ni pigo kwani ni mmoja wa wachezaji mahiri waliotarajiwa kuipamba.
Farah amesema kwamba hivi sasa anajiandaa kwa ajili ya michuano ya Ulaya iliyopangwa kufanyika Agosti mwaka huu.
Farah alijitoa pia katika michuano ya Diamond League majuzi na sasa ameikosa ya Glasgow baada ya kulazwa hospitali kwa siku mbili akilalamika kwamba ana maumivu ya tumbo.
Hadi jana England ilikuwa inaongoza kwa kutwaa medali sita za dhahabu, saba za fedha na nne za shaba, ikifuatiwa na Australia wenye tano za dhahabu, tatu za fedha na saba za shaba.
Wenyeji Scotland nao hawapo vibaya, kwani hadi jana walikuwa wametwaa medali nne za dhahabu, tatu za fedha na tatu pia za shaba.
Afrka Kusini Ghana na Nigeria ndizo zilizochomoza kwa upande wa Afrika, ambapo Afrika Kusini ina mbili za shaba na Ghana wana moja moja.
Comments
Loading…