Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Kapteni George Mkuchika atakuwa mgeni rasmi wa mechi kati ya Stars na Uganda Cranes Jumamosi na kuwaongoza Watanzania ili kuishangilia timu hiyo.
Mechi hiyo ya hatua ya pili ya Taifa Stars baada ya kufanikiwa kuiondoa timu ya taifa ya Harambee Stars ya Kenya katika mashindano hayo yanayohusisha wachezaji wanaocheza ligi ya nyumbani, mashabiki wa soka wa Kanda ya Ziwa wameshauriwa kujitokeza kwa wingi ili waipe hamasa.
Akizunguza na Mwananchi jana, ofisa habari wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF), Florian Kaijage alisema kuwa wachezaji wote 20 walioteuliwa kuunda kikosi hicho wamesharipoti kambini akiwemo golikipa Ivo Mapunda ambaye amenza mazoezi jana pamoja na wenzake.
“Wachezaji karibu wote wameripoti kambini kwa maandalizi ya mechi dhidi ya Uganda itakayofanyika Mei 3 jijini Mwanza katika Uwanja wa CCM Kirumba,” alisema Kaijage na kusema ushindi wa nyumbani ni muhimu kabla ya kurudiana na Uganda mjini Kampala.
Kuhusu wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje, Kaijage alisema wanatarajia kujiunga na kambi hiyo lakini kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya kufuzu kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika na Kombe la Dunia mwaka 2010.
Wachezaji hao ni Meshack Abel, Haruna Moshi, Erasto Nyoni, Nizar Halfan na Danny Mrwanda ambao ambao hawashirika mechi dhidi ya Uganda.
Alisema taarifa walizo nazo Uganda inatarajia kuingia nchini kesho na itafikia katika hoteli ya New Mwanza na kwamba waamuzi wa mchezo huo wanatarajia kuwasili Ijumaa.
Katika hatua nyingine kipa wa timu ya Taifa Stars, Ivo Mapunda ameanza mazoezi jana na wenzake kujiandaa kwa mchezo wa mwishoni mwa wiki akisema atajitahidi kurejesha namba yake katika kikosi cha kwanza ingawa hayuko fiti kuivaa Uganda Cranes.
Mchezaji huyo pamoja na beki Shadrack Nsajigwa waliokuwa wamefungiwa na timu yao, Yanga kwa kipindi cha miezi sita kutokana na tuhuma za utovu wa nidhamu na adhabu yao ilimalizika juzi, waliitwa na kocha Marcio Maximo juzi kurekea Stars.
Akizungumza na Mwananchi jana baada ya mazoezi ya jana asubuhi kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es salaam, Ivo alisema anajisikia raha kurejea tena kwenye kikosi hicho na kikubwa kwake ni jinsi kocha wa timu hiyo Marcio Maximo alivyomwamini ingawa huyuko tayari kucheza mchezo ujao dhidi ya Uganda.
“Najisikia furaha sana, ni kipindi cha miezi sita sijafanya mazoezi ya uhakika, bali nilikuwa nafanya mazoezi kule uswahilini, kwa hiyo nahitaji muda kidogo wa kujiweka safi kwa ajili ya mikimikiki ya kukaa golini kwa ajili ya mchezo wenye upinzani.”
“Sijacheza mchezo wowote kwa kipindi chote hicho, hivyo siwezi kucheza mchezo wowote kwa sasa ukiwemo ujao dhidi ya Uganda kwa kuwa najiona kabisa kuwa siko fiti, ingawa kocha ndiye mwamuzi wa mwisho.”
“Sasa naangalia mbele katika klabu yangu ya Yanga ilipo ajira yangu na nitaendelea kuitumikia, sitarajii kwenda kwenye timu nyingine kwa sasa, bali nitaitumikia kwa moyo wangu wote na kujitahidi kuhakikisha nairudisha namba yangu, inagawa itakuwa kazi ngumu kwa kuwa nakwenda pale kama mgeni,” alisema.
Alisema mchezaji yeyote wa mpira wa miguu anaonyesha uwezo wake mazoezini na hilo yeye atalifanya kwa juhudi zake zote, hadi jana wachezaji wote walikuwa wameripoti kwenye kambi ya timu hiyo isipokuwa Shadrack Nsajigwa pekee ambaye ataripoti leo.
Comments
Loading…