Na Propaganda Basi Mtakua Na Viwanja Vyenu…
Niliwahi kwenda mara kadhaa pale Mo Simba Arena kule Bunju hapa jijini Dar Es Salaam sehemu ambayo ndio mapishi ya kikosi cha Simba hufanyika kujiandaa na mashindano kadha wa kadha ambayo wamekua wakishiriki.
Nikiri kwa kusema kuwa ni eneo zuri sana kwani hakuna msongamano mkubwa wa watu katika eneo lile jambo ambalo linafanya kuwe na Utulivu mzuri wa wachezaji pamoja na benchi la ufundi kuandaa Vyema mbinu zao kuelekea Mechi ambazo wanakua wanajiandaa kukabiliana nazo.
Miaka 2 Iliyopita nikiwa miongoni mwa waandishi ambao niliongozana na aliyekua Afisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba kipindi hicho akiwa Barbara Gonzalez pamoja na Msanifu Majengo tulitembelea Mo Simba Arena ambapo lengo kuu lilikua ni kukagua mipaka pamoja na kutazama eneo ambalo litatumika Kwa Ujenzi Wa uwanja wa Mo Simba Arena.
Wakati huo alisema kwamba mipango mikubwa ni kuhakikisha kuwa wanajenga majukwaa pamoja na miundombinu mingine ya uwanja na walikua wakae kikao na bodi ya wakurugenzi ili wampishe mkandarasi lakini mpaka sasa hakukufanyika kitu kipya.
Kuna wakati huwa naona kwamba hizi huwa ni siasa za mpira kwamba kuna uwanja tutajenga utakua hivi tutafanya hiki na hiki lakini hakuna lolote ambalo hutokea.
Niwapongeze sana JKT Tanzania pamoja na KMC kwa kuwa na viwanja vyao ambavyo wanavitumia Ligi Kuu wapo ambao watasema KMC ni uwanja wa Manispaa sawa hatukatai lakini kwanini vigogo Hawa wawili wanashindwa kujenga? Wanapata kiasi gani kutoka kwa wawekezaji wao? Ukiuliza huwa majibu ni yaleyale kwamba tutajenga.
Mkitaka kutuaminisha kuwa mko tayari Kwa ujenzi wa viwanja basi tutajua tu kwani hatutataka mambo ya kutambiana kuhusu jinsi utakavyoonekana waambie tu mashabiki na wanachama kwamba mipango yangu iko hivi mkandarasi ni huyu hapa na uwanja wangu utajengwa kwa namna hii.
Mimi naamini kuwa klabu hizi zimekosa mipango madhubuti ya muda mrefu inayolenga kujenga viwanja vyao. Badala yake zimekuwa zikitegemea matumizi ya viwanja vya umma kama Uwanja wa Taifa na vingine ambavyo huwa wanavitumia. Ukosefu wa mikakati ya uwekezaji yenye malengo ya kujenga miundombinu imara imesababisha kutokuwa na viwanja vyao hadi sasa.
Nimalizie tu kwa kusema kuwa ili klabu hizi zifanikiwe kumiliki viwanja vyao vya kisasa, zitahitaji kuwekeza katika mipango ya muda mrefu, kuboresha utawala, na kuvutia wadau wakubwa wa uwekezaji ambao watawezesha kufanikisha ndoto hiyo bila kusahau kuwepo kwa vikwazo Kutoka Kwa mashabiki kama ambavyo mara zote imekua ikizikumba klabu zetu hizi za Kariakoo.
Comments
Loading…