HATA makocha wanao tamaa wanapoona kipaji fulani cha mchezaji. Tamaa hiyo inawaletea madhara na wakati mwingine hujikuta kwenye presha kubwa. Hata hivyo mashabiki wa timu mbili, moja ikiwa huko Ulaya na nyingine ikiwa barani Afrika katika nchi ya Tanzania wamelazimika kuwapigia makofi wachezaji wao kama njia ya kuwahamasisha. Imani ya mashabiki imewafanya wawape heko Yanga ambaye ni bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Tanzania na Real Madrid, bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Hispania na Ligi ya Mabingwa.
Hata hivyo zipo mechi mbili zenye matokeo yanayofanana, tofauti ni idadi ya mabao yaliyofungwa katika michezo husika. Real Madrid imefungwa mabao 7, Yanga wamezabwa mabao manne katiika mechi mbili. Katika makala haya tunaangalia masuala muhimu yanayowakumba Yanga ambayo kwa namna fulani yanafanana na kule Real Madrid.
Maeneo matatu ya nguvu za mchezo
Yanga wamepigwa mabao 3-1 na timu ya Tabora United maarufu kama Nyuki wa Tabora. Aina ya uchezaji wa timu ya Tabora United sio wa kutisha kwa maana ya kimbinu na uwezo lakini wanacheza katika timu inayoshirikiana kwa kiwango cha juu. namna walivyofunga mabao yao yanaonesha wazi kuwa Yanga walikuwa wamepuuza mechi hiyo kuanzia namna kocha wao Miguel Gamondi alivyopanga kikosi chake.
Kimbinu Tabora United waliamini nguvu yao ya mchezo inatakiwa kupangwa maeneo matatu; eneo la kiungo cha kati ili kuwadhibiti wapishi wa mabao ya Yanga ama watengenezaji wa mashambulizi ya mabao. Kudhibiti eneo la Kati ni kuhakikisha Mudathir Yahya na Khalid Aucho hawaleti madhara langoni mwao. Njia zilizofungwa ni zile za kumfikishia mpira Mudathir na kumfanya arudi nyuma zaidi. Eneo la pili, ni kucheza tofauti na mtindo wa Yanga (kupishana).
Yanga wanapenda kupiga pasi nyingi na kusaka ushindi kwa madoido, lakini pia wanaweza kubadilika kwa kucheza ‘jihad’. Kwenye mchezo dhidi ya Tabora United walituliza mpira na kutaka kuwaelekeza wapinzani wao namna ya kucheza. Badala yake Tabora United walitumia eneo la pili la winga wa kushoto na kulia. Viungo wa Tabora United walipokuwa eneo la katikati ya uwanja wamepiga mipira mingi kuelekea pembeni kwa Yacouba Sogne, staa wa zamani wa Yanga ambaye aliifanya safu ya ulinzi wa kulia wa Yanga ionekane nyanya.
Kwa maana hiyo zilikuwa ‘counter attacks’ ambazo ziliwanyima nafasi Mudathir Yahya na Aucho kurudi haraka kusaidia ulinzi. Mabao yote yanaonesha jinsi eneo la kiungo la Yanga lilivyokuwa mbali kulinda safu yao. Tabora United kwa kasi hiyo walijikuta wamebaki na uhuru mwingi eneo la 18 na kuachia mashuti mawili muhimu yaliyozaa mabao. Yacouba Sogne alipika nafasi nyingi akitokea pembeni kushoto kuingia eneo la hatari. Mara kadhaa vwalipenyeza pasi na wenzake walishindwa kutumia. Kwa maana hiyo mfumo wa Gamondi ulivurugwa kwa kuwakimbiza viungo wake.
Utimamu wa miili
Wachezaji ni binadamu, sio mashine ambazo zinaweza kufanya kazi bila kupumzishwa. Upo wakati wachezaji wa kikosi cha kwanza wanachoka hivyo wanahitaji muda wa kumpuzika au kupunguziwa dakika za kucheza uwanjani ili kuwapa nafasi ya kurejesha nguvu za mwili.
Hata hivyo wachezaji wa kikosi cha kwanza cha Yanga hawapati nafasi ya kutosha kupumzika, hali kadhalika wale walioko benchi hawapewi muda wa kutosha kujiweka tayari na mechi. Baadhi ya matukio kiwnajani yanaonesha wachezaji wa Tabora United waliweza kuwazidi Yanga katika mpambano wa mabavu. Wengi wa wachezaji wa Yanga walijikuta wakianguka kila mara kuliko inavyotakiwa. Jawabu la haraka ni kwamba timu inahitaji msaada wa kuimarishwa utimamu wa mwili. Je wale wanaokaa benchi bila kupewa dakika za kuimarisha viwnago na utimamu wao kimwili watawezaje kuikoa Yanga katika nyakati ngumu? Waongezewe dakika za kucheza.
Yanga wanapenda Starehe
Ynaga walipofungwa na Azam FC 1-0 walicheza kwa starehe kubwa. Kila dakika uliwaona Yanga wanachezaji wanavyotaka, mbinu zao, uwezo wao na mikakati yao ilikuwa kuhakikisha wanawaelekeza Azam namna ya kucheza. Nao Azam kwa sababu walikuwa na hofu wakajikuta wanajilinda zaidi huku wakisahau Yanga walikuwa pungufu kiwanjani. Jambo hili limetokea tena kwa Tabora United kwa Yanga kuendeleza kucheza kwa starehe lakini walibadilikiwa kimbinu. Mbinu ya kupenda starehe ni pale ambapo timu inacheza kadiri inavyojisikia na kukuonesha yenyewe ndiyo mbabe na ana uhakika wa kunyakua pointi katika mchezo. Bahati mbaya starehe yao kwa Tabora United iliwakuta wakiwa hawana utundu wa kuwatetemesha hadi walipoambulia kichapo. Mechi hii itawarudisha kwenye meza ya mikakati.
Miguel Gamondi anamtamani Ancelotti
Matukio mawili yanayofanana kati ya makocha hao ni upangaji wa eneo la beki wa kulia. Kwa asili Dennis Nkane ni winga wa kulia ama kushoto. Hali kadhalika Lucas Vazquez ni winga wa kulia kwa asili. Nkane na Vazquez wamebadilishwa nafasi kutoka na sifa yao moja kuu; maarifa ama uwezo mkubwa wa kuwasoma wapinzani na kuwa na akili ya kushambulia. Hata hivyo linapofika suala la kujilinda au kufanya kazi kama beki halisi wa kulia wamepata changamoto. Mechi kadhaa Dennis Nkane amepangwa kama beki wa kulia badala ya nafasi iliyomtambulisha na kumpa ujiko Yanga, winga wa kulia.
Hata hivyo Dennis Nkane si mchezaji mbaya ingawa si beki mzuri wa kulia kama ilivyo kwa mwenzake wa Real Madrid Lucas Vazquez. Pale Real Madrid wametoka kuumizwa wiki hii katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwani wazee wenzao AC Milan walitumia udhaifu wa upande wa kulia wa Real Madrid kw akumpanga Rafael Leao ambaye alimtetemsha nahodha msaidizi Lucas Vazquez na kumfanya awe mhanga wa kipigo cha mabao matatu. Miguel Gamondi anakitamani kipaji cha Dennis Nkane. Anatamani kuona winga huyo anatumia maarifa hayo kuanzia nafasi ya beki kuelekea eneo la adui.
Mechi alizopangwa mara nyingi Nkane alikuwa akivuka mstari wa eneo la katikati ya dimba pembeni hucheza kama winga kwani kasi,chenga na maarifa huwafanya wapinzani warudi nyuma. Hali hiyo iko kwa Lucas Vazquez pia akivuka mstari huo anakuwa mchezaji hatari. Ni kama mawinga wa ziada kwenye mashambulizi sababu ni asili yao kushambulia (Offensive).
Hasara ya wachezaji kama Dennis Nkane na Lucas Vaszquez ni pale timu inaposhambuliwa; sio rahisi kucheza kwa umahiri kama walinzi (Defensive). Mfano Lucas Vazquez alikuwa mahiri kama beki wa kulia enzi za Zinedine Zidane akiwa kocha, lakini wa sasa anacheza zaidi kutegemea timu inaendeshwaje. Wapinzani wanayelenga maeneo dhaifu kwahiyo hilo nalo liliwapa mwanya Tabora United kufanya vitu vyao. Yacouba Sogne anao uzoefu na aliona namna eneo hilo linavyo mwanya.
Comments
Loading…