Manchester United wawapiga Liverpool
*Swansea wavuliwa ubingwa, Arsenal wavuka
Mikiki ya Kombe la Ligi England imenoga, baada ya mabingwa watetezi, Swansea kung’olewa na timu ya daraja la pili (Championship), Birmingham.
Mzunguko huu wa tatu uliwashika vijana wa kocha Michael Laudrup pabaya, kwani walipoteza mechi kwa mabao 3-1.
Katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa St. Andrew’s, nyumbani kwa Birmingham, mabao yote yalipatikana katika kipindi cha pili, yakifungwa na
Dan Burn kwa kichwa kabla ya Matt Green kuunganisha kwa mguu wa kulia majalo ya Chris Burke.
Tom Adeyemi aliwazamisha Swansea kwa bao la tatu na kumfanya kocha Lee Clark kuwa na furaha isiyo kifani na katika dakika za majeruhi mshambuliaji mpya wa Swansea, Wilfried Bony aliwapatia Swansea bao la kufuta machozi.
FARAJA KWA MANCHESTER UNITED
Katika mechi nyingine, Manchester United walijifariji wakicheza nyumbani Old Trafford walipofanikiwa kupata ushindi mwembamba dhidi ya mahasimu wao, Liverpool.
Bao la Javier Hernandez ‘Chicharito’ kutokana na kona ya Wayne Rooney lilitosha kuwavusha United na kufuta machozi ya kukandikwa mabao 4-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya England Jumapili iliyopita.
Katika kona hiyo, wachezaji wa timu zote mbili walikamiana kabla na wakati ikipigwa, baadhi wakishikana mashati.
Mpachika mabao wa Liverpool, Luis Suarez alirejea dimbani baada ya adhabu ya kukosa mechi 10 kwa kumng’ata Branislav Ivanovic wa Chelsea msimu uliopita.
Hata hivyo, uwapo wake na washambuliaji wenzake, Daniel Sturridge, Victor Moses na dakika za mwisho kinda Raheem Sterling hakukuweza kuwapatia bao, licha ya kubisha hodi langoni mwa Man U mara nyingi.
WASHIKA BUNDUKI WALENGA SHABAHA
Arsenal walifanikiwa kutinga hatua ya 16 bora baada ya kuachia uongozi wa bao 1-0 na kwenda sare hadi muda wa ziada, hivyo kuupata ushindi kwa njia ya penati dhidi ya West Bromwich Albion.
Wakati fulani Kocha Arsene Wenger aliyechezesha kikosi mchanganyiko ambacho si kile cha kwanza alionekana kama kulaumiwa na washabiki walioona kwamba walikuwa wakitolewa mashindanoni.
Bao la Arsenal la kuongoza liliwekwa kimiani na mchezaji Eisfeld dakika ya 61 na kusawazishwa na Berahino dakika 10 baadaye.
Penati ya kuamua mshindi iliwekwa kimiani na beki wa kushoto Mhispania, Nacho Monreal baada ya West Brom kukoseshwa yao na Morgan Amalfitano.
Wafungaji wengine kwa Arsenal walikuwa Chuba Akpom, Kriss Olsson na Nicklas Bendtner wakati chipukizi Mjerumani, Serge Gnabry aliyeanza kuzoeshwa kwenye ligi Jumapili iliyopita alikosa penati kwani iliokolewa na kipa Luke Daniels.
Wengine waliofunga kwa West Brom ni James Morrison, Markus Rosenberg na Steven Reid wakati Craig Dawson alikosa ya kwake.
MATOKEO MENGINE YA JUMLA
Katika mechi nyingine Jumanne hii, Newcastle walifanikiwa kuwafunga Leeds mabao 2-0 na Stoke wakawafunga Tranmere idadi hiyo hiyo ya mabao.
Katika mechi zilizochezwa Jumatatu hii, Tottenham Hotspur waliwaadhibu Aston Villa kwa mabao 4-0; Burnley wakawafunga Nottingham Forest 2 – 1 wakati Hull nao wakipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Huddersfield.
Leicester waliwafunga Derby 2 – 1 huku Manchester City wakiendeleza mapigo kwa kuwakandika Wigan mabao 5-0. Southampton walitoka kifua mbele kwa mabao 2 – 0 dhidi ya Bristol City huku Sunderland nao wakivuka awamu hii kwa kuwahsinda Peterborough kwa mabao 2-0.
Chelsea walifanikiwa kupata ushindi mgumu wa mabao 2-0 dhidi ya Swindon wakati Norwich waliibuka na ushindi wa kuchelewa wa 3-2 dhidi ya Watford.
West Ham walipata ushindi wa mabao 3 – 2 dhidi ya Cardiff wakati Fulham bila kutarajiwa waliwatoa nje ya mashindano Everton kwa mabao 2-1.
Comments
Loading…