Yanga imefanikiwa kutwaa kombe hilo kwa kuwafunga wapinzani wao wakubwa Simba kwa bao 1-0 katika muda wa nyongeza, bao lililowekwa kimiani na mshambuliaji wao Kenneth Asamoah kutoka Ghana.
Mshambuliaji huyo kipenzi cha wanajangwani alizima ndoto za mabingwa hao wa kihistoria kuweka rekodi ya kutwaa kombe hilo kwa mara ya saba alipofunga bao kwa kichwa akiunganisha krosi nzuri ya kiungo mchezeshaji Rashid Gumbo.
Gumbo, mchezaji mwenye kipaji cha pekee cha kumiliki mpira aliingia akitokea benchi katikati ya kipindi cha kwanza kuchukua nafasi ya kiungo mkabaji Juma Seif aliyeumia, aliambaambaa na mpira kwenye wingi ya kushoto akiwatoka wachezaji Mohamedi Banka na Saidi Cholo na baadaye kutoa krosi murua iliyounganishwa kiufundi na mshambuliaji huyo wa zamani wa Fc Jagodina ya Serbia.
Mara ya mwisho Yanga kutwaa kombe hilo ilikuwa ni mwaka 1999 huko Kampala Uganda ilipoifunga Sports Club Villa ya nchini humo kwa mabao 4-5 kwa njia ya penati, ambapo matokeo katika muda wa dakika 90 yalikuwa ni 0-0 na hivyo kulazimu kwenda muda wa nyongeza.
Kwa ushindi huo Yanga imeandika historia mpya ya mashindano hayo, kwani ni kombe lake la nne ikiwa imewahi kutwaa kombe hilo kwenye miaka ya 1975 huko Zanzibar, mwaka 1993 na 1999 huko Kampala Uganda na mwaka huu katika ardhi ya nyumbani.
Katika michuano hii ya mwaka huu Tanzania iliwakilishwa na timu tatu ambapo ni mabingwa watetezi Simba kwa maana ya msimu uliopita, washindi wa pili Yanga na kwa upande wa Zanzibar walikilishwa na timu ngeni kabisa katika mashindano hayo, timu ya Ocean View.
Katika michuano hiyo ya wiki mbili hakukuwa na kipya sana kutoka kwa timu zetu kubwa za Simba na Yanga kwa maana ya ubora wa kiwango cha uwanjani na wachambuzi wa masuala ya soka wanasema kwamba uenyeji na uzoefu wa timu hizo katika mashindano hayo kwa kiwango kikubwa vilichangia timu hizo kufika hatua ya fainali.
Timu pekee kutoka Tanzania ambayo ilionyesha kiwango bora ni Ocean View ya Zanzibar ingawa uchanga wake katika michuano hiyo uliifanya itolewe katika hatua ya makundi, lakini ilicheza soka la kifundi na kitimu tofauti na Simba na Yanga.
Katika michuano hiyo ambapo Yanga na Simba zote zilikuwa katika kituo cha Dar es salaam kutokana na utashi wa Baraza la Vyama vya Soka kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati(CECAFA) na Shirikisho la Soka nchini, TFF zikiamini kuwa kuziweka kituo hicho kungetengeneza faida kubwa ya mapato kutokana na ukweli kwamba mkoa huo maarufu nchini ndio wenye washabiki wengi wa soka wa Simba na Yanga na wenye vipato vya kuingia mpirani.
Katika kituo hiki cha Dar es salaam Simba ilipangwa kundi A ikiwa na timu za Vitalo ya Burundi, Ocean View ya Zanzibar na Etincelles ya Rwanda.Simba ndio ilikuwa ya kwanza katika kundi hili ambalo halikuwa gumu, ingawa ilipata wakati mgumu ilipocheza na Vitalo na Red Sea kwani haikuweza kupata bao hata moja.
Yanga ndio ilikuwa kundi la kifo, kundi B lililokuwa na timu za El Merreikh ya Sudan, Bunamwaya ya Uganda na Elmani ya Somalia. Merreikh ndio ilionekana kama timu tajiri kwa kuwa wachezaji wake wengi ghali, ilicheza soka la kuvutia na la ufundi wa hali ya juu, katika mchezo wake wa kwanza dhidi ya Yanga zilitoka sare ya mabao 2-2.
Bunamwaya iliundwa na wachezaji wengi chipukizi ilimaliza ikiwa ya tatu katika kundi hilo na kupata kucheza hatua ya robo fainali kama timu iliyoshindwa kwa taabu, “Best Loser” sambamba na Yanga vinara wa kundi hilo na Merreikh walioshika nafasi ya pili.
Elman timu kutoka Somalia kama kawaida yake ingawa angalau ilijitahidi katika mashindano ya mwaka huu, hasa katika mchezo wao dhidi ya Yanga ambapo iliwabidi mpaka dakika za lala salama kuweza kupata mabao, katika ushindi wake wa mabao 2-0 dhidi ya timu hiyo.
Kituo cha Morogoro kilikuwa na timu za St.George, Ulinzi ya Kenya na APR ya Rwanda ambayo ndio ilikuwa bingwa mtetezi wa mashindano hayo na Ports ya Djibout.Lilikuwa kundi gumu kwa maana timu zote hizo zilikuwa na ubora wa hali ya juu ukiachilia mbali Ports ambayo ndio ilikuwa kapo la magoli.Wachunguzi wa mambo wanaamini hili ndilo lilikuwa kundi lenye timu ngumu na St George ndiyo ilikuwa timu bora kwa maana ya soka la kiufundi.
Katika hatua ya robo fainali Simba iliifunga timu ngumu ya Bunamwaya kwa mabao 2-1,Yanga ikaifunga Red Sea kwa penati 4-3,El Merreikh ikiitoa Ulinzi Kenya kwa penati na St George ikaifunga timu ya Vitalo ya Burundi na kutinga hatua ya nusu fainali.
Mpaka zinaingia fainali Simba na Yanga zote hazikuonyesha kandanda la kuvutia zaidi ya kucheza kwa uwezo wa mchezaji mmoja mmoja na kwa shinikizo la mashabiki wao zaidi kuliko muunganiko wao kama timu.
Makocha wa timu hizi mbili, Sam Timbe wa Yanga na Mosses Bassena wa Simba hakuna hata mmoja kati yao aliyewahi kukiri kuwa timu zao zilicheza vizuri zaidi ya kufurahia matokeo na kusema kwamba wanayatumia mashindano haya katika kutengeneza timu zao kwa ajili ya michuano kimataifa kama vile klabu bingwa Afrika na kombe la shirikisho.
Ukiachilia mbali ukweli wa kwamba timu zote hazikupata muda mzuri wa maandalizi kutokana na kwamba ndio ligi ilikuwa imekwisha na wachezaji kuwa mapumzikoni, kuchelewa kupatikana kwa mdhamini wa kuandaa mashindano hayo, kuliathiri kwa namna moja au nyingine maandalizi ya timu hizi, lakini kuna kitu kimejificha ndani ya timu hizo.
Hakika timu hizi zinaundwa na wachezaji wengi wapya kila msimu kitu ambacho
Comments
Loading…