TAKRIBAN mwezi mmoja uliopita Mtanzania Hamisi Kondo alishinda mashindano ya kimataifa ya kuruka kamba huko Orland Marekani.
Bila kujua wala kujulikana, mwenzetu huyu ametupatia ujiko wa hali ya juu. Nani alimjua kabla ya ushindi huo, nani alijua kwamba alikuwa kwenye maandalizi ya mashindano hayo, nani alijua ushiriki wake, lakini licha ya yote hayo mwenzetu katubeba.
Tumekuwa tukihangaika sana na soka, haijatubeba mpaka sasa ambapo inakuwa kama homa ya vipindi; kuna nyakati inatia moyo na kuna nyakati inakatisha tamaa kutokana na wachezaji wetu kutoandaliwa kisoka tangu utotoni na kukosekana kwa uzalendo, mambo ambayo tulishawahi kuyajadili.
Riadha sasa hivi ipo kama haipo. Huwezi kujihakikishia kufanya kitu cha maana kwa wanariadha wetu wa taifa kukaa kambini kwa wiki chache kabla ya mashindano!
Enzi zao, kina Filbert Bayi walikuwa wakiishi maisha yao yote kama wanariadha jeshini. Walikuwa wakifanya mazoezi huko jeshini kuanzia Januari mosi mpaka Desemba 31, kuwepo au kusiwepo mashindano.
Aidha, kulikuwa na mashindano mengi ya riadha ya ndani kama michezo ya majeshi walikojaa wanariadha, mashindano ya kanda na kadhalika. Hapo hujazungumzia maandalizi ya wanariadha hao kwenye mashindano ya UMISSETA kwa shule za sekondari ambayo chimbuko la wanamichezo wake lilikuwa mashindano ya UMITASHUMTA ya shule za msingi.
Tanzania ilifanikiwa kwenye riadha si hivi hivi tu, bali kulikuwa na mipango iliyoratibiwa na WATU wenye weledi wa kupangilia mambo kwa kutumia sehemu ya ARDHI yetu kama viwanja vya kuwaandaa vijana kimichezo.
Viwanja hivyo ni kama vile vya Jangwani, Dar es Salaam na maeneo mengi ya wazi yaliyoachwa kwa madhumuni hayo, tukibebwa na SIASA SAFI iliyokuwa na kauli mbinu nyingi kama Michezo ni Afya, Michezo hudumisha urafiki, Michezo hutangaza nchi na kadhalika.
Kupitia kauli mbiu hizo, kushiriki michezo hakukuchukuliwa kuwa suala la matashi wala uamuzi binafsi, bali suala mojawapo la ujenzi wa taifa.
Haya yalikuwa matokeo ya UONGOZI BORA uliojihusisha na mambo mengi kama ukombozi wa Afrika, ujenzi kiuchumi wa taifa changa kupitia kilimo na viwanda lakini bila kuacha kushughulikia michezo.
Sisi tanzaniasports.com tunaona kwamba ipo haja ya kuufumua uongozi wa riadha wa Tanzania uliopo, kwani si tu unaonekana kukosa ubunifu bali pia unaona kuwepo uongozini imekuwa kama sehemu ya maisha ya viongozi hao.
Hii ni kwa sababu katika hali ya kawaida, baada ya kushindwa mara kadhaa kufikia malengo, wangeondoka kuwaacha wengine wajaribu ubunifu wao. Lakini mtu anafeli na kuendelea kuwepo madarakani, anakuwepo kufanya nini kama si kuchukulia kwamba nafasi aliyo nayo ya uongozi ni yeye na yeye ni nafasi ya uongozi aliyonayo?
Kwa upande mwingine, tunaishauri serikali kuimarisha UMITASHUMTA , UMISSETA na ajira za wanamichezo majeshini. Ni vizuri kurudisha au kuimarisha vitengo vya michezo mbalimbali majeshini. Hilo la majeshi, yaachiwe majeshi yenyewe kuchimbua vipaji mbalimbali vya michezo toka Tanzania nzima na hii ni kwa michezo yote; ya timu kama mpira wa wavu, mpira wa kikapu, pete, netiboli, soka na kadhalika.
Kadhalika, iangaliwe michezo ya mtu mmoja mmoja kama mbio za urefu tofauti, kuruka kamba, kuruka juu na chini, kuruka kwa upondo, kuinua vitu vizito, kurusha tufe, kurusha kisahani, kurusha mkuki, kutunisha misuli, kuogelea na kadhalika.
Tukishajizatiti kwenye michezo hiyo, serikali ianzishe mchakato wa kutengeneza chama kimoja au vyama vichache huru kushughulikia michezo ya mtu mmoja mmoja isiyo na vyama huku chama cha riadha kikibaki kushughulikia wafukuza upepo tu. Yaani kuruka kamba, kuruka juu na chini, kuruka kwa upondo, kuinua vitu vizito, kurusha tufe, kurusha kisahani, kurusha mkuki, kutunisha misuli na kadhalika iwe na timu moja ya viongozi wake tofauti na wale wa riadha, kupigania mafanikio ya taifa kupitia michezo hiyo kimataifa.
Tunaamini kwa njia hiyo, tunaweza kutoka kimichezo kwani chama hicho kitashughulikia kuanzia kutafuta wenye vipaji vya michezo hiyo, kuwaimarisha na kuwaanda kimashindano na hao ndio wanaweza kutuletea medali kadhaa.
Kwa mfumo wa sasa, wanamichezo hao wako kama watoto yatima. Mtunisha misuli wetu maarufu David Nyombo Mkobi anajitahidi kufanya mambo mengi ya kimataifa ya kuitangaza nchi lakini hakuna mamlaka yoyote ya kitaifa inayoshughulika naye na hivyo hakuna mkakati wowote wa kuwapata kina David Nyombo wengine kwa kukosa uongozi wa michezo ya mtu mmoja mmoja.
Turudishe ya zamani yaliyotuletea mafanikio kimichezo na tubuni mikakati mipya itakayotuinua kimichezo kama huu tulioshauri hapa. Mungu ibariki Tanzania.