Imetimia miaka 20 tangu uzinduzi wa Ligi Kuu ya England, hivyo ni wakati mwafaka kusherehekea hatua hiyo kubwa iliyofikiwa kwa Tuzo za Misimu 20.
Kwa kuzingatia miongo hiyo miwili ya ligi kubwa zaidi nchini England, Uongozi wa Ligi Kuu umewaalika mashabiki kuchagua Goli Bora, Mechi Bora, Uokoaji Bora na Ushangiliaji Bora, wakati jopo la wadau wa soka na waandishi wa habari watachagua Mchezaji Bora, Kocha Bora, Timu Bora, Msimu Bora na Nukuu ya Kukumbukwa Zaidi.
Tuzo itakayokuwa na mvuto zaidi katika kuwaniwa ni ile ya Mchezaji Bora. Wateule watakaowania tuzo hiyo ni Dennis Bergkamp, Eric Cantona, Ryan Giggs, Thierry Henry, Roy Keane, Cristiano Ronaldo, Paul Scholes, Alan Shearer, Patrick Vieira na Gianfranco Zola.
Walioorodheshwa kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora ni 10 tu, huku pakionekana wazi kwamba kuna wanasoka mashuhuri walioachwa. Kwa mfano, Wayne Rooney wa Manchester United na David Beckham aliyewahi kuchezea pia Mashetani Wekundu hao wameshindwa kuingia kwenye mchujo huo.
Ama kwa Chelsea, wapo wawili – Didier Drogba na Frank Lampard, akiwa kiungo pekee aliyefunga magoli 150 katika Ligi Kuu hii. Nahodha wa Liverpool, Steven Gerrard naye pia yupo nje.
Mfaransa Cantona ameteuliwa kuwania tuzo kwenye makundi matano, yakiwa mengi kuliko ilivyo kwa mchezaji mwingine yeyote.
Ukiacha tuzo ya Mchezaji Bora anayowania, Cantona aliyefanikisha timu yake kunyakua kombe mara nne anawania tuzo ya Mfungaji Bora, Nukuu ya Kukumbukwa Zaidi, Ushangiliaji Bora wa Goli na Mshambuliaji Bora. Mshambuliaji wa zamani wa Blackburn na Newcastle, Alan Shearer ameteuliwa kuwania tuzo kwenye makundi manne, wakati washambuliaji wa zamani wa Arsenal, Dennis Bergkamp na Thierry Henry wana makundi matatu kila mmoja.
Matt Le Tissier ndiye mchezaji pekee aliyeteuliwa kuwania tuzo mara mbili kwenye kundi la ‘Goli Bora’.
Kocha wa Manchester United, Sir Alex Ferguson anaelekea kukubalika zaidi kwenye kundi la Kocha Bora, ambapo Mskoti huyo anapambanishwa na
Arsene Wenger, Jose Mourinho, Harry Redknapp na David Moyes.
Comments
Loading…