in , , ,

Mfumo wa Man United katika miguu ya Amad Diallo

Kama kuna kocha ambaye halali usingizi kipinid hiki cha msimu wa sikukuu kwenye Ligi ya England basi Pep Guardiola. Kwa mara ya pili Guardiola anakubali kipigo kutoka kwa kocha kijana Ruben Amorim. Manchester City wamekubali kipigo cha mabao 2-1 katika mfululizo wa Ligi Kuu England. Ni kipigo ambacho kinaendeleza hali mbaya ya bingwa mtetezi wa EPL ambaye anashikilia nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi hiyo. Uchezaji wa timu,ari,shauku ya ushindi, na kazi ngumu ya kulinda mafanikio ni miongoni mwa mambo yanaokiadhibu kikosi cha Man City. Je nini hasa kilichotokea katika mchezo wa watani wa jadi Man City na Man United?

Mawinga asilia bila ushindi

Pep Guardiola amebahatika kurundikiwa wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu, amesajili Savinho  kama mchezaji wa kuchukua nafasi ya Riyaz Mahrez, lakini bado hajaonesha makeke yake. Katika kikosi cha Man City kila unapotazama majina na aina ya uchezaji ni lazima uogope. Katika mfumo wa wapishi watatu; kulia, kushoto na nyuma ya mshambuliaji ni dhahiri Erlin Haaland ni mshambuliaji mwenye wapishi wengi lakini matokeo yamegoma kuwa upande wao. 

Katika mfumo wa 3-1-3-2-1, Man City inakuwa na mawinga wawili na kiungo mchezeshaji mmoja huku Haaland akisubiri malisho mazuri toka kwa viungo wake lakini mambo yalikuwa magumu. Kwanini? Njia ya kwanza ni kuwanyima nafasi wapishi wa Man City. Katika kiungo cha Man United aliwapanga Ugarte,Mainoo na Fernandez kuhakikisha wanaziba mianya inayoleta mipira kwa Phil Foden kutoka kwa Bernado Silva. Lakini pia kuziba mianya inayokuja kwa Foden. Upande wa kulia na kushoto ndiko kulikuwa na uhai, lakini hawakuweza kuliona lango. 

Viwango duni, makosa mengi

Bao la kwanza la Man United lilitokana na kiwango duni cha kuzuia katika safu ya ulinzi. Mpira mrefu uliopigwa kutoka eneo la ulinzi la Man United na kwenda moja kwa moja Amad Diallo ambaye aliingia katika eneo la hatari na kabla hajafanyiwa madhambi na mwamuzi kuamuru ipigwe penati. Baada ya bao hilo Man United walionekana kuanza kuamsha ari lakini wangali wenye woga kwenye ulinzi. 

Hata hivyo katika mfumo wa mabeki watatu wa ulinzi, nahodha Kyler Walker alishindwa kuendana na kasi ya mpira mrefu uliopigwa toka langoni mwa MAN United na kutua mguuni mwa Amad Diallo kabla hajamzidi maarifa golikipa Edersson na kupachika bao la ushindi. Uchezaji wa Man City si rahisi kuruhusu mabao ya namna hiyo. Kiwango duni cha ulinzi na kuzuia hatari kimeiadhibu timu hiyo. Kutokana na kujaza viungo eneo la katikati, Man United waliona suluhisho ni kupiga mpira mrefu uliovuka eneo hilo na kutua kwneye safu ya ushambuliaji hivyo kuyumbisha mabeki wa Man City. Uchezaji wa kasi ndiyo uliowaathiri na kujikuta wakishindwa kumdhibiti Amad Diallo.

Mfumo unakwenda kwa Amad Diallo

Ruben Amorim anaonekana kuunda timu yake kupitia kinda huyu. Tangu alipochukua timu hiyo amemfanya chipukizi huyu kuwa mchezaji hatari na mwenye kasi kuliko wote dimbani. Amad Diallo ndiye anayeanzisha mashambulizi hatari. Ni winga ambaye anafanya uamuzi mgumu mara nyingi kuingia eneo la hatari akitokea upande wa winga wa kulia. 

Mara kadhaa amepangwa kama winga wa kushoto na wakati mwingine kama beki wa kulia mwenye jukumu la kucheza kama nambari saba. Siri ya ushindi wa mechi au namna mpango wa mchezo wa mechi husika anaofanya kocha Ruben Amorim anamtegemea Amad Diallo kama silaha yake ya kwanza. Kinda huyo ndiye aliyewafanya Man City waonekane wameshuka viwango katika kulinda lango lao. Ni aina ya mawinga ambaye anaweza kupangwa upande wowote na kumpa matokeo kocha wake.

Mfumo hauna mwenye namba kwenye ulinzi

Katika mechi dhidi ya Liverpool, kocha RubenAmorim alifanya uamuzi mgumu kwa kubadilisha safu yake ya ulinzi na kuwaingiza wengine wapya. Katika mchezo wa Man City pia safu ya ulinzi ilikuwa na wengine wapya walioingia kipindi cha pili. Mabadiliko ya mwalimu kumtoa Mazroui yalikuwa ya kustaajabisha lakini ghafla timu ilitawala mchezo dhidi ya wapiga pasi nyingi Man City. Katika mfumo anaotumia wa mabeki watatu au wanne, inaonekana hakuna mwenye uhakika wa kubaki kikosi cha kwanza kwa muda mrefu. Man United hubadilika kimfumo kila wachezaji wanapobadilishwa iwe mabeki,viungo na washambuliaji.

Nini kinachowasibu Man City?

Kwanza wanapambana na maadui watatu; kupandisha viwango vyao, kupigania ubingwa wao na kutumikia mfumo wa Pep Guardiola liwake au lisiwake jua. Katika kupigania ubingwa wao maana yake wameelemewa na mzigo wa mafanikio na ambao unawaathiri mabingwa wote katika msimu wa pili toka wachukue ubingwa. 

Timu inapochukua ubingwa inakuwa imetumia nguvu nyingi na maarifa, kwahiyo inapoingia msimu mpya lazima ikabiliwe na kibarua kigumu cha kubaki katika kiwnago kilekile kilichowapa ubingwa. Man City wanaweza kurejea kwenye hali zao lakini bado wana changamoto ya kushindana na timu azinazozidi kujiimarisha. Kutumikia mfumo ina maana Pep Guardiola hawezi kubadilika bali ataendelea kutumia mfumo uleule na kuhakikisha anairudisha timu kwenye kiwnago chake cha msimu uliopita.

Itakuwaje Amad akukamiwa?

Makocha wanawatzama Man United kwa makini na kuichambua kimbinu na maarifa binafsi. Ni dhahiri kuwa makocha wanaitazama timu hiyo katika mabadiliko kwani imekuwa ikiimarika siku hadi siku bila kutegemea mchezaji mmoja. Hata hivyo silaha kubwa ya kocha Ruben Amorim ni Amad Diallo, itakuwaje siku akikamiwa na kushindwa kufurukuta? 

Ni dhahiri timu hiyo itakuwa kwenye wakati mgumu, lakini kuna namna nyingine imeanza kuonekana. Winga Antony anaonekana kuwa mchezaji mpya katika kikosi cha Man United. Katika mchezo dhidi ya Man City aliingizwa kipindi cha pili na kwenda kucheza upande wa kulia (kama beki wa kulia mwenye jukumu la kushambuliaji). Hii ina maana Antony anakuwa mchezaji mwingine anayweza kuchukua jukumu la Amad Diallo lakini swali linabaki anaweza kuwa na kasi ileile ya mwenzake? Hilo linahitaji muda kujibiwa.

Kwa ujumla Man United inaimarika lakini safari yao ni ndefu hadi kuwa bora na kuwafikia wapinzani wao Man City. 

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Adhabu ya Refa imewapa ushindi Simba

Tanzania Sports

Navutiwa Na Ligi Kuu Ya NBC Msimu Huu