in , , ,

Mfahamu Zidane wa Tanzania

MSIMU wa Ligi Kuu 2024/2025 umebakiza miezi michache kukamilishwa huku kukiwa na matukio kadhaa muhimu ambayo yatakumbukwa zaidi. Miongoni mwa matukio hayo ni kuibuka kwa kipaji cha mchezaji mwenye jina la Zidane. Nakumbuka mwanzoni wakati anatangazwa kusajiliwa na klabu ya Azam wengi walijiuliza ikiwa hilo ndilo jina lake. 

Lakini kimahesabu unaona bayana kuwa Zidane wa Tanzania alipata jina hilo kutoka kwa Zidane wa Ufaransa ambaye ana asili ya Algeria na mtu maarufu sana duniani kutokana na kuweka rekodi ya kisoka ikiwemo kuweka rekodi ya kufunga mabao mawili katika mchezo wa fainali ya Kombela dunia mwaka 1998 pamoja na kutwaa mataji matatu mfululizo ya UEFA akiwa kocha wa Real Madrid kuanzia mwaka 2016-2018.

Jina la Zidane wa Tanzania lilivuma zaidi kwenye mchezo wa Ligi kati ya Azam na Simba akiwa nyota aliyeingia kipindi cha pili kupachika bao la kusawazisha kwa Azam hivyo kuwanyima pointi 3 muhimu vigogo wa Msimbazi. Zilivuma habari nyingi kuhusiana na nyota huyo na baadhi ikaonekana kama vile wanaanza kumfahamu akiwa klabuni hapo.

Zidane wa Tanzania ni nani?

Jina lake kamili ni Zidane Sereri. Ni mchezaji mwenye umri wa miaka 19. Ni mzaliwa wa wilaya ya kondoa mkoani Dodoma.

Ni mshambuliaji chupikizi wa mabwanyenye wa Chamazi, Azam Fc kwa mkataba wa miaka mitano Nyota huyo alianza kucheza ligi Kuu Tanzania katika msimu wake wa kwanza 2023/2024 akiwa mchezaji wa klabu ya Dodoma Jiji ya mkoani Dodoma. Zidane alisajiliwa kwenye dirisha dogo la usajili akiwa na kibarua kigumu kugombania namba na mastaa kama vile JHonier Blanco, Iddy Nado, na wengineo. Washindani wake klabuni baadhi wanatokea nchini Colombia. Nyota huyu alizaliwa huko visiwani Zanzibar na mmoja wa chezaji wanaong’ara katika kikosi cha Zanzibar Heroes.

Safari yake ya mpira ilianzaje

Taarifa kuhusu mchezjai huyu zinaonesha kuwa cheche zake zilimkosha kocha wa Dodoma Jiji Melis Medo kiasi cha kumpa nafasi kwenye kikosi cha kwanza. Katika kikosi cha kwanza alicheza pamoja na mkongwe Hassan Mwaterema na Seif Karihe. Safari yake ya kucheza soka ilianzia kwenye mashindano ya michezo ya Shule za Msingi UMITASHUMTA na Sekondari maarufu kama UMISETA. Baada ya kuonesha cheche kwenye mashindano ya hayo ya shule, alichukuliwa na Mwenyekiti wa chama cha soka mkoa wa Dodoma (DOREFA) Aden Mohammed na kumpeleka Makole Academy ikifundishwa na Omary Omaroh. Kisha akajiunga na Dodoma Jiji kwenye kikosi chao cha vijana. Kocha Masoud Djuma raia wa Burundi ndiye alimpandisha timu ya wakubwa kabla ya Melis Medo kumpa nafasi zaidi. Mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu ulikuwa dhidi ya Coastal Union ya Tanga.

Bao la dakika mbili

Moja ya sifa kubwa anayopewa ni jinsi alivyowatungua Simba. Nyota huyo alifunga bao la kusawazisha kwa klabu yake zikiwa zimebaki dakika mbili kumalizika kwa mchezo huo. Aliwalamba chenga beki na nahodha wa Simba, Mohamed Hussein na golikipa wake Mousa Camara. Bao la Zidane lilimaanisha mchezo wao dhidi ya Simba ulimalizika kwa sare 2-2 hivyo kugawana pointi.

Beki anayemhofia

Nyota huyo wa Azam amepata kukiri kuwa kati ya mabeki wanaomsumbua katika Ligi Kuu Tanzania ni nahodha msaidizi wa klabu ya Yanga, Dickson Job. “Huwezi kuona Job anaadhibiwa na marefa, hapati kadi sababu anacheza kwa maarifa makubwa. Hapati kadi za hovyo maana ni mchezaji anayekuja kwa akili sana, anafanya kazi yake kiakili mno. Ni fundi,”

Uzito wa jina lake

Katika historia ya soka baadhi ya watoto wa wachezaji wamegomea kutumia majina ya baba zao ambao walikuwa mastaa katika mchezo wa soka. Miongoni mwao ni watoto wa David Beckham, Marcelo, Zineine Zidane na wengineo. Watoto wa Zinedine Zidane walishauriwa kutotumia jina la Zidane kwa hofu ya kuelemewa na presha kutoka kwa wadau. Kwamba wengi waliamini mtoto wa Zidane angekuwa staa kama baba yake, lakini ajabu ni kwamba watoto wake walitumia majina tofauti. Mfano mtoto wa Marcelo anatumia jina la Enzo, sawa na watoto wa Zidane wenye majina tofauti. Kwahiyo ilitarajiwa kuwa kijana huyu wa Kitanzania angeliepuka uzito wa jina alilopewa na wazazi wake la Zidane, badala yake angeweka Sereri mgongoni. Hata hivyo nyota huyo ametuliza kichwa chake, anaendelea na kazi yake vyema.

Je Zidane Sereri ni mchezaji wa aina gani?

Huyu ni winga mzuri sana na anaweza pia kucheza nafasi ya mshambuliaji. Kwa uchezaji wake ni winga wa kulia au kushoto, na matumizi ya kocha yakiongezeka basi anaweza kupangwa nambari 9 kisha akaitumikia vizuri tu. Ni aina ya wachezaji wenye kasi, stamina na maarifa. Bao lake dhidi ya Simba lilionesha jinsi anavyoweza kukabiliana na matumizi ya nguvu katikati ya shinikizo la mabeki wa timu pinzani.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

14 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

EPL, Liverpool, kuhusu kipaji cha Federico Chiesa

Tanzania Sports

Rekodi ya kipekee toka kwa Lewis-Skelly