Wingu la shaka na wasiwasi limetanda Nou Camp kuhusu hatima ya mchezaji nyota wa Barcelona, Lionel Messi.
Mazungumzo kuhusu mkataba wake mpya yanasuasua na ile nadharia kwamba Messi hatakaa aondoke Barca inaelekea kufutika kidogo kidogo, wakuu wa hapo nao wakijiandaa kisaikolojia.
Mchezaji huyu aliyetwaa mara nne tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia – Ballon d’Or amepata kusema kwamba anataka kujipiga kitanzi hapo, lakini kwenye mazungumzo ya mkataba wenyewe anaonekana kudai malipo makubwa kupita kiasi.
Kiwango cha Messi kimekuwa kikishuka kadiri muda unavyokwenda, huku akikumbwa pia na majeraha na kujirudia kutapika uwanjani, na sasa kuna wanaouliza kwani bila yeye Barcelona haitakuwepo kama ilivyokuwapo kabla yake?
Aliongeza mkataba wake kwa mara ya mwisho mwaka 2012 na sasa anataka nyongeza ya mshahara na marupurupu iwafunike kwa mbali sana wachezaji wenzake na kudhibiti umiliki wa kampuni inayosimamia haki zake.
Inaelezwa kwamba kinachogomba sasa ni Euro milioni 9, ambapo Messi anazitaka kwenye kitita chake wakati klabu inataka zisiwepo, hivyo mjadala umekuwa ukizungukia hapo kwa muda sasa.
“Itakuwa ngumu sana kuzileta pande mbili hizo pamoja katika mvutano wa namna hii kuhusu kiasi kikubwa hivyo cha fedha,” mmoja wa wadau wa karibu anasema na kuongeza kwamba jinamizi la mkataba wa Neymar linazungukia hatima ya Messi klabuni hapo.
Inaelezwa kwamba kiwango cha fedha za fidia kilichotolewa kwa Santos ambayo ni klabu ya zamani ya Neymar kiliwaudhi sana watu walio kwenye kambi ya Messi. Agosti mwaka jana, Rais Sandro Rosell (ambaye ameshajiuzulu sasa) alimuahidi babaye Messi ambaye pia ni wakala wake kwamba wangewapatia mkataba mnono, lakini inaelekea haupatikani.
Rosell alilazimika kujiuzulu kutokana na makandokando ya mkataba wa Neymar, ambapo pia familia ya kinda huyu wa Brazil anayekuja juu ililipwa mamilioni ya Euro. Neymar ameanza kuchukuliwa kama mtu anayeweza barabara kuziba pengo la Messi.
Nafasi ya Rosell imechukuliwa na Josep Maria Bartomeu ambaye aliwasilisha ofa ya mkataba kwa Messi ambayo alishituka na kuona ni ndogo mno, isiyo na hadhi yake. Barca wanataka kuwa na aina ya hisa kutokana na malipo ya kampuni mbalimbali ambazo Messi anavaa vifaa vyake au matangazo yanayotumia jina lake.
Wakati hayo yakiendelea, matajiri wa klabu nyingine wanafuatilia kwa karibu, huku kukiwa na habari kwamba Manchester City wapo tayari kutoa Euro milioni 200 kumnasa Messi majira ya kiangazi lakini pia Paris Saint-Germain wamejisogeza kufikiria dau la kutoa kumpata Messi mwenye umri wa miaka 26.
Comments
Loading…