Mchezaji wa Barcelona na Timu ya Taifa ya Argentina, Lionel Messi ametajwa kuwa mchezaji bora wa Ulaya.
Messi ameibuka katika nafasi hiyo baada ya kumzidi mchezaji bora wa dunia anayemaliza muda wake, Cristiano Ronaldo wa Real Madrid na Ureno na Luis Suarez ambaye Messi alishirikiana naye vyema Barcelona msimu uliopita. Suarez ni mshambuliaji wa kimataifa wa Uruguay.
Kura ya kutafuta mchezaji bora wa Ulaya iliendeshwa mubashara na wanahabari Alhamisi hii ikijumuisha nchi zilizo katika Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa). Messi amepata kuwa mchezaji bora wa dunia mara nne, ambapo yeye na Ronaldo wanafungana kwa idadi ya mabao 77 katika UCL.
Messi alifunga mabao 58 na kusaidia mengine 31 katika kuwawezesha Barca kutwaa ubingwa wa La Liga, Kombe la Mfalme (Copa del Rey) na Ubingwa wa Ulaya. Ronaldo na Real Madrid walipata kigugumizi msimu uliopita na klabu wakamfukuza kocha Carlo Ancelotti na kumwajiri Rafa Benitez aliyeanza kwa sare na timu iliyopanda daraja msimu huu.
Suarez ndiye alifunga bao muhimu katika ushindi wao wa 3-1 dhidi ya Juventus kwenye fainali ya UCL na alifanikiwa kufika kwenye tatu bora licha ya kwamba alianza kucheza ligi akiwa amechelewa – Oktoba – kutokana na adhabu ya kufungiwa aliyopewa baada ya kumng’ata Giorgio Chiellini katika mechi ya Kombe la Dunia baina ya Uruguay na Italia mwaka jana.
Messi ndiye mshindi wa kwanza kutwaa tuzo hii mara mbili, baada ya kuwa ameitwaa ilipozinduliwa msimu wa 2010/11. Ronaldo ndiye aliyeitwaa msimu uliopita kabla ya kusonga mbele kutwaa ile ya mwanasoka bora duniani.
Comments
Loading…