NI miaka 43 sasa tangu Mchezo wa Mpira wa Wavu (Volleyball) uingie nchini Tanzania, sambamba na usajili wa chama chake kinachojulikana kama Tanzania Volleyball Association (TAVA).
Mchezo huo wa wavu, pamoja kuwa na umri mkubwa umekuwa na mdororo na kutofahamika kwa wengi, licha ya kwamba mwaka 2000 uliwahi kuwa na wadhamini waliosadia kuunyanyua, wakiwamo kampuni ya vinywaji baridi ya Bonite, KLM,TIPPER na Yellow Pages.
Sababu nyingi zinazotajwa kuhusu mdodoro huo ni kufutwa kwa michezo katika shule za msingi kulikofanywa na serikali mwaka 2001, hali iliyosababisha hata wale waliokuwa wanaupenda kukataa tamaa.
Miaka saba baadaye (2008) michezo iliporudishwa tena shuleni mpira wa wavu nao ulipata nafasi yake lakini mwonekano wake haukuwa mzuri kwani katika kipindi hicho cha miaka saba hapakuwa na juhudi zozote za kuuendeleza kwa maana ya kucheza na kujifunza hali iliyosababisha mchezo huo ku potea masikioni na machoni mwa watu.
Kutokana na hali hiyo,juhudi za kuurudisha tena mchezo wa wavu zinaonekana kusuasua kwa kutokuwa na mwitikio, si tu miongoni mwa wachezaji, wadau na wafadhili, bali pia kwa viongozi wa chama hicho ambao wanaona kama serikali imewatenga kwa kutotilia nguvu katika kuinua mchezo huo tofauti na inavyofanya katika michezo mingine hususan soka.
TAVA kupitia kwa Katibu wake, Alen Alex wamesema kuwa kudororo kwa mchezo huo kunatokana na vijana kutopata mafunzo stahiki ya mchezo huo, hasa ukitilia maanani kwamba mpira wa wavu hauwezi kuchezwa kwa mtu ambaye hajafundishwa.
“Unajua mpira wa wavu si miongoni mwa michezo ambayo unaweza kucheza kwa kuangalia kama ilivyo kwa soka, mchezo ambapo unawakusanya watoto na kuwapa mpira na kuanza kuucheza,” alibainisha Alex.
Aidha wadau mbalimbali wa mchezo huo wa mpira sababu ya mchezo huo kuwa katika mdororo ni viongozi kutokuwa na hisia,na hamasa kwa vijana wanaohitaji kucheza pamoja na kukosekana kwa mikakati na mipango madhubuti ya chama kwa kusaka wachezaji nje ya Dar es Salaam.
Wadau hao pia wamedai sababu nyingine ni kasumba ya viongozi wa mchezo huo kuona na kuamini ya kwamba Dar es Salaam tu ndipo wanapoweza kupatikana wachezaji bora, wakati ukweli ni kwamba wachezaji wazuri wanaweza kupatikana pia mikoani.
Mchezo huo pia umekuwa na changamoto ambazo zinaufanya udorore kama vile ukosefu wa vifaa na viwanja vya mchezo huo, waamuzi, wakufunzi na wadhamini.
Aidha wadau wa mchezo huo wameitaka Serikali kupunguza au kuondoa kabisa kodi kwa vifaa vya mchezo huo, kusimamia sera ya kuwapo sehemu za wazi kwa ajili ya watoto kucheza na kujifundisha, lakini pia wazazi wawape nafasi watoto wao kujifunza na kuwa nao katika mazoezi.
Vyombo vya habari na wanahabari wametakiwa kutoegemea upande mmoja wanaporipoti taarifa zinazohusu michezo na burudani na badala yake watupie jicho pia katika kuziandika habari za mchezo wa mpira wa Wavu nchini.
Kwa upande wake, Serikali kupitia Mkurugenzi wa Michezo, Wizara ya Vijana, Habari, Utamaduni na Michezo, Leonard Thadeo imekitaka Chama cha Mpira wa Wavu Tanzania kupanga mikakati madhubuti na kuweka mipango endelevu ya kuutangaza mchezo huo ili uchezwe na watu wengi.
“Ni jukumu la TAVA kupanga na kuandaa mashindano ya mara kwa mara ili watu wahamasike kucheza mpira wa wavu na kuupenda ili utoke katika hali ya mdororo,” alisema.
Comments
Loading…