Na Phillip Nkini
UMILIKI wa jezi za timu ya Taifa Stars umezua balaa kwa baadhi ya wachezaji wa timu hiyo kujikuta wakikatwa fedha zao za posho kwa madai ya kufidia jezi ambazo ama walibadilishana na wenzao wa Cameroon au kupoteza.
Kwa upande wake, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linasema: ”Jezi si mali ya wachezaji.”
Kampuni ya Bia ya Serengeti Breweries na Benki ya NMB, wadhamini wa Stars wamekuwa wakitoa vifaa kwa wachezaji wa timu hiyo kuanzia vile vya mazoezi hadi vya mechi mbalimbali ambazo timu hiyo imekuwa ikicheza.
Lakini, pamoja na hali hiyo kumezuka tatizo kwa baadhi yao (wachezaji) na uongozi wa timu hiyo kukosana baada ya baadhi yao kubadilishana jezi majuzi na wachezaji wa Cameroon, Indomitable Lions, jambo ambalo limewazulia mambo.
Mchezaji mmoja kinda wa timu hiyo (jina tunalo) alishindwa kumpa Geremi Njitap wa Cameroon jezi yake kwenye mchezo kati ya Stars na Cameroon mjini Yaounde baada ya mchezaji huyo kutaka wabadilishane.
Kinda huyo aliiambia Mwananchi kuwa alihofia kuja kurejea nchini na kudaiwa jezi.
Lakini, beki wa timu hiyo alibadilishana jezi na mshambuliaji wa Cameroon, Samuel Eto’o Fils baada ya Mcameroon huyo kumfuata mwenyewe na kumtaka afanye hivyo.
Hata hivyo, pamoja na wachezaji hao kudaiwa jezi hizo Ofisa Habari wa TFF, Florian Kaijage aliithibithishia Mwananchi kuwa jezi si mali ya wachezaji, bali ni mali ya shirikisho hilo na mchezaji atakapoipoteza, basi utaratibu wa malipo utafanywa.
”Jezi sio mali ya wachezaji ni mali ya Shirikisho la Soka, kila mchezaji anapewa jezi kwa kufuata utaratibu maalum ukipewa lazima urudishe usiporudisha unaandaliwa utaratibu wa kulipia.”
“Sisi bado tupo nyuma sana hatujafika huko walipo hao akina Senegal au Cameroon kuwa na wadhamini wakubwa, kiasi kwamba mchezaji mmoja kuwa na jezi zaidi ya kumi. Hapa kwetu, tunaweza kutumia jezi moja kwenye mechi mbili wenzetu kila mechi na jezi yake.
”Ukiangalia mchezaji kama Eto’o anandaliwa jezi zaidi ya 50 na Kampuni ya Puma ni tofauti sana na sisi, ingawa kubadilishana moja mbili siyo vibaya, lakini isiwe watu kumi na kuendelea,” alisema Kaijage.
Uchunguzi wa Mwananchi umeonyesha kuwa wachezaji hao wa Stars wamekuwa hata wakati mwingine wakipigiwa simu wakiwa majumbani kwao ili warudishe jezi ambazo wamekuwa wakiondoka nazo kwa bahati mbaya au ambazo zimekuwa zikipotea.
Ukweli ni kuwa kila mchezaji wa Stars anapopoteza jezi moja hukatwa posho yake kuanzia Sh20,000 na kuendelea.
Hali hiyo ndiyo inayosemekana kuwa itamkumba beki na nahodha msaidizi, Nadir Haroub Cannavaro aliyeamua kubadilisha jezi na Eto’o.
Eto’o, ambaye yuko katika ziara ya nchi kadhaa za Afrika, alionekana jijini Kampala, Uganda akiwa na jezi yenye nembo ya NMB huku akitoa mafunzo ya soka kwa watoto.
Comments
Loading…