*Man City, Arsenal, Man U wapumuliana
*Sunderland wafukuza kocha, QPR hoi
Ushindi wa bao 1-0 wa Liverpool dhidi ya Swansea umefanya mpambano wa kuwania nafasi nne za juu kuwa mkali zaidi.
Kwenda sare kwa Chelsea dhidi ya Southampton mwishoni mwa wiki, mabingwa watetezi, Manchester City kufungwa na Burnley nako kumeweka timu kusogeleana.
Kadhalika ushindi wa Arsenal wa 3-0 dhidi ya West Ham na ushindi wa Manchester United wa 3-0 dhidi ya Tottenham Hotspur nao umeongeza ushindani.
Timu zikiwa zimechea mechi 29, isipokuwa vinara Chelsea wenye pointi 64 na wanaoshika mkia, Leicester wenye pointi 19, kuna kila dalili kwamba atakayeteleza kidogo atajilaumu karibuni.
Man City wanalia kwa kushindwa kupunguza pengo dhidi ya Chelsea na hivyo ubingwa wao kuwa rehani, kwani wamebakiwa na pointi 58, zikiwa ni moja tu zaidi ya Arsenal na mbili tu zaidi ya Man United, huku Liverpool wakifuatia wakiwa na pointi 54.
Southampton na Spurs wanafunga kwa pointi 50, wakifuatiwa na Stoke waliojikusanyia 42, Swansea wana 40 huku 10 bora ikifungwa na West Ham wenye pointi 39.
Katika eneo la kushuka daraja, jahazi linazidi kwenda mrama kwa Leicester, huku Queen Park Rangers nao wakiwa na pointi 22 tu na Burnley wakiwa nazo 25. Sunderland walionyukwa vibaya 4-0 na Aston Villa wamemfukuza kocha wao, Gus Poyet aliyewaokoa kushuka daraja msimu uliopita, na sasa wanazungumza na Dick Advocaat aje kuokoa jahazi lao.
Timu zisizo na shinikizo kubwa kwa kuwa katikati ya msimamo ni Newcastle wenye pointi 35, Crystal Palce 33 sawa na West Bromwich Albion, Everton wana 31 lakini wanaotakiwa kujichunga pia ni Hull na Villa wenye 28 kila mmoja.
Comments
Loading…