“Chuki ya nini mimi siyo mtanzania mbona, nilikosea kucheza timu za Tanzania nini”, maneno ya Fiston Mayele kupitia ukurasa wake wa Instagram ambako alizua taharuki kwa wadau wa michezo baada ya kutupa lawama zake hizo. Mayele alionekana kukerwa na jambo fulani na kuingia ista kisha kuandika ujumbe mzito uliowashangaza watu wengi hususani mashabiki wa Yanga.
KUJIUNGA NA YANGA
Kabla ya sakata lake hilo nikukumbushe safari ya Fiston Mayele kucheza Yanga SC. Ilikuwa Jumamosi ya Julai 31, 2021, Mayele alipotua rasmi nchini kuja kusaini mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo kongwe ya Yanga SC huku akiongozana na meneja wake Nestor Mutuale walipotokea wako nchini DR Congo. Hakuna aliyemjua Mayele kabla ingawa alikuwa na jina tayari kwani alishafanya makubwa pale As Vita Club ya nchini kwao. Septemba 25, 2021 fainali ya Ngao ya Jamii Katika dimba la Benjami Mkapa unaweza kusema ndiyo iliyomtambulisha ramsi Fiston Mayele baada ya kuifunga Simba SC kwa goli safi akipokea pasi nzuri kutoka kwa Farid Musa ndani ya dakika 12 ya mchezo, ndipo hapo akaitambulisha rasmi staili yake ya ushangiliaji iliyompa umaarufu kwa kutetema.
MAFANIKIO YAKE NDANI YA YANGA
Kuisaidia Yanga SC kucheza fainali michuano ya kombe la Shirikisho Afrika, ambapo Yanga SC ilicheza na timu ya USM Alger ya Algeria na kumaliza kwa USM kutwaa Ubingwa huo. Kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara mbili mfurulizo, 2021, 2022 huku Yanga pia ikitwaa Ubingwa mwingine wa Shirikisho la Azam ‘ASFC’. Kwa mantiki hiyo tunaweza kusema, Mayele ndiye mshambuliaji aliyecheza kwa mafanikio makubwa ndani ya kikosi cha Yanga SC kwa msimu wa hivi karibuni.
KUONDOKA YANGA
Mwishoni mwa msimu wa 2022/2023 wa Ligi ndipo safari ya Fiston Mayele ikamalizika ndani ya mabingwa wa tetezi wa Ligi Kuu NBC na yeye kumtikia zake nchini Misri na kujiunga na Klabu ya Pryamids FC. Safari yake hiyo ya yeye kujiunga na Pryamids ni kama imeleta maneno kwani Mayele siyo mara moja kusikika kuwa kuna baadhi ya viongozi wa Yanga wamekuwa wakimlaumu kwanini ameondoka klabuni kwao na kuicha timu huku wakimtaka arejee tena kama watashindwana na wana Farao hao. Yeye mwenyewe amenukuliwa mara kadhaa kwa kauli zake kuwa, hawezi kurejea tena kwa mabingwa hao kwani ni kama hawako naye vizuri.
USHAURI WA MANARA
Aliyewahi kuwa msemaji wa Klabu ya Wekundu wa Msimbazi, Simba SC Kisha baadae kuwa msemaji wa Yanga SC kwa kuwa na ukaribu na mchezaji huyu Fiston Mayele, hakusita kumfuata kwenye ukurasa wake wa Instagram na kumpa ushauri. ” My brother pls futa hii siyo nzuri”. Kisha baadae Mayele akamjibu Manara baada ya andiko lake hilo ambalo alikuja kumundikia kwenye ile post yake kuhusu kuwatuhumu viongozi wa Yanga. ” Manara, naacha sababu napokea meseji na viongozi tena siyo vizuri, mimi nilikuja kutafuta kazi Tanzania kama mtu yoyote anaenda kutafuta kazi, lakini nimechoka mpaka nimeposti jua Bugatti (Manara) na mimi ni binadamu, siwezi kuishi kinafki, mwache maisha yangu nitafute pesa nimechoka na majini wallah’.- maneno ya Mayele. Hata hivyo haikuishia hapo alitaka kuingia ista live ili awataje viongozi hao lakini hakufanya hivyo kama alivyoahidi.
MENEJA APIGA GOTI YANGA
Kauli za Fiston Mayele zilimfanya meneja wake bwana Nestor Mutuale kutoka mbele na kuomba radhi viongozi pamoja na mashabiki, wanachama wa klabu hiyo huku akidai kuwa Kijana wake ameteleza kwa kauli zake. Mutuale aliongeza kuwa, alikaa chini na mchezaji huyo na kuzungumza naye na kutaka kuachana na vitu kama hivyo kwani vinachafua taswira nzima ya soka na kwa kufanya hivyo ni kama kuifunga njia ambayo wao walishaitengeneza.
YANGA NA WA CONGO
Klabu ya Yanga SC tangu kuanzishwa kwake imekuwa na mahusiano mazuri na wachezaji kutoka DR Congo. Utakumbuka vizuri miaka ya 90, liliwahi kupita jina la mchezaji aliyecheza kwa mafanikio makubwa tena Bara la Ulaya, Shaban Christophe Nonda hili siyo jina geni kwako mchezaji aliyevichezea vilabu kama, Vaal Professional FC, Zurich, Rennes, Monaco, Roma, Blackburn Rovers na baadae kumalizia pale Galatasaray mwaka 2010. Wachezaji wengine ni kama, Banza Tshikala, Petch Kongo, Delo Ntumba Patrick Katalay, Sadic Kalokola, Laurent Kabanda, Sambitumba Iyela. Wote hao walikipigwa na Yanga SC.
TETESI ZA USAJILI
Ipo minong’ono kuwa Mchezaji Fiston Kalala Mayele tayari vilabu kutoka nchini vya Simba na Azam FC kuitaka saini yake, taarifa hizo zinakuja baada ya kusemekana kuwa, Mayele hayafurahii sana maisha ya Pyramids na kudai kutaka kuondoka na hii ndio kupelekea kuzua vuguvugu kubwa kwa wadau wa soka nchini.