Nyota wa zamani wa soka nchini leo wanatarajia kufanya matembezi ya hisani kwa ajili ya kukusanya fedha za kumsaidia nyota wenzao, Jella Matagwa anayesumbuliwa na maradhi ya kupooza.
Matembezi hayo ya kumchangia Mtagwa aliyewahi kuwika na timu za Yanga, Pan Afrika na Taifa Stars, yamepangwa kuanzia Magomeni na kumalizika kwenye Hoteli ya Friend’s Corner, Manzese ambapo ndipo watakapoukabidhi msaada huo.
Akizungumza jana jijini Dar, Mratibu wa Matembezi hayo, Paul Lusozi ‘Father’, alisema zaidi ya nyota 40 wa zamani na wa sasa watashiriki katika matembezi hayo.
“Tunashukuru wengi wamethibitisha kushiriki matembezi haya, kwa kweli ndugu yetu (Mtagwa) anahitaji msaada kutokana na hali yake ya kupooza mwili, tumepanga kukutana kwenye hoteli hiyo na kukabidhi msaada wetu kwa kuwa nyumba yake ipo karibu na eneo hilo,” alisema Lusozi.
Kwa mujibu wa Lusozi, msaada watakaoukabidhi kwa Mtagwa ni pamoja na fedha taslimu kwa ajili ya kumsaidia kwenye matibabu yake na familia yake kwa ujumla.
Aidha, alisema kuna haja kwa serikali kuwatafuta na kuwasaidia wachezaji wenye matatizo kama akina Mtwaga ambao walijitolea kulisaidia taifa enzi zao.
Alisema, wachezaji wa zamani waliweka mbele uzalendo na maslahi ya taifa mbele tofauti na ilivyo sasa ambapo soka limekuwa biashara, hivyo kuwafanya waishi maisha duni.
Alisema mpango wa kuwakumbuka wachezaji wa zamani wenye matatizo mbalimbali unatarajiwa kuendelea kufanywa jijini Arusha kumchangia fedha Alain Shomari anayesumbuliwa na tatizo la macho na Badi Saleh aliyekatwa mguu kutokana na tatizo la maradhi ya kisukari anayeishi Sinza, Dar.
Comments
Loading…