UZALENDO ni miongoni mwa sababu zinasochangia mashirikisho ya soka kote duniani kuchukua hatua kali za kutunga kanuni na taratibu za kuongoza Ligi zao. Kila Ligi Kuu hapa duniani kuna masharti ambayo yanatumika ili kulinda vipaji vya wachezaji wazawa pamoja na kuinua viwango vyao katika usakataji wa kandanda. TANZANIASPORTS inachambua mmojawapo ya masharti mapya ya Ligi Kuu Tanzania kuanzia msimu ujao 2025/2026. Msingi wa masharti hayo umejengwa katika uzalendo ambao unatarajia kulinda wachezaji wa Kitanzania, pamoja na kuwapa nafasi ya kuonesha uwezo wao. Sharti hilo limetolewa na Ris wa TFF, Wallace Karia hivi karibuni ambalo limekuwa gumzo miongoni mwa wadau wa soka nchini.
Je Rais wa TFF alisema nini?
Akizungumza kwenye kipindi kimoja cha redio nchini Tanzania, Rais wa Shirikisho la Soka, TFF, Wallace Karia amebainisha kuja na masharti mapya ambayo yataboresha Ligi Kuu pamoja na kuinua hali ya viwango vya wachezaji wazawa hasa eneo la golikipa. “Kuanzia msimu ujao tunakuja na kanuni ya golikipa mmoja tu wa kigeni kwenye kila timu, haiwezekani kwenye timu moja kuwe na magolikipa wawili wa kigeni haiwezekani hii. Nilikuwa namtania Rais mwenzangu wa shirikisho la soka, aliniambia mbona kwenye Ligi yako kuna wachezaji wa kigeni wengi sana, nikamjibu kuwa siwadekezi watu wavivu, ukiangalia pale Yanga kuna mabeki wengi wazawa ndiyo wanacheza hata Simba pia hivyo hivyo,”. Katika mazungumzo hayo na kipindi cha Jana na Leo, Rais Karia alionesha wazi kuwa umefika wakati kuwaambia wachezaji wa Kitanzania kupigania uwezo wao kuliko kutegemea hisani kwa kigezo cha uzawa.
Timu mbalimbali zimekuwa na makipa wa kigeni ambao wameongeza chachu ya ushindani na ubora wa Ligi Kuu. Simba wanaye golikipa mahiri Moussa Camara, hali kadhalika Yanga wanaye Djigui Diarra. Makipa hawa wameonesha viwnago vya juu na wanastahili kutunzwa kama lulu kwenye Ligi hii. Katika klabu ya Simba ilijikuta kuwa na makipa wawili wa kigeni, Ayoub Lakred na Mousa Camara, pamoja nawazawa wawili Ali Salim na Aishi Manula. Wakati Yanga wanaye Abdultwalib Msheri, Khomein na Diarra.
Je ni nchi gani inafuata sharti hilo?
Misri ndiyo nchi ambayo inaweza kutumika kama shamba darasa kwenye masharti ya wachezaji wa Ligi Kuu yao. shirikisho la Soka nchini Misri lina sharti moja muhimu kwa timu zinazoshiriki Ligi hiyo. Sharti hilo linahusiana na nafasi ya golikipa. Timu zote zinatakiwa kutekeleza masharti ya kikanuni ya kusajili golikipa mzawa. Katika Ligi ya Misri hakuna timu inayoruhusiwa kusajili golikipa wa kigeni, badala yake wote wanatakiwa kuwa wazawa. Uamuzi wa shirikisho la soka la Misri, ulikuja kutokana na ushauri walioipewa na aliyekuwa kocha wa timu ya Taifa ya nchi hiyo, Hassan Shehata. Kocha huyo aligundua kuwa uhaba wa magolikipa wazawa pale ambapo nchi nzima ilikuwa ikimtegemea El Hadary pekee kama mlindamlango mahiri wa Timu ya Taifa. Hakukuwa na namna nyingine zaidi ya kuweka sharti hilo ili kuibua vipaji vya magolikipa wazawa. Hata kama hawakuwa na kiwnago kama El Hadary lakini palitakiwa kuwa na uwingi wa wachezaji wa nafasi hiyo katika Ligi yao. Misri imetutangulia kimaendeleo ya soka, lakini masharti yao ni vyema yakaigwa.
Umuhimu wa makipa wa kigeni
Uamuzi wa TFF kuja na sharti hilo la kusajili golikipa mmoja wa kigeni ni mzuri na unawezesha wazawa kupata nafasi mbili; kwanza wazawa watakuwa na uhakika wa kupata nafasi ya kucheza pale golikipa namba moja akiwa mgeni anapoumia au kupumzishwa. Pili, wazawa watajifunza mbinu mpya kutoka kwa makipa wa kigeni ambao wanatokea katika utamaduni mwingine. Kwa mfano ujio wa kigeni Djigui Diarra na Moussa Camara ni magolikipa wa viwango vya juu sana kuwahi kutokea hapa nchini. Ligi Kuu Tanzania inapaswa kujivunia kuwa na makipa hawa ambao wanaonesha na kufundisha namna bora ya kuwa golikipa wa mifumo ya kisasa. Makipa hawa wanatuma ujumbe muhimu kwa wachezaji wazawa wa nafasi hiyo. Ni muhimu TFF itakambua pia makipa hawa wanatoka kwenye nchi zilizotutangulia kiamendeleo au wanatoka katika mifumo ambayo imewajenge ubora hivyo kuwa walimu wa uwanjani wa makipa wengi wa Kitanzania. Wakati sharti hilo likiwekwa kuanzia msimu ujao, ni muhimu kuwa na mtazamo chanya kuliko hasi peke.
Mpango mpya TFF, Vilabu
Baada ya kutoa sharti hilo ambalo litatumika kuanzia msimu ujao, ni wazi shirikisho la soka la TFF linatakiwa kuandaa mpango wa kudumu kuhusu nafasi ya golikipa. Uamuzi wa kusajili kipa mmoja ni mzuri sana kuliko kufuta kabisa. Sharti hilo lina maana TFF na vilabu vinatakiwa kuzalisha makipa wenye viwnago. Ni jukumu la wadau kuhakikisha wanalea na kuibua makipa wenye vipaji vya hali ya juu ili kuziba pengo la kipa wa pili wa kigeni ambaye hataruhusiwa kucheza nchi. Sharti hilo liendane na mpango madhubuti wa kuimarisha eneo la golikipa kupitia vituo mbalimbali vya soka vilivyoko nchini. Kwa pamoja tunaweza kukamilisha hili.
Comments
Loading…