*Pia marufuku wanaofanya mapenzi jinsia moja
Mashabiki wa klabu maarufu ya Urusi, Zenit St Petersburg wamezua mtafaruku kw a kuwakataa wachezaji weusi na wale wanaofanya mapenzi ya jinsia moja.
Washabiki hao wenye kundi linaloitwa ‘Landscrona’ wametaka uongozi wa klabu kuchukua hatua mara moja, kuhakikisha wachezaji wanaibaki kwenye timu ni weupe tupu na wasiofanya mapenzi ya jinsia moja.
Hatua hiyo imeushitua ulimwengu wa kandanda, kwa sababu Urusi ndiyo inaandaa mashindano ya Kombe la Dunia kwa mwaka 2018.
Landscrona ndilo kundi kubwa zaidi la mashabiki wa klabu hiyo nchini Urusi, na madai ya kuwakataa ni kwamba weusi wanaiangusha klabu na wanaofanya mapenzi ya jinsia moja hawastahili kuwa katika jiji lao maarufu.
Uongozi wa Zenit iliyoanzishwa mwaka 1925 umetoa taarifa ya kuwakana washabiki hao, na kutupilia mbali matakwa hayo.
Kocha Mkuu wa Zenit, Luciano Spalletti, amezungumza bila kulitaja kundi hilo, akisema anaamini kwamba uvumilivu ndilo jambo muhimu zaidi katika kukubali tofauti zilizopo
“Zaidi ya hapo, kuwa mvumilivu kunamaanisha kupambana na kila aina ya ujinga,” akasema kocha huyo Mtaliano.
Klabu hiyo inayomilikiwa na kampuni kubwa ya gesi ya serikali, Gazprom, imetoa taarifa kwamba husajili wachezaji kwa kuzingatia uwezo wao pekee.
Kwamba sera ya timu yao ni katika maendeleo na kuunganisha jamii katika ulimwengu wa soka.
Zenit ilikuwa klabu pekee kubwa Urusi ambayo haikuwa na mchezaji mweusi, hadi majira ya kiangazi mwaka huu ilipomsajili mshambuliaji wa Brazili, Hulk na kiungo Mbelgiji, Axel Witsel kwa Euro milioni 80.
Zenit walimwinda na kutaka kumnasa kiungo Mfaransa, Yann M’Vila, lakini alikataa kuhamia Urusi Agosti mwaka huu, baada ya kupokea vitisho vya kuuawa.
Hata hivyo, washabiki hao wa Zenit wamesisitiza katika shinikizo lao kwamba wao si wabaguzi, bali kutokuwa na wachezaji weusi ni jadi yao, na ndiyo alama ya timu yao.
Urusi imekuwa ikijaribu kupambana na ubaguzi na machafuko kwenye viwanja vyake vya mpira, inapoelekea kuandaa michuano hiyo ya Kombe la Dunia ya mwaka 2018.
Imekuwa kawaida kwa wachezaji weusi kufanyiwa ishara za nyani. Walengwa wa vitendo hivyo ni pamoja na Robert Carlos na Christopher Samba wa
Anzhi Makhachkala waliopata kurushiwa ndizi na washabiki.
Ni mara chache, hata hivyo, waamuzi wameonesha dhamira ya kukabili ubaguzi mchezoni. Washabiki wa Lokomotiv Moscow mwaka 2010 ‘waliishukuru’ England kwa kumsajili mchezaji wao, Peter Odemwingie, wakabeba na picha za ndizi.
Wakati huo, kiongozi wa kampeni za Urusi kuwania kuandaa kombe la dunia alidai ndizi zilikuwa ishara ya kufeli mtihani, na si ubaguzi kwa Odwmwingie.
Hata hivyo, washabiki wa Zenit wamedhihirika wazi kuwa wabaguzi, na hata kocha wa zamani wa klabu hiyo, Dick Advocaat anakiri washabiki hawapendi wachezaji weusi, ndiyo maana hakusajili hata mmoja.
Wachezaji weusi wenyewe wanakiri kwamba washabiki wa Zenit ni wabaguzi. Mmoja ni mfungaji bora wa zamani wa Urusi, Vagner Love na Serge Branco.
Waziri Mkuu wa Urusi, Dmitry Medvedev ambaye ni shabiki wa Zenit pia, ametoa mwito kwa mashabiki wakorofi na wenye fuj kupigwa marufuku kuhudhuria mechi.
Comments
Loading…