in , , ,

Marcus Rashford ni mwisho wa enzi?


Mshambuliaji namba moja kwa muda mrefu wa Man United, Marcus Rashford ana umri wa miaka 27 sasa. Anapokea kitita cha pauni 320,000 kwa wiki kutoka vitabu vya uhasibu vya Man United. Tangu akiwa kinda amekuwa akitabiriwa kuwa mshambuliaji bora na pengine angefikia ubora wa kupchika mabao kama wa Dwight Yorke au Andy Cole mastaa wa zamani wa klabu hiyo.


Wengine walitabiri alipokuwa kinda angeweza kuwafunika wakongwe kama Wayne Rooney, Ruud Van Nistelrooy, Robin van Persie na wengineo. Kila msimu matumaini yamekuwa makubwa kwa mshambuliaji huyo. Msimu uliopita akiwa chini ya kocha Eric Ten Hag alipachika mabao 30 katika mashindano yote. Lakini hakuonesha umahiri zaidi kipindi hicho na hakukuwa na dalili kwa nyota huyo kuzitafuta rekodi za wakongwe.


Chini ya kocha mpya Ruben Amorim, hali ya mambo imekuwa tofauti. Wikiendi iliyopita kuelekea mchezo dhidi ya watani wa jadi Man City Rashford aliachwa kikosini. Hakusafiri na timu kwenda dimbani, hivyo alishuhudia mchezo huo akiwa nyumbani. Si yeye pekee, winga Alejandro Garanacho naye aliachwa kikosini hivyo akabaki nyumbani. Nini kimetokea katika kipaji cha nyoita huyo? TANZANIASPORTS inachambua kwa kina uimara na udhaifu wake.


Je kwanini kocha Amorim alimtema kikosini?


Uamuzi wa kocha kumtema mchezaji unaumiza, si kwake pekee hata wadau wake kwa maana ya menejimenti mzima. Lakini Marucs Rashford kama mchezaji anawajibika kupokea maelekezo ya kocha wake. “ninafuatilia kila kitu kuhusu mchezaji, namna anavyotembea, hulka yake, anavyokula,kushirikiana na wenzake, na jitihada zake mazoezini,” alisema kocha Amorim kwenye mahojiano na vyombo vya habari baada ya mchezo wa watani wa jadi.


Lakini kocha huyo aliendelea kwa kusema, “mchezo uliopita umepita, sasa ni wiki nyingine, wakati mwingine, maisha mapya na mchezo mwingine, Marcus Rashford ana kipaji na tutakuwa sote mazoezini,”. Mbali ya maelezo hayo, uchezaji wa Rashford hauridhishi. Ni mshambuliaji aliyeko kwenye timu kubwa, mifumo inambeba na kumpa nafasi ya kucheza. Makocha wamefika na kuondoka lakini Marcus Rashford hajawahi kuimarika. Kadiri siku zinavyokwenda amekuwa akidumaa zaidi. Hata kama uamuzi wa kocha wake unamuumiza lakini lazima dunia iambiwe juu ya mshambuliaji kama anaweza kuleta matunda kikosini ama aachwe aende zake.


Kwa upande wake Marcus Rashford amekaririwa na vyombo vya habari akisema yuko tayari kwa changamoto mpya. Kauli hiyo pia imchukuliwa na kocha wake kama kosa, kwani alitakiwa kumshirikisha kwanza. Hata hivyo Rashford hajamaanisha changamoto mpya ya kuhama bali kupambana chini ya kocha mpya. Hiyo ndiyo changamoto inayomkabili.


Rashford anafaa kucheza namba ngapi kiwanjani?


Hili ni swali ambalo wasomaji inabidi kushiriki kulijibu. Wamepita makocha wakubw akama Louis van Gaal, Jose Mourinho, Eric Ten Hag na Ole Gunnar Solskjaer lakini Rashford hajawahi kuwa hata mfungaji bora wa msimu. Katika maisha yake ya soka pale Man United si mshambuliaji wa kutegemea aweze kupachika mabao 20 ya EPL kwa msimu.


Aina ya uchezaji wake anaonekana kama vile anafaa nambari 9, wakati mwingine anapangwa nyuma ya mshambuliaji yaani namba kumi. Pia anaweza kutumika kama winga wa kulia (namba 7) na winga wa kushoto (namba 11). Hizo ni nafasi ambazo anacheza, lakini hajawahi kufanyia kazi kwa ufasaha.
Mara kadhaa amepangwa winga wa kushoto ili kumpa nafasi ya kuingia eneo la hatari, lakini matokeo yake si makubwa. Pia amepangwa nambari 9 kama mshambuliaji wa mwisho na mwenye jukumu la kupachika mabao, nako hajafanya kazi yake kwa umahiri ndiyo maana hana rekodi ya kuwa mfungaji bora wa msimu. Nafasi zote hizo hajazitendea haki, pia upotezaji wa mipira kirahisi na kushindwa kucheza kitimu.


Ana nini katika kipaji chake?


Kiufundi Rashford anaonekana kama mchezaji ambaye anapaswa kutengenezewa timu. Yaani timu icheze kulingana na matakwa yake, imzunguke yeye na kumfanya staa wao. Ni mchezaji ambaye miguu yake inaweza kupiga mashuti,kutoa pasi vizuri na kusaidia baadhi ya majukumu eneo la ushambuliaji. Kipaji chake kinaweza kumshawishi kocha atamani kujenga timu kupitia yeye, lakini makocha kadhaa wamejaribu pasipo mafanikio hadi sasa Amorim ameamua kufyatua bomu juu ya huduma ya mchezaji huyo.


Je udhaifu wake ni upi?


Kama mshambuliaji anatakiwa kupambana na walinzi wa timu pinzani. Jukumu hilo linamfanya awe na maamuzi ya kutafuta nafasi za kupita na kuwahadaa wapinzani wake. Changamoto iliyopo ni kwamba uwezo wake wa kufanya maamuzi ni hafifu. Matukio kadhaa yameonesha namna anavyokosa ule uhodari wa kufanya maamuzi kwenye majukumu yake dhidi ya wapinzani. Katika soka, kwenye nafasi ya mwisho ya kufunga mabao inahitaji mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa wa kukabiliana na walinzi pamoja na ufanyaji wa maamuzi. Amebarikiwa uwezo wa kutumia miguu yote miwili lakini akili ya Rashford haifanyi uamuzi mzuri kwa maslahi ya timu.


Kwanini Man United wamemlinda Rashford?


Kwanza kwa upande mwingine Rashford anabaki kuwa mtu muhimu kwa serikali ya Uingereza kutokana na mchango wake katika kipindi na ugonjwa wa corona. Rashford anaheshimika serikalini lakini kwenye kazi yake uwanjani kila kukicha umahiri wake unadidimia. Kila uamuzi anaofanya haonekani kutaka kufanya kitu cha ziada. Ni kama amekosa ile ari au njaa ya mafanikio huku vitabu vya wahasibu vikionesha malipo manono kila wiki.
Man United kama zilivyo klabu nyingine zinapenda kuwalinda wachezaji wao waliokulia kwenye akademi zao. Hata kama Man United wataamua kumuuza leo mfano kwa pauni Milioni 40, fedha zote zitakwenda klabuni kwa sababu ndiko alikokulia na sheria inawalinda. Vilevile kumlinda mchezaji aliyekulia klabuni ni kutengeneza taswira chanya kwa makinda walioko akademi, wakimtazama kama mfano wao wa kuigwa. Hii ni sababu muhimu kuchochea ari za wachezaji wa akademi.


Mbio nyingi,mpira mwingi


Kama kuna jambo linaloweza kumwondoa Rashford pale Olt Traford basi ni mbinu za kocha Ruben Amorim. Falsafa ya kocha huyo inawataka wachezaji ambao watakimbia kwa muda mrefu (intensity) pamoja na kucheza mpira mwingi mno.
Kasi ya uchezaji inabadilika ndiyo maana baadhi ya wachezaji wamekuwa wakifurahia soka lao sasa akiwemo Amad Diallo, Mazroui,Lisandro Lopez, Antony na wengineo. Uchezaji wa kasi unapaswa kumwamsha Rashford na kutambua zama zimebadilika, kama anataka kubaki kikosi cha kwanza basi anapaswa kubadilika. Kinyume chake itakuwa hasara kwa kipaji chake na kumwona akiondoka timu kubwa kama Man United kisha akaishia kwenye klabu zinazopigania kutoshuka daraja. Kupanga ni kuchagua.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Navutiwa Na Ligi Kuu Ya NBC Msimu Huu